Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Umelani wilayani Kibaha mkoani Pwani, Omary Ally (31) amehukumiwa kwenda jela kwa muda wa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mvulana mwenye umri wa mika (12) ambaye ni mpwa wake.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya Kibaha, Salome Mshasha chini ya mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi Inspekta, Kulwa Merdad.
Mshitakiwa alidaiwa kutenda kosa hilo Januari 18 mwaka huu majira ya saa 6 usiku huko mtaa wa Umerani.
Mahakama ilielezwa kuwa wakati mshitakiwa akitenda kosa hilo mkewe alikuwa kwao akisubiri siku za kujifungua na alipokwenda kumsalimia mkewe nyumbani kwao alikuta amekwenda hospitali na kukaribishwa na wenyeji wake alale na wapwa zake wawili na ndipo alipomlawiti mtoto huyo.
Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Mwendasha mashitaka aliomba mshitakiwa apewe adhabu kali kutokana na tukio hilo ili iwe fundisho kwake na jamii kwani kitendo hicho ni cha kinyama na mshitakiwa hastahili kukaa na jamii iliyostaarabika.
Akijitetea mahakamani hapo mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani yeye ni mgonjwa na anatumia dozi halafu ni baba wa familia ya mke na watoto wawili wanaomtegemea.
Hakimu Mshasha akitoa adhabu hiyo alisema kuwa mshitakiwa alikuwa na dhamana ya kulinda haki za mtoto huyo na si kuzivunja kama alivyofanya jambo ambalo ni unyanyasaji na udhalilishaji mkubwa na kuwa adhabu ya makosa kama hayo inajulikana.
Alisema baada ya kupitia ushahidi na vilelezo vilivyotolewa na upande wa mashitaka amejiridhisha na kutoa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia yaka hiyo.
No comments:
Post a Comment