Adai uongozi wake ni sawa na vichekesho vya komedi
Na Abdi Suleiman, Pemba.
LICHA ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa Pemba kudai kuwa kimemfungia kocha mkuu wa timu ya Malindi SC ya Unguja Mohammed Shubeir, kocha huyo ameibuka na kudai hajapokea barua inayomtaarifu juu ya kifungo hicho. Shubeir ameliambia gazeti hili kuwa, taarifa hizo amekuwa akizisikia na kuzisoma katika vyombo vya habari tu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa michezo Gombani, Shubeir amesema licha ya kutokupata barua hiyo, hajawahi kusikia duniani, mwalimu wa timu kufungiwa mwaka msimu mzima wa ligi, labda kusimamishwa kwa mechi chache na kupigwa faini.
“Mimi, hata ningepigwa faini ya shilingi milioni 20 ningetoa, kuliko kusema wamenifungia. Wewe umeona au umesikia wapi mwalimu au kocha, anafungiwa kwamuda wote huo? Hii ni aibu kwa ZFA Taifa Pemba”, alisema Shubeir akikosoa hatua ya chama hicho.
Akiuponda uongozi wa ZFA Pemba, Shubeir alidai ni wa vichekesho, kwani hata msaidizi wake amepigwa faini kwa kitendo cha kwenda kulalamika kwa kamishna wa mechi, huku akionesha shaka kuwa huenda njama hizo zinafanywa dhidi ya timu yake tu.
“Kwa kweli utendaji na hukumu zinazotolewa na ZFA dhidi ya timu ni sawa na komedi kwani dunia nzima hakuna mambo kama hao, labda wanaifanyia Malindi tu. Lazima tuwe makini kwani huku ni kuua soka si kuliendeleza”, alibainisha Shubeir.
Hata hivyo, alisema uongozi wa klabu yake unajipanga kujadili uendeshaji wa ZFA Taifa Pemba, kwa kile alichodai kuwa imeshindwa kusimamia majukumu yake na badala yake inatawaliwa na chuki na maamuzi yaliyojaa ubinafsi, huku akidai haiwezi hata kuongoza mashindano ya kugombea mbuzi.
Alipoulizwa, Kaimu Msaidizi wa ZFA Taifa Pemba Abdallah Suleiman Sharif, alisema kuwa wao hawakupaswa kumkabidhi barua Shubeir, bali kiutaratibu, walipaswa kumpa meneja wake, hatua aliyosema wameifanya, na ni kiroja kudai kuwa hajapewa.
Shubeir ambaye timu yake Malindi imeshuka daraja msimu wa ligi kuu uliomalizika Mei 4, mwaka huu, alipigwa faini ya shilingi laki moja na ZFA Pemba, pamoja na kufungiwa mwaka mmoja, kwa kosa la kumkaba koo mwamuzi msaidizi Mohammed Seif, katika mchezo wa timu yake na Chipukizi uliochezwa Aprili 6, mwaka huu na timu hiyo kulala kwa mabao 2-1.
TATIZO KUBWA LILOPO KATIKA HICHI CHAMA CHETU CHA MPIRA (ZFA) NI VIONGOZI WANAOENDESHA CHAMA HICHI WANA ELIMU NDOGO, NAFIKIRI IMEFIKA TIME KWA NDUGU ZETU WENYE ELIMU NA WENYE UWEZO KUJITOLEA KUSIMAMIA SOKA YA ZANZIBAR
ReplyDelete