Na Mwajuma Juma
ZIKIWA zimebaki chini ya takriban saa 58 kabla pambano la watani wa jadi Simba na Yanga, Kocha Msaidizi wa timu ya Simba SC Jamhuri Kihwelu, amejigamba kuwa wapinzani wao hawana uwezo wa kuwafunga mabao matano kama walivyoazimia.
Yanga na Simba, zinatarajiwa kutiana mikononi keshokutwa Mei 18, mwaka huu, katika moja ya mechi za kufunga pazia la ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mazoezi ya Simba juzi, ambayo yanafanyika kwenye uwanja wa Mao Dze Tung mjini Zanzibar, Kihwelu anayefahamika sana kwa kuutumia mdomo wake sawasawa, alisema pamoja na majigambo yanayotolewa na Yanga, anaamini kuwa, haina ubavu wa kuifunga Simba mabao hayo ili kulipa kisasi.
Itakumbukwa kuwa, katika mechi ya mzunguko wa mwisho msimu wa ligi kuu Bara msimu ulipita, Simba iliwatafuna mahasimu wao hao kwa kuwachapa mabao 5-0, ambayo hadi leo yamekuwa yakiwaumiza kichwa viongozi wa Yanga, wakifikiri vipi watafuta kipigo hicho.
Kihwelu, maarufu kwa jina la Julio, aliiponda Yanga akisema timu hiyo kwa sasa, uwezo wake ni mdogo kwani imekuwa ikiibuka na ushindi wa idadi ndogo ya mabao katika michezo yake mingi ya ligi kuu.
“Mie nashangaa sana kusikia kuwa wanasema watarejesha mabao hayo, lakini ninawaambia hilo wasitarajie hasa kwa vile sisi tunacheza kiuzoefu zaidi na kama wao ni wakali, wangelianza kushinda katika mechi zao za awali’, alisema.
Kuhusu mashabiki wao wa hapa Zanzibar kupata wasiwasi wakiona mazoezi ya Simba ni mepesi kulinganisha na ukubwa wa mechi dhidi ya Yanga, beki huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema wameshajitayarisha zamani na sasa wanawaandaa wachezaji kikawaida na sio kufanya mazoezi ya nguvu.
“Ina maana wanataka tupande juu ya ghorofa kufanya mazoezi? Sisi tunafanya mazoezi kwa ajili ya kukiweka sawa tu kikosi chetu na si vyenginevyo”, alieleza Julio.
Kwa upande wake, kocha wa timu hiyo Mfaransa Patrick Liewig, alisema hadi sasa, kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi na wala hakuna majeruhi na wachezaji wote wako sawa.
Aliisifia hali ya hewa ya Zanzibar, na kusema inampa faraja kubwa kwamba wachezaji wake watafanya vizuri katika mchezo huo.
Tayari Yanga imeshatwaa ubingwa, na mechi kati yake na Simba, itakuwa ya kulinda heshima tu na kuweka rekodi nzuri kwa timu hizo.
No comments:
Post a Comment