Na Asya Hassan
CHAMA cha CUF kimesema kimepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa
ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho,Musobi Mageni Musobi
kilichotokea Mei 30 mwaka huu.
Taarifa kutok a Makao Makuu ya CUF Mtendeni Zanzibar imesema Musobi ambaye
ameugua kwa muda mrefu alifariki majira ya saa 2:00 usiku nyumbani kwake, Ngudu
wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na chama hicho kupitia vyombo vya
habari, zimesema Chama hicho kimesema kimepokea kwa huzuni msiba wa kiongozi
huyo shupavu,ambaye alibeba jukumu la uongozi,wakati mgumu chini ya misingi ya
nidhamu,umoja,uwazi,uadilifu na demokrasia ya kweli.
Taarifa hiyo ilisema kuwa marehemu huyo alikiongoza chama hicho akiwa
mwenyekiti wa pili tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo Julai 13, 1995 nafasi
ambayo aliitumikia hadi kustaafu kwake Disemba 1999.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa pamoja na uongozi huo pia Mwenyekiti huyo
katika uhai wake aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi,ikiwa ni pamoja
na Waziri wa Ardhi,nyumba na Maendeleo ya Miji ya Serikali ya awamu ya kwanza
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ambapo aliongoza kuanzia mwaka 1972 hadi
1975.
Chama cha CUF kwa niaba ya watendaji,wanachama,wafuasi na wapenzi
wake,wakiwemo wilaya zote 10 na majimbo yote 50 ya uchaguzi na matawi ya Zanzibar
wanatoa salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa chama Taifa, Profesa Ibrahim
Haruna Lipumba pamoja na familia ya marehemu na kushikamana nao wakati huu
mgumu wa msiba.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa maziko ya marehemu huyo yanatarajiwa
kufanyika Jumatatu Juni 4 mwaka huu kijijini kwake Ngudu,ambapo marehemu huyo
amezaliwa, Aprili 1, 1931,marehemu huyo ameacha vizuka wawili,watoto 15 na
wajukuu kadhaa,Mungu amlaze mahala pema peponi.
No comments:
Post a Comment