DAR ES SALAAM
TIMU ya Simba, jana ilipata kipigo kama cha watani wao Yanga kwa kufungwa mabao 2-0 na watoza ushuru wa Uganda (URA) katika mchezo kundi A wa Kombe la Kagame uliopigwa uwanja wa Taifa wakati wa saa kumi.
Kipigo hicho kinakuja siku moja baada ya Yanga kulala kwa mabao kama hayo mbele ya Atletico ya Burundi.
Waganda walianza kucheka na nyavu katika dakika ya 1-0 kwa bao lililopachikwa nyavuni na mchezaji Owen Kasule.
Licha ya washambuliaji wa Simba kujaribu kupapatua, matokeo hadi yalibaki hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili timu hizo zilishambuliana kwa zamu, lakini siku haikuwa njema kwa Simba kwani ilijikuta ikipachikwa bao la pili lililofungwa na mchezaji Feni Ali dakika chake kabla mchezo kumalizika.
Na katika pambano lililopigwa uwanja wa Chamazi saa kumi, wenyeji Azam FC walilazimishwa sare ya bao 1-1 na walinda wafungwa wa Zanzibar timu ya Mafunzo.
Azam ndiyo iliyotangulia kupata bao lake kupitia kwa John Bocco mnamo dakika ya 26, kabla ya Ali Juma kuisawazishia Mafunzo kwenye dakika ya 60.
Mafunzo pia iliweza kupata bao la pili ambalo lilikataliwa na mwamuzi, na kuibua makalamiko kutoka majukwaani.
Nayo timu ya Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilikula pweza kizani kwa kuichakaza Ports ya Djibouti magoli 7-0 katika mchezo uliofanyika uwanja wa Chamazi wakati wa saa nane.
Michuano hiyo inaendelea tena kesho kwa mechi kati ya Atletico na APR kwenye uwanja wa Taifa saa nane mchana, na baadae Yanga kujaribu bahati mbele ya Wau El Salaam uwanjani hapo wakati wa saa kumi jioni.
No comments:
Post a Comment