Habari za Punde

Watoto 10 Wafariki kwa Matumbo ya Kuharisha



Na Asya Hassan

WATOTO 10 wamefariki dunia kwa maradhi ya matumbo ya kuharisha wakipatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katibu wa hospitali ya Mnazi mmoja, Dk. Omar Abdalla, alisema kuwa idadi hiyo ya vifo imeripotiwa ndani ya mwezi uliopita baada ya kuongezeka kwa maradhi ya matumbo ya kuharisha kwa watoto kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Katibu huyo alisema kuwa chanzo cha maradhi hayo kinasababishwa na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar.


Alisema  wananchi wa Zanzibar hawana utamaduni wa kuchemsha maji, kusafisha mazingira yao wanayoishi pamoja na kunawa mikono mara kwa mara hivyo, jambo linalopelekea mripuko wa maradhi hayo hasa kwa watoto.

Katibu huyo alifahamisha kuwa ugonjwa uliopo hivi sasa ni matumbo ya kuharisha na sio kipindupindu ambapo watoto ndio waathirika wakubwa wa maradhi hayo kutokana na idadi ya wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo idadi kubwa ni watoto.

Katibu Omar, alisema kutokana na idadi ya watoto kuwa ipo juu kwa kuathirika na maradhi hayo ipo haja kwa wazazi kuchukuwa juhudi za makusudi za kuwadhibiti watoto hao kutochezea maji machafu yanayo toka katika makaro pamoja na kuwepo kwa mvua zinazoendelea kunyesha.

"Wananchi wa Zanzibar hatuna tabia ya kusafisha mazingira yetu,hatuchemshi maji na watoto wetu tunawaacha wanacheza katika mazingira ambayo hayaridhishi,wanacheza katika maji machafu ambayo yanatoka katika karo,ndio maana watoto wengi wameathirika na matumbo ya kuharisha na kupelekea kupoteza maisha,"alisema.

Kwa upande wa Muuguzi dhamana wodi ya watoto, Khadija Muombwa Ame, alisema mwezi uliopita, idadi ya watoto walipokelewa kwa wingi katika wodi yao kwa siku imeongezeka na kufika watoto kumi hadi 15 huku ikiwa hakueleza kuwa ni jumla ya wagonjwa wangapi wamepokewa hospitalini hapo.

Alisema wagonjwa hao wanatoka katika sehemu mbali mbali za mjini na mashamba Unguja na kusema kuwa watoto wanaofika hapo wengi wao ni chini ya umri wa miaka miwili.

"Siku za nyuma tulikuwa tunapokea wagonjwa wa aina hii lakini idadi yao ilikuwa ndogo sana, toka kuanza kwa mwezi wa tano idadi imekuwa kubwa sana kwani watoto kumi hadi 15, hali inatisha na watoto wenyewe wadogo ambao hawajui wajikinge vipi,hivyo wazazi wawe na tahadhari juu ya hili,"alisema.

Muuguzi huyo akizungumzia juu ya dawa wanazotumia katika kipindi hicho alisema dawa zinakuwepo na ikiwa hawana wanamuandikia mwenyewe mgonjwa na kwenda kununua nje,hivyo hakuna msaada wa aina yoyote juu ya dawa wanazotumia kwa maradhi hayo.

Khadija alisema ni vizuri kwa wazazi kuchukuwa tahadhari kwa watoto hao pale wanapowakuta kuanza dalili hizo kwa kuwachemshia maji na kutia chumvi ili kunusuru pomoja na kudhibiti hali hii.

Kwa upande wa mdhamini wa wodi ya watoto wa kiume, Raya Nassor Issa, alisema hali ya wagonjwa kwa mwezi wa Mei ilikuwa kubwa kwani kwa siku walikuwa wanapokea idadi ya wagonjwa watatu hadi wanne.

Aidha alisema kuwa maradhi ya kipindupindu yamepungua baada ya kupatiwa chanjo za kuzuia kuharisha iliyotolewa miaka iliyopita,hivyo wagonjwa wanaowapokea sasa ni wa maradhi ya kuharisha.

Alisema  changamoto kubwa inayowakabili juu ya wagonjwa hao ni kucheleweshwa kufikishwa hospitali hapo kwa kupatiwa matibabu kwa haraka

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.