Habari za Punde

Maalim Seif afanya ziara ofisi za usajili na kituo cha serikali mtandao

 Maalim Seif akiangalia ramani ya Zanzibar jinsi Mkonga wa Mawasiliano unavyoweza kuziunganisha taasisi za serikali kupitia mradi wa e-government katika ofisi za kituo hicho Mazizini Zanzibar
Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Zanzibar (Zan ID), Mohd Juma Ame akionesha mfumo wa utayarishaji wa vitambulisho hivyo katika ofisi hizo zilizoko Mazizini Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad, OMKR


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea umuhimu wa kuwepo uadilifu katika mchakato mzima wa utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.
Amesema kitambulisho hicho ni muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa, hivyo umakini na uadilifu unahitajika kuhakikisha kuwa wanapewa wanaohusika.
Maalim Seif ameeleza hayo leo wakati akiwa katika ziara maalum ya kutembelea ofisi za usajili na kadi za utambulisho Zanzibar pamoja na kituo cha Serikali Mtandao e-government kilichopo Mazizini.
Amesema kuna taarifa kuwa wapo baadhi ya watu wasiokuwa raia wa Tanzania wamekuwa wakipatiwa vitambulisho hivyo na kuwaacha wazanzibari wenye sifa, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi.

Hata hivyo ameelezea kuridhishwa kwake na utendaji wa ofisi hiyo, na kuwataka kuongeza juhudi ili kuhakikisha kuwa wanapata ujuzi wa kutosha katika kuendeleza kazi hiyo.
Amewahimiza wanasiasa kuwashajiisha wafuasi wao kufuatilia vitambulisho vyao, ili kila mzanzibari aliyetimiza masharti aweze kupata kitambulisho hicho ambacho kitamsaidia katika harakati zake za maisha.
“Kitambulisho hiki ndio maisha kwa sasa, bila ya kuwa nacho huwezi kufanya jambo lolote la maendeleo, yaani hata ukitaka leseni ya udereva lazima uwe na kitambulisho, seuze kusafiri, kuendelea na masomo au kutafuta ajira”, alifahamisha Maalim Seif.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho Bw. Mohd Juma Ame amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa wanafanya kazi kwa utaalamu wa hali ya juu kuhakikisha kuwa hakuna udanganyifu unaofanywa katika utoaji wa vitambulisho hivyo.
Amesifu ubora wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, na kwamba vinatengenezwa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu inayoweza kudhibiti taarifa za siri za muhusika ambazo haziwezi kuonekana bila ya kutumia kifaa maalum, na hivyo kuweza kudhibiti ubadhirifu.
Akizungumzia kuhusu mtandao wa serikali, e-government Maalim Seif amesema mradi huo umeanza vizuri na kutaka undelezwe kwa maslahi ya taifa.
Ameelezea matumaini yake kuwa iwapo mpango huo utatumiwa vizuri unaweza kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali, kwa vile watendaji wataweza kuwasiliana, kufanya vikao na kukubaliana kupitia njia hiyo ya mtandao.
Amewahimiza watendaji wa ofisi hiyo kuandaa vipindi maalum vya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa mfumo huo wa e-governmet, ili kuongeza uelewa na kuweza kuona faida za mfumo huo.

1 comment:

  1. kitu cha kushangaza hivi vitambulisho kwanini vipo vya kiZanzibari,vipi tupewe na vya kitanzania???na hizi ni nchi mbili tofauti,au kuna namna?.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.