Na waandishi wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana kufuatia kuzama kwa boti ya Mv Skagit ambayo imepoteza maisha ya watu 31 na zaidi ya 136 kujeruhiwa hadi jana.
Meli hiyo ilizama juzi ikiwa karibu na kisiwa cha Chumbe eneo la Pungume, ikitokea jijini Dar es Salaam na kuelekea katika bandari ya Malindi iliyopo mjini hapa.
Akitoa salamu rasmi za serikali, Dk. Ali Mohamed Shein katika kipindi hicho bendera zote zitapepea nusu mlingoti na kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za maombolezo kuanzia jana.
Dk. Shein alisema serikali imehuzunishwa sana kwa mara nyengine tena kujitokeza tatizo la kuzama kwa meli na kupoteza maisha ya watu na mali zao na inatoa pole, ambapo alibainisha kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba abiria 250 na mabaharia tisa wakiwemo watoto 30 pamoja na mizigo.
"Nimesikitishwa sana na msiba huu, Katika wakati huu si vyema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu", Dk. Shein alieleza katika taarifa hiyo.
Dk.Shein amevipongeza vya ulinzi na usalama, pamoja na vyombo vyengine vya usafiri kwa juhudi kubwa walizofanya waliposhiriki kwenye kazi ya uokoaji jambo lililosaidia kuokolewa kwa watu wengi zaidi.
Aidha Dk.Shein alivishukuru vyombo vya habari vya Serikali na binafsi kwa kuonesha moyo wa kusaidia wananchi kupata taarifa za haraka kuhusiana na tukio hilo.
RAIS KIKWETE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, kupitia kwa Rais wa Zanzibar alitoa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha yaliyowapata wananchi wa Tanzania pamoja na wale wa kigeni waliokuwemo kwenye boti hiyo.
"Huu ni msiba wetu sote na kwamba majonzi yenu ni majonzi yangu na ni ya Watanzania wote, ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na kulijenga Taifa letu",alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alimpongeza Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti wa kukabiliana na ajali hiyo tangu taarifa ya kutokea kwa ajali ya kuzama kwa boti hiyo.
Aidha, amewapongeza maofisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya uokoaji wa watu waliopatwa na maafa hayo makubwa.
WANANCHI
Kwa upande wao wananchi waliozungumza na gazeti hili, walisema serikali inatakiwa kujipanga upya katika kulishughulikia suala la kuwa na vifaa vya kisasa vya uokozi.
Mohammed Nassor, alisema maisha ya watu wengi yangeweza kuokolewa kama vingekuwepo vyombo na vifaa vya kisasa vya uokozi, na kuishauri serikali kuhakikisha inakata pua na kuunga wajihi kwa kuwa vifaa hivyo wakati huu.
"Nadhani hatujifunzi kutokana na makosa, mambo kama haya yalitufika wakati wa Mv Spice Islander I, kadhalika Mv Skagit inazama hatuna vifaa, tunaelekea wapi?",alisema mwananchi hiyo.
Aidha mwananchi huyo aliwashauri wananchi kuwa makini kwa kutozidharau taarifa za hali ya hewa, kwani siku hiyo ukweli hali ya bahari ilikuwa chafu sana.
Kwa upande wake Maua Said, alisema umefika wakati kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, kuhakikisha nayo inashirikishwa kikamilifu katika uratibu wa safari za vyombo vya baharini, kwani utaalamu wao unaweza kuepusha majanga ya namna hiyo.
Alifahamisha kuwa endapo utabiri wa Mamlaka hiyo ungekuwa unafuatwa kikamilfu hasa wakati kama huu wa pepo za Kusi, ingewezekana kabisa kupunguza athari za janga hilo.
WAZAMIAJI
Kikosi cha uzamiaji na uokozi, walisema ni vyema Zanzibar kikawepo Chuo cha masuala ya uzamiaji hali ambayo itaviwezesha visiwa hivi kuwa na wataalamu wengi watakaoweza kupunguza maumivu ya majanga yanapojitokeza.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema Zanzibar pamoja na kuzungukwa na bahari lakini ina tatizo kubwa la uhaba wa wazamiaji wenye utaalamu.
"Serikali ianzishe chuo cha uzamiaji, hali hii itatufanya kuwa na wataalamu wengi, nchi yetu imezungukwa na visiwa linapotokezea janga tutaweza kupunguza ukali wa maumivu", alisema.
VYAMA VYA SIASA
Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib alitoa mkono wa pole kwa ndugu jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huo na kuwataka kuwa na subira katika kipindi hicho kigumu cha msiba mkubwa.
‘Chama cha TADEA, tuko pamoja na wafiwa wote kwa msiba huu uliotufikia Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu pahali pema peponi’,alisema Katibu huyo.
Mkurugenzi Mipango Uendeshaji na Sera wa Chama cha AFP, Rashid Yussuf Mchenga kwa niaba ya chama hicho alisema kufuatia utokea kwa msiba huo Zanzibar imekuwa katika kipindi chengine kigumu.
"Ni wakati mgumu tulionao kwa msiba uliotokezea lakini tunatakiwa kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha maafa haya yaliyotokezea",alisema Mchenga.
