Habari za Punde

Jengo jipya la Skuli ya Mwanakwerekwe C kukabidhiwa karibuni

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watuwa China aliyepo hapa Zanzibar Bibi Chen Qiiman akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 
Na Othman Khamis Ame OMKR
 
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China inatarajia kuikabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Mwana kwerekwe C katika kipindi cha siku chache zijazo baada ya kukamilika ujenzi wake.
Ujenzi huo umekuja kufutia ziara ya aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa China Bwana Hui Liangyu ambae ameshastahafu aliyoifanya hapa Zanzibar na kutia saini Mkataba kati ya serikali yake na Zanzibar katika masuala ya Uchumi na Ufundi ukiwemo pia mradi huo wa ujenzi wa skuli ya mwanakwerekwe C.
Mkataba huo uliotiwa saini umelenga kuipatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya RMB Milioni Sitini { 60,000,000 } sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 14.8 ambapo kati ya fedha hizo ujenzi wa skuli hiyo pekee umegharimu jumla ya dola za kimarekani Milioni 1.6.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Chen Qiiman alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi hapo Katika Ofisi yake iliyopo katika Jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Chen Qiiman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wahandisi wa ujenzi huo wako katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa masuala madogo madogo ili baadae ikabidhiwe Serikalini.
Bibi Qiiman alifahamisha kwamba Sera za China zaushirikiano wake na Mataifa ya Bara la Afrika ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa ujumla ilitiliwa mkazo zaidi na Rais wa Nchi hiyo Bwana Xi Jinping wa kati alipofanya ziara yake ya kwanza Nchini Tanzania hivi karibuni tokea achaguliwe kuliongoza Taifa hilo kubwa Barani Asia.
Alimueleza Balozi Seif kwamba kupitia Sera hizo Jamuhuri ya watu wa China itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukijengea mazingira mazuri ya kielimu kizazi chake cha sasa kwa faida ya baadaye.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi ameishukuru China kwa hatua za keza kuendelea kuunga mkono Zanzibar katika kuelekea kwenye maendeleo.
Balozi Seif alisema Jamuhuri ya watu wa China kwa kipindi kirefu sasa imekuwa ikiendelea kuisaidia Zanzibar Kitaaluma na hata uwezeshaji katika Nyanja tofauti za Maendeleo, Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Ujenzi wa skuli hiyo ya msingi ya mwanakwerekwe c ulioanza mapema mwezi agosti mwaka jana na kugharamiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China ulitanguliwa na ule wa skuli ya Msingi ya Kijichi iliyopo Wilaya ya Magharibi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.