• Dk.Shein ataka nchi nzima ifaidike nao.
• Amshukuru Rais Obama.
• Marekani yaahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imelitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuwapatia mikopo wananchi wasio na uwezo wa kuunga umeme katika kipindi hichi ambapo Zanzibar ina umeme wa uhakika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo jana alipozindua mradi wa umeme wa uhakika kutoka Ubungo hadi Mtoni, uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Dk. Shein, alisema baada ya mradi huo kukamilika tatizo la mgao halipo tena, sasa Zanzibar inakuwa na huduma ya uhakika ya umeme, hivyo ni vyema ZECO likaangalia utaratibu wa kutoa mikopo kwa watu wanaotaka kuunga umeme hasa vijijini.
Alisema idadi ya watumiaji umeme kwa sasa ni asilimia 7 kiwango ambacho bado ni kidogo na vyema ZECO likaongeza wateja kwa kuwahudumia kwa njia ya mkopo.
Alisema waya mpya una uwezo wa kuzalisha megawati 100 ambazo zitakuwa ni mara mbili ya mahitaji ya wananchi na ni lazima ZECO watumie kiwango hicho kwa kuongeza wateja wapya.
Sherehe hizo zilizoambatana na furaha kubwa na ngoma za vikundi vya utamaduni na kizazi kipya zilibadilisha Mji wa Zanzibar hapo jana kwa kuuona katika furaha kubwa.
Dk. Shein, alisema matarajio ya serikali ni kuongezeka uwekezaji wa ndani na nje, kwani hilo lilikuwa changamoto kubwa kwa serikali kipindi ambacho Zanzibar haikuwa na umeme wa uhakika.
“Nawasihi wananchi watumie fursa hii ya umeme wa uhakika kuongeza uzalishaji zaidi na kuanzisha shughuli mbali mbali za kujiajiri wenyewe,” alisema.
Alisema waya huo utatoa fursa kwa Zanzibar kuunganishwa kimawasiliano na mkonga wa wawasiliano uliopo Tanzania Bara ili na serikali iziunganishe taasisi zake kimtandao chini ya mradi wa e-Goverment.
Mradi huo umetumia dola za Marekani milioni 64.4 kupitia msaada wa taasisi ya changamoto za millennium ya Marekani na serikali ya Zanzibar imechangia dola milioni 1.5.
Aliwataka wananchi kuthamini mchango huo unaotokana na kodi za wananchi wa Marekani na Zanzibar kwa kuitunza miundombinu ya umeme.
Aliwataka wananchi kutoa mchango zaidi wa ulinzi wa miundombinu hiyo kwa kutumia vikundi vya ulinzi shirikishi.
Alilitaka ZECO kuendelea kuwadhibiti wanaounga huduma ya umeme bila kufuata taratibu na kuongeza jitihada za kukusanya madeni kutoka kwa wateja wao na taasisi za serikali.
Aliishukuru Marekani kupitia rais wake Barak Obama kwa mchango wake kufanikisha mradi huo, mradi wa malaria, mradi wa kupambana na ukimwi, mradi wa elimu,teknolojia ya mawasiliano kwa skuli za msingi (T21) na kusaidia mradi wa ujenzi wa bohari kuu ya dawa Zanzibar.
Alimpongeza Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Benjamin Mkapa, Rais mstaafu wa Zanzibar,Dk. Amani Abeid Karume na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa hatua mbali mbali walizozichukua kuanzisha na kuusimamia mradi huo.
Mapema Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Millennium Challenge (MCC),Daniel Yohannes, alisema serikali ya Zanzibar itarajie kupata mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za kijamii baada ya kukamilika mradi huo.
Alisema hatua hiyo ni ya msingi kwa Zanzibar kukamilisha malengo yake ya millennia na kupambana na umaskini.
Kutokana na hiyo ndio maana serikali ya Marekani ilikubali kusaidia Tanzania kutekeleza miradi ya nishati, huduma ya maji na umeme.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, ALfonso Lenhardt, alisema Maerekani imefurahi kuona mradi huo unakamilika jambo ambalo litaifanya nchi hiyo kuendelea kutoa misaada kwa Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Khalil Mirza, akitoa maelezo ya kitaalamu juu ya mradi huo alisema serikali ya Zanzibar katika mradi huo imechangia dola za Marekani milioni 1.4 ambazo zilitumika kulipia fidia wananchi huku shirika la umeme Zanzibar (ZECO)likitoa dola za Marekani 400,000.
Waziri wa wizara hiyo, Ramadhani Abdalla Shaaban, aliwashukuru wananchi kwa kuwa wavumilivu katika kipindi chote huduma hiyo ilipokosekana.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, aliwataka wananchi kuupokea mradi huo na kuhakikisha wanatunza na kuutumia vizuri umeme huo.
Sherehe hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na Rais Mstaafu, Dk.Amani Abeid Karume pamoja na viongozi wengine na wanafunzi wa skuli.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo, Dk.Shein na watendaji wakuu wa MCC walishiriki katika uzinduzi wa mradi huo huko Kituo kikuu cha kurushia umeme Zanzibar kilichopo Mtoni.
No comments:
Post a Comment