Na
Mwantanga Ame
BAADA
ya serikali kukabidhiwa ripoti ya Kamati teule ya Baraza la Wawakilishi,
iliyochunguza mambo mbali mbali yaliyoibuka kwenye majadiliano ya
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, ameahidi kuwachukulia hatua watu
waliotajwa ndani ya ripoti hiyo baada ya kufuja mali ya umma.
Dk. Shein, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na
Waandishi wa Habari huko katika Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya utaratibu
wake aliojiwekea wa kuzungumza na Wananchi kila baada ya mienzi mitatu.
Alisema tayari ripoti hiyo imepokelewa na serikali lakini
inalazimika kuridhiwa kwa ajili ya kuwachukulia hatua watu waliotajwa ndani ya
ripoti hiyo kama tuhuma zilizo juu yao.
Alisema kama serikali ina njia zake za kupita katika
kulifanyia kazi suala hilo ni lazima zifuatwe na si vyema kukurupa bila ya kufanya utafiti kwa kuwa
ripoti hiyo inaelezea mambo mengi.
Alisema kama yeye ndio kiongozi wa nchi hatoacha
kuwawajibisha watumishi watakaowaona kuwa wanastahiki kufanyiwa hivyo kwani
nchi ni lazima suala la utawala bora ni moja ya jambo la msingi ambalo
linalazimika kulisimamia.
Alisema ni kweli Chama cha Mapinduzi, kilitoa tamko la
kutaka kuwawajibishwa watu waliotajwa kufuja mali ya umma katika Serikali ya
Muungano, lakini kabla ya kufanya hivyo serikali ilipata nafasi ya kujiridhisha
na uchunguzi uliofanywa kwa Mawaziri waliotajwa kuhusika na masuala hayo.
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein, alisema na serikali ya
Zanzibar kwa kufuata mfumo huo wa ndani ya Chama cha Mapinduzi atahakikisha
kazi hiyo inatekelezwa bila ya kumuonea mtu ambapo wakati ukifika jamii
itaelezwa bayana.
“Taarifa imeletwa kuna taratibu tunazifanya kama serikali
hakutakuwa na siri mtayasikia wakati wa kufanya maamuzi hata Serikali ya
Muungano iliyapima mwisho nasi tutaamua wakati ukifika,” alisema Dk. Shein.
Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa Nne wa Baraza la Wawakilishi ambao
ulikuwa maalum kwa ajili ya Bajeti,
Baraza hilo liliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi
kuchunguza mambo mbali mbali.
Matokeo ya
Kamati hiyo iliyoifanya kazi hiyo chini ya hadidu rejea saba imetoa mapendekezo
mbali mbali huku ikiwataja baadhi ya Mawaziri waliopo madarakani kuhusika na
matukio mbali mbali ya uharibifu wa mali za umma.
Baadhi ya
mapendekezo hayo kwa Idara ya Mrajis serikali imetakiwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Wananchi wote waliohusika katika
udanganyifu uliojitokeza katika Upatikanaji wa Mikataba ya Mauziano kutoka
katika Mamlaka ya Serikali na kumuuzia Juma Ali Kidawa na mauziano baina ya
Juma Ali Kidawa na Amina Aman Abeid Karume.
Aidha Kamati hiyo imeagiza zichukuliwe kwa watendaji wakuu wa Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati waliohusika na upatikanaji wa Mkataba wa
Mauziano ya Nyumba Namba 755/56 kwa thamani ya shilingi. 5,000,000/- baina ya
Wizara hii na Kidawa pamoja na Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali walioshiriki
katika upatikanaji wa Mkataba wa Mauziano hayo.
Watu wengine waliotajwa kutaka kuchukuliwa hatua ndani ya ripoti hiyo ni
pamoja na Viongozi na Watendaji wote waliohusika na kadhia ujenzi wa jengo
jipya la Wizara ya Fedha, Pemba wawajibishwe kisheria, kwa sababu
imethibitika kwamba, Wizara ya Rais,
Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo imechangia kutokezea kwa tatizo la
kujengwa jengo hilo chini ya kiwango.
Hali hiyo imeelezwa na ripoti hiyo ilitokea baada watendaji waliosimamia
hilo kushindwa kufuata taratibu za Sheria ya Manunuzi na Ugavi wa Mali za
Serikali , Namba 9 ya mwaka 2005, katika kumtafura Mjenzi wa Jengo la Ofisi ya
Wizara.
Kamati hiyo pia imependekeza Viongozi na Watendaji Wakuu
wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora waliohusika na kadhia kufanya ajira katika Wizara ya Mawasiliano
baada ya kudaiwa kuwapa jamaa zao wawajibishwe kisheria.
Pendekezo jengine lililotolewa
na kamati hiyo ni hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe kwa Watendaji
Wakuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mamlaka ya Uwanja wa
Ndege waliohusika na upotoshaji wa Kamati kwa kutoa taarifa zisizo za kweli.
Vile vile kamati hiyo imeagiza hatua za kinidhamu
zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika na uzembe wa ununuzi wa jenereta
hilo, huku msisitizo ukiwekwa kwa Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais, Fedha,
Uchumi na Mipango ya Maendeleo na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano;
Mkurugenzi na Meneja wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege.
No comments:
Post a Comment