Habari za Punde

Vietnam na Zanzibar zakubaliana kuimarisha uhusiano

Na Rajab Mkasaba
 
Hanoi,Vietnam 23.11.2012
ZANZIBAR na Vietnam zimekubaliana kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kukuza sekta za maendeleo na uchumi huku Vietnam ikiahidi kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha inafikia malengo yake iliyojiwekea katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzaniaikiwemo Zanzibar na Vietnam hasa katika sekta za maendeleo na uchumi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Rais wa Vietman Mhe. Bi Nguyen Thi Doan huko katika ukumbi wa Ikulu ya nchi hiyo mjini Hanoi.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam kutokana na nchi hiyo kupata mafanikio makubwa katika uimarishaji wake wa uchumi na pamoja na sekta za maendeleo.
Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo kati ya Zazibar na Vietnam ni pamoja na sekta ya uvuvi, kilimo, utalii, uimarishaji wananchi kiuchumi, biashara pamoja na sekta nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein amueleza Makamu huyo wa Rais kuwa Tanzania na Vietnam zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu tokea miaka ya 1960 na zimeweza kuungana mkono katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo, kiuchumi na hata kisiasa.
Dk. Shein alimueleza kingozi huyo hatua zinazochukuliiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi na mafanikio yaliofikiwa katika kutekeleza Dira ya 2020 pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi a Kupunguza Umasikini (MKUZA).
Kwa upande wa kilimo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Tanzania imeweka mikakati maalum ya kuimarisha sekta ya kilimo ambapo kwa upande wa Zanzibar Serikali mechukua juhudi kubwa katika kuhakikisha sekta hiyo inapewa kipaumbele.
Dk. Shei alisema kuwa sekta ya kilimo ndio uti wa mgongo wa Zazibar hali ambayo inapelekea kutafuta kila njia katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ikiwa ni pamoja na kuimarisha kilimo cha kisasa chenye kuendana na sayansi na tekolojia na kuwapa unafuu wakulima wadogo wadogo kwa kuwawekea mazingira bora ya kilimo.
Mbali ya juhudi hizo, Dk. Shein alimueleza kionhozi huyo hatua zilizochukuliwa na Serikali yake katika sekta ya kilimo kwa kukimarisha Chuo cha Utafiti wa Kilimo kiopo Kizimbani Zanzibar kusisitiza haja ya kuwepo mashirikiano katika utafiti huo wa kilimo.
Akieleza juu ya hatua za kiuchumi inavyoimarisha kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu ambayo inachangia sana pato la taifa la Zanzibar na kusisitiza haja ya kuwepo mashirkiano kwa pande mbili hizo ili kuweza kuimarika zaidi. Pia, alimueleza jinsi uchumi wa Zanzibar unavyoimarika.
Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi na kueleza haja ya kushirikiana katika sekta hiyo, kutokana na Vietnam kupata mafaikio makubwa katika sekta hiyio.
Pia, Dk. Shein aeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeunda Wizara maalum inayoshughulikia uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika kwa lengo la kuwasaidia wananchi katika kuwaletea maendeleo hatua ambayo Vietnam imefanikiwa.
Dk. Shein pia, alimueleza kiongozi huyo hatua zinazochukuliwa na serikali anayoiongoza katika kuimarisha amani na utulivu uliopo. Alimueleza kuwa amani na utulivu ndio msingi mkubwa wa maendeleo hivyo Zanzibar itahakikisha inaiimarisha na kuiendeleza kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo mafanikio yalipatikana katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa pamoja na kueleza kuwa kuwepo kwa hatua hiyo kulichangia kufanyika kwa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki huku akisisitiza kuwepo mashirikiano mazuri ndani ya serikali hiyo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa ziara za viongozi kati ya pande mbili hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uhusiano na ushirikiano.
Nae Makamu wa Rais wa Vietnam Bi Nguyen Thi Doan, alitoa pongezi kwa Dk Shein kwa kukubali muwaliko wa nchi hiyo kwa ajili ya ziara hiyo hatua ambayo inaonesha wazi jinsi Zazibar inavyothamini uhusiano na ushirikiano kati yake na Vietnam.
Katika maelezo yake, kiongozi huyo alisisitiza kuwa Vietnam taendelea kuiunga mkono azibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo miradi ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, uvuvi na nyenginezo
Mhe. Doan alimueleza Dk. Shein kuwa Vietnam imekuwa na ushirikiano mwema na Tanzania kwa muda mrefu hivyo hatua zilizokuwepo hivi sasa ni kuimarisha na kukuza uhusiano huo hasa kwa Zanzibar.
Alisema kuwa Vietnam imekuwa ikishirikiaa vyema na nchi kadhaa za Afrika zikiwem Angola, Afrika ya Kusini, Msumbiji, Guinea na nchi nyenginezo na kuweza kuanzisha miradi mbali mbali ya maendeleo
Pia, Vietnam imeleeza azma yake ya kushirikiana na Zanzibar katika sekta za uwekezaji, viwanda, biashara, mawasiliano ya simu, afya,elimupamoja na sekta nyenginezo huku ikisisitiza haja ya kuwepo ziara za kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya pande mbili hizo.
Sambamba na hayo, Vietnam ilitoa ombi maalum kwa Tanzania la kuiunga mkono nchi hiyo katika ombi lao la kutaka kutambuliwa kuwa Taifa la Soko Huru Ulimwenguni Pia, alipongeza juhudi za kimaendeleo zinazochukuliwa na Zanzibar pamoja na uimarishaji wa amani na utulivu.
Makamu huyo wa Rais pia, alieleza kuwa Vietnam iko tayari kufanya mazungumzo ya kuwakutanisha viongozi wa Zanzibar wakiwemo Mawaziri na wale kutoka nchini humo ili kukaa pamoja na kuangalia maeneo ya kushirikiana katika kukuza sekta za maendeleo.
Mapema Dk. Shein, aliweka shada la maua na kutoa heshima katika makaburi ya mashujaa akiwa ameambatana na Mkewe Mama Mwanamwema Shein pamoja na ujumbe aliofuatana nao ambapo baada ya hapo aliweka shada la maua na kutoa heshima katika kaburi la Hayati Baba wa Taifa hilo Ho Chi Minh, katika kumbusho liliopo mjini Hanoi, Vietnam

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.