Na Abdi Suleiman, Pemba
Kamati ya Olimpiki Maalum Tanzania, (SOT), imeanza kutoa mafunzo ya siku nne kwa makocha na viongozi wa jumuiya mbalimbali za watu wenye ulemavu wa akili kisiwani Pemba.
Mkufunzi wa mafunzo hayo ambae pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kamati hiyo Frank Macha, amesema kuwa watu wenye ulemavu wa akili wana uwezo mkubwa wa kushiriki katika mashindano mbalimbali kama ilivyo kwa watu wasiokuwa na ulemavu.
Alisema, michezo inayochezwa na watu kama hao, ni sawa na ile ambayo watu wengine wanashiriki kuicheza, ingawa inatafautiana kidogo katika mbinu za kufundishia kulingana na maumbile ya wenye ulemavu wa akili.
Naye Mratibu wa SOT tawi la Pemba Mashavu Juma Mbarouk, aliwataka makocha hao kutumia ujuzi watakaoupata baada ya mafunzo hayo, ili kuinua vipaji vya watoto wenye ulemavu wa akili.
Makocha 35 kutoka wilaya za Pemba, wanashiriki mafunzo hayo yanayofanyika uwanja wa Gombani yenye lengo la kuwafundisha watoto wenye ulemavu wa akili michezo ya aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment