Habari za Punde

Dk Shein afanya mazungumzo na Rais wa Vietnam, Mhe Truong Sang

 
Na Rajab Mkasaba, Hanoi, Vietnam
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang ambapo kiongozi huyo wa Vietnam alieleza kuwa ziara hiyo itafungua ukurasa mpya hasa katika masuala ya mashirikiano ya kiuchumi baina ya pande mbili hizo.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu mjini Hanoi, Vietnam, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Dk. Shein nchini humo.
Katika maelezo yake, Rais Sang alimueleza Dk. Shein kuwa Vietnam inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Rais Sang alieleza kuwa Vetnam ina historia kubwa kati yake na Tanzania na kutoa shukurani kwa Tanzania kutokana na kuiunga mkono nchi hiyo wakati wa ukombozi wake.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaimarika zaidi iwapo kutakuwa na ziara za mara kwa mara za viongozi wa nchi mbili hizo na kuwataka Mawaziri wa nchi hizo kutembeleana ili kuweza kubadilishana uzoefu na utaalamu sanjari na kupanga mipango ya uimarishaji wa sekta za maendeleo.
Aidha, Rais Sang alimueleza Dk. Shein kuwa kuwa Vietnam inaunga mkono uhusiano na ushirikiano katika sekta za maendeleo hasa katika sekta ya kilimo na uvuvi ambapo nchi hiyo imeweza kupiga hatua.
Kiongozi huyo alieleza jinsi alivyovutiwa na mazungumzo yaliofanyika kati ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Bi Nguyen Thi Doan pamoja na Rais wa Zazibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika maelezo yake ya kuunga mkono mazungumzo hayo, Rais Sang alimueleza Dk. Shein kuwa Vietnam imevutiwa na juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na mipango, Dira, Sera na mkakati wake wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Rais Sang alieleza kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano na nchi za Afrika hasa Tanzania ikiwemo Zanzibar. Pia, alisisitiza kuwa katika mashirikiano hayo nchi yake itaelekeza zaidi ushirikiano katika sekta ya uwekezaji na biashara.
Rais huyo wa Vietnam alisisitiza haja ya kuungwa mkono nchi yake na Tanzania katika ombi lake la kutaka kutambuliwa kuwa Taifa la Soko Huru Ulimwenguni hatua ambayo pia itazinufaisha nchi rafiki ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa jumla.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo alimuomba Dk. Shein kumfikishia salamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete huku akieleza kuwa anatambua juhudi anazozichukua katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi wa Tanzania na kumtakia afya njema na ufanisi zaidi wa kazi zake.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi na shukurani kwa kiongozi huyo kutokana na mualiko rasmi kwa Rais wa Zanzibar nchini humo, hatua ambayo inaonesha jinsi nchi hiyo inavyothamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha ziara za kimaendeleo kwa viongozi wa Zanzibar kwenda nchini humo kwa ajili ya mashirikiano ya pamoja zinafanyika.
Aidha, alieleza kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam na itaendelea kujifunza kwani inatambua mafanikio iliyoyapata nchi hiyo katika sekta za maendeleo.
Alisema kuwa kama inavyofahamika kuwa Vietnam ni nchi ya pili ulimwenguni kwa kusafirisha mchele kutokana na kupata mafanikio makubwa katika uzalishaji wa zao la mpunga, hivyo kuna haja ya kupanua wigo wa mafanikio hayo na kusoma jinsi walivyofikia hatua hiyo ili iwe kigezo kwa Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ulimwenguni inafanya masafa ya dunia kuwa karibu na kufanya safari kati ya Zanzibar na Vietnam haizidi zaidi ya masaa 24, hali ambayo inarahisisha mawasiliano na mashirikiano kati ya pande mbili hizo
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Rais Sang kuwa tayari viongozi kadhaa wa Tanzania wameshaitembelea nchi hiyo kwa lengo la kuimarisha ushirikiao na uhusiano uliopo akiwemo Rais Mstaafu Benjamin Willium Mkapa alietembelea Vietnam mwaka 2004, Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa mwaka 2007 na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda ambaye alietembelea nchi hiyo mwaka 2009.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Nguyen Tan Dung, huko Ikulu mjini Hanoi, Vietnam ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao walisisitiza mashirikiano kwa manufaa ya pande mbili hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.