Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati umefika kwa wananchi wa Kiwani kuchagua viongozi wanaoweza kuwatumikia na kuwaletea maendeleo jimboni humo.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipozungumza na kuomba kura kwa wananchi wa vijiji vya Kendwa, Kirimdomo,Vizuke, Kichaka na Chwaka.
Amesema amekusudia kuimarisha zaidi huduma za kijamii katika jimbo la kiwani ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa na vituo vya Afya vitakavyotoa huduma zote za matibabu na vipimo bure pamoja na kusimamia suala zima la nidhamu kwa madaktari na wahudumu wa Afya ili wananchi waweze kupata huduma za matibabu kwa uangalizi kwa nidhamu ya hali ya juu.
Amesema azma yake ni kuhakikisha wajasiriamali na wenye vikundi vya ushirika watapatiwa mitaji, elimu ya ujasiriamali na mikopo isiyo na riba ili kukuza biashara zao pamoja kutafutiwa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi ili kuwa na uhaki wa kuuza biashara zao.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amesema akichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Jimbo la kiwani atajenga soko kubwa la kisasa katika kijiji cha Kendwa ambalo litatoa fursa kwa wafanyabisha wa kijiji hicho na vijiji jirani kufanya biashara zao katika mazingira mazuri na salama.
Ndugu Hemed amewaahidi wananchi wa Kiwani kujengwa kituo cha Zimamoto na Uokozi jimboni humo pamoja na wananchi kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa kujikinga na majanga mbali mbali yanapojitokeza jambo litakalookoa maisha ya watu na mali zao.
Akizungumzia Sekta ya elimu Mhe. Hemed amefahamisha kuwa ndani ya Jimbo la Kiwani skuli za ghorofa za msingi na Sekondari zimejengwa, ongezeko la madarasa katika skuli mbali mbali, ujenzi wa dakhalia za wanafunzi wasichana na wavulana pamoja na ujenzi wa nyumba za kuishi walimu jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa ufauli jimboni humo.
Amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake watahakikisha gharama zote za masomo na dakhali kwa wanafunzi wa Kiwani zitagharamiwa na viongozi wa jimbo ili kuwapunguzi ukali wa maisha wazazi wenye wanafunzi wanaosoma mbali na maeneo yao wanayoishi.
Mhe. Hemed ameahidi kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kupatiwa huduma zote muhimu watoto wenye uhitaji maalum na mayatima waliomo ndani ya jimbo la kiwani ambapo amewataka wazazi na walezi wenye watoto hao kuacha tabia ya kuwafungia ndani na kuwakosesha fursa zao za msingi wakiona ni mzigo kwao.
Amefahamisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami unaendelea katika vijiji mbali mbali ambazo watahakikisha barabara zote za kiwani zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kutoa fursa ya kukuza harakati za kiuchumi ndani ya jimbo hilo.
Amesema atahakikisha anaiondoa kabisa changamoto ya maji safi na salama kwa kuhakikisha anachomba kisima kila penye uhitaji wa huduma hio pamoja na kujengwa kwa matenki makubwa ya kuhifadhia maji ambayo yatasambaza huduma ya maji katika vijiji vyote vilivyomo jimboni humo.
Ametumia fursa hio kwa kuwaomba kura wananchi wa vijiji vya Kendwa, Kirimdomo,Vizuke, Kichaka na Chwaka wa Jimbo la kiwani ili aendele kuwatumikia kwa uwanifu mkubwa na kuweza kutimiza adhma yake ya kuiona kiwani yenye maendeleo.
Wakizungumza kwa niaba ya wazee wa vijiji hivyo Bwana Omar Talib na Mzee Sultan Omar Mjawiri wamewaomba wagombea hao watakaposhinda kuwasaidia katika suala zima la kupatiwa mikopo ili kuweza kuendeleza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.
Aidha wamesema msikiti wao wanaofanyia Ibada umekuwa mdogo kutokana na ongezeko la waumini wanaofanya ibada katika msikiti huo hivyo wameomba kusaidiwa kupata msikiti unaokidhi pamoja na madrasa kwa ajili ya kusomea watoti Qur-an ili kuwajenga na kuwakuza katika misingi ya dini na Imani.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Tarehe 20 / 10 / 2025.
No comments:
Post a Comment