Habari za Punde

Zanzibar mwenyeji wa mkutano wa 36 Baraza la utawala la ARIPO



MKUTANO WA 36 WA “ADIMINISTRATIVE COUNCIL” YA ARIPO

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 36 wa Baraza la Utawala la ARIPO (ARIPO Adiministrative Council), unaondaliwa kupitia Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Shirika la kusimamia Mali za Ununifu la Kanda ya Afrika (African Regional Intellectual Property Organization –ARIPO).

Mkutano huo wa kimataifa utachukua muda wa siku tano kuanzia tarehe 26 – 30 Novemba 2012, utafanywa katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli Zanzibar Beach Resort iliyoko Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ambapo Mgeni Rasmi atakaefungua Mkutano huo anatarajiwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Jumla ya washiriki 75 kutoka nchi wanachama wa ARIPO pamoja na waalikwa kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika, pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali yanayosimamia mali za ubunifu wanatarajiwa  kushiriki katika mkutano huo.


Shirika hili (ARIPO) limeanzishwa mjini Lusaka, Zambia, terehe 9 Disemba, 1979 kupitia mkataba maalum unaojulikana kama Makubaliano ya Lusaka (Lusaka Agreement), kwa lengo la kuimarisha mashirikiano katika kulinda  rasilimali za nchi wanachama, kushirikiana, kubadilishana taarifa  pamoja na kuweka misingi ya pamoja ya sheria katika kusimamia kazi za Tasnia ya Mali za Ubunifu (zikiwemo Alama za biashara (TradeMark), Hataza /uvumbuzi (Patent), miundo (Design), Viashiria vya mahala (Geographical Indications), Hakimiliki (copy rights) katika kila nchi mwanachama wa shirika hili.

Madhumuni makuu ya ARIPO yamebainishwa katika kifungu cha tatu cha Mkataba wa Lusaka, ambayo ni pamoja na kuweka misingi ya kushirikiana kwa madhumuni ya kufikia maendeleo ya teknolojia na kiuchumi kwa nchi wanachama  kuimarisha usimamizi wa Tasnia za Mali za Ubunifu.

ARIPO inaundwa na vyombo viwili vikuu ambavyo ni Baraza la Mawaziri (Council of Ministers) ambalo wajumbe wake ni Mawaziri wanaosimamia Mali za Ubunifu katika nchi wanachama na Baraza la Utawala (Administrative Council) ambalo wajumbe wake ni wakuu wa taasisi au idara zinazosimamia Mali za Ubunifu katika nchi wanachama. Makao makuu ya shirika hilo yapo Harare, Zimbabwe.

Baraza la Utawala linakutana kila mwaka katika chini mwanachama itayoomba na kukubaliwa kuandaa mikutano hiyo. ARIPO ina jumla ya nchi wanachama kumi na nane (18) ambazo zinazozungumza lugha ya Kiingereza ambazo ni wanachama wa shirika hilo  ni pamoja na Botswana, the Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Malawi, Mozambique, Namibia, Sierra Leone, Liberia, Rwanda, Somalia, Sudan, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Miongoni mwa faida zilizopatikana na nchi wanachama kutokana na ARIPOni kuziweka pamoja rasilimali watu na rasilimali fedha, ambapo  nchi nchi wanachama zimeweza kufaidika kimaendeleo na kiuchumi kutokana na kupata fursa ya kutumia rasilimali adimu mbazo na muhimu kwa mahitaji na maendeleo  ya nchi wanachama na raiya wake.

Umuhimu wa kusimamia rasilimali hizi zinazotokana na mali za ubunifu, umedhihihirika katika nchi mbalimbali ambazo zimetoa kipaumbile katika kusimamia mali za ubunifu. Mfano mzuri wan chi zilizofaidika kwa kusimamia vizuri mali za ubunifu ni Korea ya Kusini. Kipindi kifupi kilichopita Korea ya Kusini ilikuwa mingoni mwa nchi masikini duniani kutokana na kukosa rasilimali za asili zenye ubora. Kwa sababu nchi hii imeweka mikakati imara ya kusimamia mali za ubunifu imeweza kupiga hatua kubwa za kimaendelea tena kwa haraka, na kuiweka katika nafasi ya nne katika nchi zilizoendelea kwa teknolojia ambapo ya kwanza ni Marekani inayoifuatiwa na Japani na China.

Hii ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huu, lakini ni mara ua pili kwa Tanzania. Mkutano wa kwanza ulifanyika jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano huu wa 36 ni pamooja na Bajet ya kuendeshea shughuli za ARIPO, Masuala ya utendaji na uwajibikaji, Taarifa za utekelezaji za nchi wanachama, semina kuhusu Teknolojia ya Habari na viashiri vya pahala (geographical Indication) na uchaguzi wa viongozi wapya wa ARIPO. Aidha washiki watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria.

Serikali inatoa wito kwa vyombo vyote vya habari nchini kutoa taarifa kwa wananchi juu ya umuhimu wa mkutano huu na usimamizi wa mali za ubunifu. Mali za ubunifu ni moja kati ya nyenzo muhimu katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na teknolojia, kilimo, sanaa na utamaduni. Aidha waandishi wa habari wanaomba wafuatilie mwenendo wa mkutano huo ili waweze kuwaarifu wananchi juu ya mambo mbalimbali yatayojadiliwa katika mkutano huo. Halikadhalika Serikali inawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa watendaji wake pamoja na wageni watakaoshiriki katika mkutano huo.

 

 

Imetolewa na:

 

Afisi ya Mrajis Mkuu wa Serikali

Zanzibar, 

 

Na

 

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tanzania.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.