Na Mwandishi wetu, Hanang
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kama watu waliobinafsishiwa mashamba ya
kilimo cha ngano ya Basutu, wilayani Hanang, wameshindwa kulima ngano basi
wayarudishe serikalini.
Aidha, Rais Kikwete alisema mashamba
hayo hayakupewa watu binafsi ili nao watumie ardhi hiyo kuwakodishia wananchi
bali walipewa kulima ngano.
Na ili kupata ufumbuzi wa matumizi ya
mashamba hayo, Rais Kikwete alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo
kukaa chini na Kamati ya Maendeleo ya Mkoa (RDC) kujadili masuala yote
yanayohusu mashamba hayo na kutoa mapendekezo kwa serikali.
Rais Kikwete aliyaeleza hayo kwenye
mkutano wa hadhara wa wananchi wa Katesh, Hanang wakati aliposimama kwa muda
mjini hapo akiwa njiani kutoka Babati, Manyara, kwenda Singida kwa ziara ya
siku mbili kukagua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete wakati anataka waliopata
mashamba hayo katika zoezi ya ubinafsishaji kulima ngano kama ilivyotakiwa lakini
pia ametaka wananchi ambao aliwagawia mashamba mawili ya serikali katika eneo hilo nao wayatumie mashamba hayo kama
walivyoomba.
“Napenda pia kuwataka wale wananchi
waliopewa ardhi katika yale mashamba yaliyokuwa ya serikali nao wahakikishe
kuwa mashamba hayo yanafanya kazi,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alilizungumzia suala hilo
baada ya Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Rose Kamili kulalamikia kutokutumika kwa mashamba hayo yaliyobinafsishwa kwa
watu binafsi baada ya kushindwa kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment