Habari za Punde

G 20 yashauriwa kuwekeza ndani ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

 Viongozi wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakiimba Wimbo wa Mataifa hayo kabla ya kuanza kwa Mkutano wao wa 11 kwenye Hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha.
Kutoka Kushoto kuelekea kulia ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre Damien Habumuryemi,Rais wa Burundi Bwana Pierre Nkurunziza, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete,Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.
  Baadhi ya Mawaziri wa SMT NA SMZ walioshiriki Mkutano wa Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye Hoteli ya Ngurdogo Mkoani Arusha Tanzania.
Kutoka kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais MBM Dr. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Abdullhabib Fejeji, Waziri wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sita na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Tanzania Mh. Mahadhi Juma
 Rais Uhuru Kenyata wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza baada ya Kuchaguliwa kuwa rais wa Kenya hivi Karibuni.
 Mwenyekiti wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni aliyeshika Kofia akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wenzake wa jumuiya hiyo mara baada ya kumaliza Mkutano wao wa 11 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ngurdoto Mkoani Arusha.
Kushoto ya Rais Museveni ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.
Kulia ya Rais Museveni ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre Damien Habumuryemi pamoja na Rais wa Burundi Bwana Pierre Nkurunziza.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwaongoza Wajumbe wenzake kutoka nje ya Ukumbi wa Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mshariki mara baada wa kumaliza Mkutano wao kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto Mkoani Arusha.
Picha na Hassan Issa wa - OMPR - ZNZ
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Mataifa yanayoendelea kupiga hatua za haraka za Kiuchumi Ulimwenguni ya G. 20 yameshauriwa kuwekeza ndani ya Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } ili kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Mataifa hayo.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.
Rais Museveni alisema Mataifa hayo yenye muelekeo mzuri wa Kiuchumi yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya Miundo mbinu ya Bara bara ,Mawasiliano na hata Sekta binafsi.
Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya Wananchi wake kwa kuimarisha Sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa Serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa Vijana bado ni mdogo.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitolea mfano Taifa lake la Uganda ambalo limejizatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo yao ambao hubaki wakizurura bila ya utaratibu wa kufanya kazi.
“ Vijana popote pale walipo ndio nguvu kazi ya Taifa. Hivyo bado upo umuhimu wa kuwaandalia mazingira mazuri yatakayotoa fursa ya kuyatumikia vyema Mataifa yao “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Museveni wa Uganda.
Akiwahutubia Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar pamoja na Watendaji wao Rais Museveni alimpongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya.
Alisema Wananachi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya wanastahiki kupongezwa kutokana na hatua yao ya kufanya uchaguzi Mkuu katika hali ya amani na utulivu.
Naye akiuhutubia Mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa Kenya Bwana Uhuru Kenyata alisema Kenya inaendelea kujivunia kuwa mwanachama wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki.
Alisema Uanachama huo unasaidia kuendeleza ushirikiano wa ujirani mwema uliopo katika kuimarisha masuala ya Kiuchumi, Forodha, Usafiri wa Anga na hata ule wa Bara bara zinazounganisha Mataifa hayo wanachama.
Bwana Uhuru Kenyata aliwaahidi viongozi wa Jumuiya hiyo kwamba Nchi yake itaendelea kuwa huru kwa mwananchi yeyote wa Jumuia hiyo kuishi au kuwajibika katika shughuli za kiuchumi Nchini mwake kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“ Lengo la waasisi wa jumuiya hii ni kuona Afrika Mashariki inakuwa moja Kiuchumi,Kibiashara, Fedha, Mawasiliano na hata Ustawi wa Jamii “. Alisisitiza Rais Uhuru Kenya.
Alieleza kwamba Wana Jumuiya ya Afrika Mashariki wana wajibu wa kufanya kazi pamoja katika kuona ushirikiano wa Jumuiya hiyo unaendelea kuwa wa kudumu milele.
Akizungumzia suala la Amani Rais Uhuru Kenyata alisema Nchi hiyo itaendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha hali ya ulinzi ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Bara la Afrika.
Bwana Uhuru Kenyata alieleza kuwa matatizo ya ugaidi, sambamba na masuala ya uharamia yanayoikumba pembe ya Bara la Afrika yanaweza kudhibitiwa endapo nguvu za ushirikiano wa pamoja zitadumishwa ipasavyo.
Mkutano huo wa Wakuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika ya Mashariki umemteua Bwana Charles Kackson Njoroge kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Uteuzi unaotarajiwa kuanza rasmi Tarehe 9 June mwaka huu wa 2013.

1 comment:

  1. huu unafiki wa kujidai kuwaweka viongozi waliorubuniwa wazanzibari katika picha hauto wavunja moyo wazanzibari wa kweli wenye kuipenda nchi na maendeleo yao. hao viongozi na matumbo yao makubwa kuna siku yatatumbuka kwa kula fedha za haramu na kuiuza znz kwa watanganyika.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.