Aidha Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wananchi kutozidharau taarifa za Mamlaka ya hali ya hewa kwani zina umuhimu wake pamoja na kuiomba serikali kuhakikisha inakuwa na vifaa vya kisasa vya uokozi.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini Magharibi, katika taarifa yake kilisema uongozi wa chama hicho Mkoa huo umepokea kwa huzuni, majonzi na masikitiko taarifa za kuzama kwa meli ya Mv. Skagit na kuwapa mkono wa pole majeruhi wa ajali hiyo.
Kwa niaba ya Katibu wa CCM mkoa huo, Ali Suleiman alisema uongozi huo unawapa mkono wa pole wale wote waliohusika moja kwa moja na msiba huo na kwamba kadhia ya ajali hiyo imesababishwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Chama cha CUF, kimeeleza kusikitishwa kwake na msiba huo na kutoa salamu za rambi rambi kwa wote walioguswa kwa namna moja au nyengine, ambao ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein na Watendaji wakuu wa serikali yake, ambapo imewaombea subira katika wakati huu mgumu wa maombolezo.
Katika taaarifa yake iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Haki za binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani, CUF imeeleza kwamba inathamini juhudi zilizokwishaanza kuchukuliwa na Serikali kuwapunguzia na kuwaondolea adha ya usafiri wananchi hasa wa baharini ndani na nje ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo taarifa hiyo ya Bimani imetoa wito kwa Serikali na Mamlaka husika kuendelea kufanya uchunguzi wa kina na pia kuchukua hatua muafaka za dharura ili kuyanusuru maisha ya wasafiri, kuweka mazingira ya msaada wa haraka pindi yatapotokea matukio ya aina hiyo na kuyawekea kinga yasitokee kwa kadri inavyowezekana.
IGP, KAMISHNA MUSSA
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali, Said Ali Mwema, alisema tukio la kuzama kwa Mv. Skajit litafanyiwa uchunguzi na kueleza kuwa wizara ya Mambo ya Ndani imehuzunishwa na tukio hilo.
IGP Mwema alisema jeshi lake litalazimika kuongeza timu ya uchunguzi kufuatilia tukio hilo ili kuweza kujiridhisha na hali halisi ya ajali hiyo ilivyotokea.
"Tayari timu ya kuchunguza tukio hilo imeshaundwa na inakuja kutafuta chanzo na hali halisi ya mkasa wa kutokea kwa tukio hilo",alisema IGP Mwema.
Wakati huo huo Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema pamoja na kutokea kwa tukio hilo hali ya usalama bado ni nzuri na kuwataka wananchi kutulia.
Alisema Jeshi la Polisi, litaendelea kusimamia kazi za uokozi ili kuona waliopotea maiti zao zinapatikana na kukabidhiwa familia zao na kuwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa za watu watakaowaona.
HALI YA USAFIRI WA BAHARI
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano asubuhi ya jana ilizuia usafiri kwa vyombo vya baharini vunavyofanya safari kati ya Unguja Dar es Salaam na kutoka Unguja kuelekea Pemba.
Hata hivyo majira ya saa 6 mchana, boti hizo ziliendelea na safari zake kama kawaida kwa kupeleka watu kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam.
Kusitishwa kwa vyombo hivyo wakati wa asubuhi kuliwafanya wasafiri wengi kujazana bandarini Zanzibar huku wakionekana kuwa na nyuso zenye wasiwasi.
HOSPITALI YA MNAZIMMOJA
Katibu wa hospitali ya Mnazimmoja, Omar Abdalla alisema hospitali hiyo hadi jana asubuhi ilikuwe imepokea watu 142 waliojeruhiwa kwenye kadhia ya kuzama kwa Mv Skagit.
Alisema kati ya hao zaidi ya watu 80 waliruhusiwa kurejea nyumbani kwao baada ya afya zao kuonesha kuridhisha.
Alisema ni majeruhi wawili tu waliokuwa katika chumba cha wagonjwa mahatuti na mmoja aliyevunjika mguu ndio bado afya zao zitachukua muda kidogo.
"Wagonjwa wote waliofikishwa hapa wengi wao waliruhusiwa na kuchukuliwa na ndugu zao, lakini wagonjwa wanane bado hawajatambulikana na jamaa zao kwani ni wenyeji wa Tanzania bara’,alisema katibu huyo.
VIONGOZI WALIOTEMBELEA MAJERUHI
Baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein kutembelea hospitali kuu ya Mnazimmoja juzi usiku kuangalia majeruhi, viongozi wengine jana walifika kuwatembelea majeruhi katika hospitali hiyo wakiongozwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, baada ya Baraza hilo kukatisha kikao chake jana ili kutoa fursa kwa Wajumbe kushiriki katika msiba huo ambao umewagusa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
TUME YA KUKUSANYA MAONI
Kufuatia ajali ya kuzama kwa Mv Skagit, tume hiyo jana ilisitisha mikutano yake ya kukusanya maoni ya katiba mpya kwa wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba.
Taarifa ya tume hiyo iliyotolewa jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa zoezi la kukusanya maoni litaendelea Jumamosi ya Julai 21 mwaka huu kwa wananchi wa Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara.
"Tume imepokea kwa masikitiko makubwa Taarifa ya ajali ya Meli ya MV SKAGIT na imesitisha mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba," imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Habari hii imeandaliwa na Mwantanga Ame, Mwashamba Juma, Hafsa Golo, Asya Hassan na Madina Issa.
No comments:
Post a Comment