Habari za Punde

Viongozi taasisi za umma watakiwa kuzungumza na wafanyakazi

Said Ameir, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa wizara, idara na taasisi za umma kujenga utamaduni wa kuzungumza na watumishi wao ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Alisema katika mikutano hiyo watumishi waelezwe maamuzi mbalimbali yanayofanywa na pia kupewa fursa ya kuuliza na kutoa maoni kuhusu masuala yanayohusu maeneo yao ya kazi.

Dk. Shein alitoa wito huo jana mwishoni mwa mkutano wa kutathmini utekelezaji wa mpango kazi wa kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2012-2013 wa wizara ya Katiba na Sheria pamoja na utekelezaji maagizo yaliyotokana na mkutano kama huo uliofanyika Disemba 2012.

Mkutano huo uliofanyika ikulu ulihudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Alisema utamaduni wa namna hiyo unasaidia kujenga mazingira mazuri kazini na kujenga mlahaka mzuri kati ya watumishi na uongozi.

Alisema katika hali hiyo inakuwa rahisi wakati mwingine kuzungumza masuala yanayoonekana makubwa na kupatiwa ufumbuzi kwa urahisi.

Dk. Shein aliupongeza uongozi wa wizara hiyo kwa kutekeleza maagizo 22 kati ya 24 yaliyotokana na kikao kama hicho kilichofanyika Disemba 2012 na pia kwa kuonesha mafanikio katika utekelezaji wa majukumu ya msingi.

Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakar Khamis Bakary alisema serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za mahakama ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza utoaji haki.

Alisema mbali ya kuboresha mazingira ya kazi kwa kuyafanyia ukarabati majengo ya mahakama idara hiyo pia imepewa nafasi 35 za ajira mpya kuimarisha utendaji.

Aidha amebainisha kuwa baadhi ya watumishi wa idara hiyo katika kipindi cha Julai 2012 na Machi 2013 wamepatiwa mafunzo kuimarisha taaluma na kuongeza weledi katika kutekeleza majukumu yao.

Kuhusu kesi zilizoshughulikiwa, alisema jumla ya kesi za jinai 2,044 kati ya kesi 3,965 na kesi za madai 139 kati ya 453 zilizofunguliwa katika kipindi hicho zimeshatolewa uamuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.