Na Maelezo Zanzibar 20/02/2013
Mamia ya Wananchi wa Zanzibar leo wameshiriki Mazishi ya Padri Evaristus Mushi aliyeuwa kwa kupigwa Risasi na Watu wasiojulikana ambayo yamefanyika katika kijiji cha Kitope Wilaya ya Kaskazini B,Unguja.
Katika mazishi hayo Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad,Viongozi wa Serikali na Vyama vya siasa walihudhuria.
Akitoa salamu za Serikali katika Mazishi hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed alisema Serikali imeguswa sana na kifo cha Padri huyo na kuongeza kuwa itahakikisha waliohusika na tukio la mauji hayo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikacana Michael hafidh amewataka Waamini wa dini ya kikristo kuwa watulivu bila kulipiza kisasi bali waiachie Serikali kufanya kazi yake ili kuwabaini waliopoteza Uhai wa Marehemu huyo.
Awali Mazishi hayo yalitanguliwa na Misa takatifu ya kumuombea Marehemu iliyoendeshwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam Muadhama Policarp Kadinali Pengo katika Kanisa la Minara Miwili Mjini Zanzibar.
Padri Mushi alifariki dunia Februari 17 baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akielekea Kanisani kuendesha Misa ya Asubuhi katika Kigangwe cha Mtakatifu Teresia eneo la Beit El Raas mjini Unguja
Enzi za uhai wake Padri Mushi alikuwa Msomi wa Shahada ya Uzamivu ya Elimu ya Ushauri nasaha aliyoipata nchini Marekani ambapo umauti ulimkuta akiwa anaelekea kuendesha Ibada ya Jumapili ya kwanza ya Kwarezma.
Padri Evarist Mushi wa Kanisa la Minara Miwili mjini Zanzibar alizaliwa June 15, 1957 Mkoa wa Kilimanjaro akiwa ni mtoto wa nne katika familia ya watoto sita ya Mzee Mushi.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment