Na Khamis Amani
MKURUGENZI wa Mashitaka Zanzibar (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim, ameshindwa kuwasilisha mahakamani sababu za msingi za kupinga dhamana kwa washitakiwa 10 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiisilamu na badala yake ameamua kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania.
DPP katika kikao kilichopita, alitakiwa na Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyo chini ya Jaji Fatma Hamid Mahmoud kuwasilisha kwa maandishi sababu za msingi za kupinga dhamana kwa washitakiwa hao pamoja na amri nyengine za usikilizwaji wa kesi hiyo.
Hayo yamebainika mahakamani hapo, wakati kesi hiyo ilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa.
Katika kikao hicho, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, Raya Issa Mselem aliiambia mahakama kuwa, DPP hakuridhishwa na maamuzi hayo ya mahakama hasa ya kuwasilisha kwa maandishi sababu za kupinga dhamana kwa washitakiwa hao na kulazimika kuwasilisha rufaa Mahakama ya Rufaa kwa maamuzi.
Hivyo Mwanasheria huyo aliiomba mahakama hiyo kutotoa maamuzi yoyote kuhusiana na kesi hiyo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa maamuzi yake kuhusiana na rufaa hiyo waliyoiwasilisha.
Licha ya upande wa utetezi kupinga hoja hizo za upande wa mashitaka, lakini Jaji Fatma alikubaliana na upande wa mashitaka na kusema hatua waliyoichukua ni haki yao ya kisheria, na kulazimika kuiahirisha kesi hiyo hadi rufaa hiyo itakapotolewa maamuzi.
Lakini hata hivyo Jaji Fatma alisema kuwa, atalazimika kuisikiliza kesi hiyo iwapo Mahakama ya Rufaa itashindwa kutoa maamuzi yake ndani ya siku 60.
Mapema, upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili Salum Taufiq uliiomba mahakama hiyo kutokubaliana na hatua hiyo waliyoichukua upande wa mashitaka na badala yake mahakama ichukue uamuzi unaofaa.
“Mheshimiwa tuliamini upande wa mashitaka watatekeleza maamuzi ya mahakama, kabla ya kuwasilisha rufaa yao Mahakama ya Rufaa walikuwa wanapaswa kuwasilisha amri uliyoitoa katika kikao kilichopita kwanza, lakini kwa makusudi tunaamini wamefanya hivyo ili shauri hili lizidi kupoteza muda bila ya kusikilizwa,”alidai Wakili huyo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Farid Had, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmad Juma pamoja na Abdallah Said.
Wote hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kuharibu mali, uchochezi, ushawishi na kuhamasisha fujo, kula njama ya kufanya kosa na shitaka la nne linamkabili mshitakiwa Azan Khalid la kufanya vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Makosa yote hayo yalidaiwa kutokea kati ya Oktoba 17, 18 na 19 katika maeneo tofauti, mashitaka ambayo washitakiwa wote hao waliyakana.
Hakuna jipya hapo ni ubabaishaji tu, wanajua fika kwamba hawa mashekhe hawana kesi ya kujibu lakini ni mabavu tu ndiyo yanayotumika kuwaweka ndani.
ReplyDeleteKama kweli wanajiamini hao wanasheria wa DPP mbona wanaogopa kuisimamia kesi yao ya msingi, kazi yao ni kukata rufaa zisizo na msingi ili waendelee kuwatesa mashekhe na familia zao jela.
Inashangaza kweli huyu Raya , Huyo Fatma,utafikiri sio waislamu kabisa hata chembe ya ihsani hawana. Ingelikuwa ni mapadri wanaokabiliwa na kesi basi serikali ingewapatia hata nyumba maalumu za kukaa badala ya mahabusu lakini Eleweni Raya na Fatma yuko hakimu muadilifu kuliko mahakimu wote na anawangalia na anarikodi udhalimu wenu, jee mnacho cha kwenda kuwalipa hao mashekhe juu ya dhulma mnayowatendea? Siku hiyo ni nzito hapa duniani ni sehemu ya kuchuma thawabu kwa ajili ya matumizi ya akhera.
Huyo jaji hata zikapita siku 60 atakujua na ngonjera nyengine ili atekeleze maagizo aliyopewa kwamba hawa wasipewe dhamana.
Alikuweko Firauni ambaye akijiita mungu leo yuko wapi na nyie kama mnaringia hizo pumzi zenu kuwadhibu wenzenu iko siku mtakuja kujuta.
Mkumbukeni ALLAH na mtubu kwa makosa yenu. Hizi sheria za duniani ambazo haziendani na maamrisho ya ALLAH ni kujiparia moto mwenyewe.