Habari za Punde

Uharibifu Kesi za Dawa za Kulevya Wakwamisha Mapambano



Na Mwanajuma Mmanga
SERIKALI imeshauriwa kuanzisha mahakama maalum itakayoshughulikia kesi za dawa za kulevya kutokana na mahakama zilizopo kuchelewesha kesi za aina hiyo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa kitengo cha kuzuia dawa ya kulevya, Mrakibu mwandamizi wa Polisi (SSP)  Mkadam Khamis Mkadam alipozungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Alisema ucheleweshaji wa kesi hizo umekuwa ni kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwani watu wengi kuamua kujiingiza katika biashara hiyo kwa kesi zake zimekuwa zikichukua muda mrefu kutolewa hukumu huku washitakiwa wakibakia nje.

"Wanapozidi kuchelewesha kesi za dawa ya kulevya uozo unazidi na watu wengine kushajiishika kujiingiza katika biashara hiyo," alisema.

Alisema iwapo mahakama zingeendesha kesi hizo kwa haraka na ushahidi kukamilika na kutolewa hukumu kungepunguza msongamano wa washitakiwa waliko mahabusu kwa makosa ya dawa za kulevya.

Mkadam ameitaka mahakama kuwa na mpango maalum wa usikilizwaji wa kesi na kufuata haki kama zinavyotakiwa.


Kwa upande wa wananchi wamelitaka jeshi la polisi kutoa ushirikiano ili kudhibiti uingizaji, usambazaji na utumiaji dawa za kulevya.

"Jeshi la polisi halitoi ushirikiano na wananchi wake katika kuondosha biashara hii,” walisema wananchi hao.

Nae Naibu Mkurugenzi wa  upelelezi wa Makosa ya jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi  wa polisi,Yusuf J. Ilembo alisema kumekuwepo uharibifu wa makusudi kwa kesi za dawa za kulevya na kusababisha kwa asilimia kubwa washtakiwa wake kukwepa mkono wa sheria.

Alisema vitendo hivyo vinafanywa na watendaji wenye majukumu ya kusimamia utekelezaji wa sheria.

Alisema hilo linachangia kwa kiasi kikubwa uzoroteshaji wa mafanikio ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwani wafanyabiashara hao hawana cha kupoteza katika mwendelezo wa biashara zao haramu.

Takwimu za dawa ya kulevya zilizoripotiwa katika kipindi cha kuanzia Januari 2010 hadi 11 Oktoba 2012 ni kesi 478, zilizofikishwa mahakamani 422 na  zilizokutwa na hatia 31.

Aidha kesi 95 zilifutwa na mahakama, kesi  zinazoendelea mahakamani 296 na zilizofutwa polisi 32. 

Nae Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar George Kazi, alisema kuweko kwa mrundikano wa kesi nyingi mahakamani na kutopatiwa hukumu ni moja ya changamoto zinazoikwaza mahakama kutoka ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) kutokamilisha upelelezi kwa wakati.

Kwa mfano alisema mashahidi wa kesi hizo wamekuwa wagumu kufika mahakamani kutoa ushahidi, hali inayozifanya kesi hizo kuchukua muda mrefu kupatiwa hukumu.

Aidha alisema kuna kesi nyingi katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali zinazosubiri ushahidi wa kitaalamu kama vile vipimo vya mkojo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.