Akiri ilikuwa Changamoto Kubwa
HATIMAYE wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameipitisha bajeti ya wizara ya Nchi Ofisi Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, baada ya kuipigishwa katwa kwa zaidi ya masaa matatu wakipitisha mafungu ya matumizi.
Wajumbe wa kadhaa wa Baraza hilo waliiwekea vipingamizi vya kupitisha
mafungu ya matumizi ya wizara hiyo wakihoji na kutaka ufafanuzi wa matumizi ya
fedha hizo kabla ya kuziidhinisha.
Pamoja na mjadala mkali huku baadhi ya
mawaziri wakimsaidia Dk. Mwinyihaji kuelezea matumizi hayo, Mwakilishi wa jimbo
la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alifanikiwa kuyaondoa matumizi ya yenye
utata ya ununuzi wa televisheni katika Idara ya Uratibu wa Shughuli za
Wazanzibari walionje ya nchi.
Matumizi hayo yenye utata yalionesha ununuzi
wa televisheni hiyo kwa shilingi milioni 40, huku kabrasha jengine likionesha
matumizi hayo shilingi milioni 141.
Waziri alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya
hoja hiyo, alisema si ununuzi wa televisheni bali ni wa jenereta, jambo ambalo
lilipingwa na Jussa na kutaka matumizi hayo yaondolewe, jambo ambalo waziri
huyo aliliridhia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya
Wenyeviti, Hamza Hassan Juma alisema waziri huyo ameponzwa na watendaji wake
kutokana na kutompa taarifa sahihi.
“Waziri ametoa majibu tofauti baada ya
kupokea tarifa kutoka juu, hili tatizo la watendaji wetu, ndugu Mwenyekiti kwa
ruhusa yako namuomba waziri tusiende kwenye kura, akubali fungu lipunguzwe”.
Naye Ismail Jussa alisema ni vyema fungu hilo likaondolewa ili iwe fundisho kwa watendaji ambao
wanaonekana kutotekeleza vyema majukumu yao
ya kumsaidia waziri.
“Kwa leo tutumie nidhamu kwa fuatwa
utaratibu wa kupitisha matumizi ya fedha za wananchi, nawaomba wajumbe wenzangu
tumpitishie fedha za ununuzi wa televisheni mwakani”,alisema Jussa.
Wajumbe wengine waliyoibana bajeti hiyo ni
pamoja na Asha Bakari Makame, Makame Mshimba Mbarouk, Rashid Seif Suleiman,
Mbarok Wadi Mussa ambapo waziri Mohammed Aboud, Omar Yussuf Mzee, Juma Duni Haji
na Mwanasheria Mkuu wa serikali Othman Massoud ndio waliokuwa vinara wa
kumsaidia waziri huyo.
Baada ya wajumbe kupitisha mafungu ya
matumizi ya bajeti hiyo, waziri huyo kabla ya kutoa hoja alisema ilikuwa
changamoto kubwa.
Awali akitoa ufafanuzi na kujibu hoja wa
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waziri Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame
Mwadini alisema kuwa serikali itamshughulikia askari na ofisa wa Chuo cha
Mafunzo atakayebainika kuwapatia bangi wanafunzi wa vyuo hivyo.
Waziri huyo
alilazimika kueleza hayo kufuatia baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo, kulalamikia
kuwepo tabia ya matumizi ya bangi kwa wanafunzi wa vyuo vya Mafunzo.
Alisema suala la
uvutaji bangi kwa wanafunzi wa vyuo hivyo linaumiza vichwa na kwamba endapo
askari au ofisa yeyote atakabainika kuwapatia bangi wafungwa atachukuliwa hatua
za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.
‘Wanafunzi
wanapelekwa Vyuo vya Mafunzo kurekebishwa tabia kutokana na makosa
waliyoyafanya, sasa itakuwaje wawepo askari au maofisa wanaowapenyezea bangi
wanafunzi, tukibaini askari
tuamshugulikia’, alisema waziri huyo.
Akizungumzia
suala la upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID), alisema Idara
ya Vitambulisho haitia vitambulisho kwa ubaguzi.
Alisema
kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni haki ya kila mwananchi wa Zanzibar,
lakini kutolewa kwake kunahitaji kufuatwa utaratibu uliowekwa ikiwemo
kuthibitisha sifa ya Uzanzibari.
Alifahamisha
kuwa wapo wananchi waliobainika kughushi hati za kuzaliwa na kula viapo vya
uongo mahakamani ili waweze kufanikisha kupata vitambulisho hivyo, lakini hata
hivyo wametiwa adabu kwa kushitakiwa na kunyang’anywa vitambulisho hivyo.
Dk. Mwinyihaji
alisema takwimu zilizopo zinaeleza kuwa kiasi cha wananchi 112,420 katika
wilaya zote za Unguja na Pemba hawajenda kuchukua vitambulisho vyao katika
ofisi za wilaya.
Aidha aliwataka
wananchi watoe taarifa kama wapo wageni waliopata vitambulisho hivyo, ambapo
wale waliobainika kuvipata vitambulisho hivyo ambao si Wanzibari wamefikishwa
katika vyombo vya sheria.
Akizungumzia juu
ya mikato ya fedha kwa ajili ya chakula kwa askari wa vikosi Maalum, alisema utaratibu
huo umeondoshwa na kwamba suala la chakula kwa askari hao limebebwa na serikali
kwa kuongea bajeti kutoka milioni 400 hadi kufikia milioni 750.
Kuhusu nyumba za
viongozi wa serikali, alisema kamati maalum imeundwa ambayo inashughulikia
suala hilo na kwamba kwa hatua ya kwanza kamati hiyo imeshatembelea eneo lote
la Mazizini.
No comments:
Post a Comment