Habari za Punde

Zanzibar Heroes yatinga nusu fainali kombe la Cecafa, Kilimanjaro Stars nayo ndani


 
Wachezaji wa Zanzibar wakiwa wamembeba kipa wao, Mwadini Ally baada ya kupangua mkwaju mmoja wa penalti, na kuiwezesha timu hiyo kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuifunga Burundi kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Lugogo, mjini Kampala, Uganda jioni hii. Zanzibar sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi.

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
 
ZANZIBAR imeingia Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuifunga Burundi kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Lugogo, mjini Kampala, Uganda jioni hii kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
 
Kwa matokeo hayo, Zanzibar sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
 
Shujaa wa Zanzibar leo alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundin walipoteza penalti zao leo.
 
Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
 
Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
 
Zanzibar leo walicheza soka ya kuvutia na kiungo Suleiman Kassim ‘Selembe’ ndiye aliyekuwa nyota ya mchezo kutokana shughuli kubwa aliyoifanya akicheza katika dimba la juu.
 
Ndikumana leo aliwekewa ulinzi mkali na hakuwa na madhara kwa Watanzania wa upande wa pili wa Bahari. 
 
Mapema katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali, Bara ilifanikiwa pia kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Lugogo mjini hapa.
 
Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.
Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili,
Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili 53 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.
Baada ya bao hilo, Rwanda walionekana kupagawa, lakini hawakusahau kushambulia lango la Stars na dakika ya 86 Dadi Birori hakujali ameotea akasukuma mpira nyavuni, lakini refa akakataa bao hilo.
Kwa ushindi huo, Stars sasa inasubiri mshindi kati ya Uganda na Ethiopia kesho kukutana naye kwenye Nusu Fainali.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Amri Kiemba, Salum Abubakar/Athumani Iddi dk51, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa na John Bocco/Shaaban Nditi dk 85.
Rwanda; Jean Claude Ndoli, Emery Basiyenge, Ismail Nshutimayamangara/Fabrice Twagizimana dk19, Jimmy Mbaraga/Imran Nshiyimana dk67, Charles Tibingana/Barnabe Mbuyumbyi dk61, Michel Rusheshangoga, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jean Claude Iranzi, Dadi Birori na Tumaine Ntamuhanga

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.