Habari za Punde

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Yaridhishwa na Maandalizi ya Uchaguzi Pemba

 

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefanya ziara kisiwani Pemba kukagua maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika Afisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya ya Chake Chake, Micheweni, Mkoani na Wete.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Jaji George J. Kazi, alisema kuwa Tume imeridhika na hali ya maandalizi ilivyo katika wilaya zote, akibainisha kuwa vifaa vya uchaguzi, miundombinu na mazingira ya kazi kuelekea katika Uchaguzi Mkuu 2025 yako katika hatua nzuri.

"katika ziara hii nimeridhika kwamba kwa asilimia zaidi ya 90 vifaa vyote kwaajili ya Uchaguzi Mkuu vipo katika maghala na kwa asilimia chini ya 10 kwa vifaa ambavyo hatujavikamilisha vipo mbioni kuvikamilisha kwa mujibu wa mpango kazi wetu kabla ya tarehe 20 Oktoba vifaa vyote vitakuwa vimeshasambazwa" alisema Jaji Kazi.

Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuatilia hatua kwa hatua maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025 katika Wilaya zote kumi na moja kwa Unguja na Pemba.

Mhe.George J. Kazi ameendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi siku ya tarehe 29 Oktoba 2025 kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa maandalizi yote yanakwenda kwa mujibu wa mpango kazi  uliowekwa.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.