Habari za Punde

Wageni Yanga, Simba Azam kikaangoni

 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU za Azam, Simba na Yanga, huenda zikalazimika kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni katika vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao kutoka watano hadi watatu, iwapo kikao cha pamoja kati ya klabu za Ligi Kuu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kitaafiki kanuni mpya, iliyofikiwa katika Azimio la Bagamoyo miaka mitatu iliyopita.


Katika azimio hilo lililohusisha pia viongozi wa klabu, iliafikiwa kwamba kuanzia msimu wa 2013/2014 klabu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni, lakini Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, amesema jana kuwa, watakaa kwanza na klabu kujadili suala hilo, ili kupata maoni yao.


“Lazima tukae kwanza na klabu ili tupate maoni yao. Kwa sababu ilikuwa tuanze mapema tu kutumia sheria hiyo, lakini klabu zikaomba katika Azimio la Bagamoyo tuanze msimu wa 2013/2014”, alisema Osiah.



Haijulikani TFF itaingia na wazo gani katika kikao chake cha pamoja na klabu, lakini kama itatoa fursa kwa klabu zipige kura kuchagua kuendelea na wachezaji watano au kufuata Azimio la Bagamoyo, kuna hatari Azam, Simba na Yanga ‘zikala hasara’.

Hiyo ni kwa sababu wapinzani wao, klabu nyengine 11 hazina wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu na nyingi hazina kabisa, hivyo kama zitataka kupunguza nguvu ya vinara hao wanaotawala Ligi Kuu, zinaweza kupiga kura ya kuunga mkono Azimio la Bagamoyo

Ukiondoa, Azam, Simba na Yanga, klabu nyengine zinazotarajiwa kushiriki Ligi Kuu msimu ujao ni Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, JKT Oljoro, JKT Mgambo, Prisons, Rhino FC, Ashanti United na Mbeya City.

Hata hivyo, kutokana na viongozi wa klabu nyengine kati ya hizo kuwa na mapenzi na timu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga kuna hatari hata kwenye upigaji kura zikapuuza maslahi ya timu zao wanazoziwakilisha.

Azimio la Bagamoyo lilifikia makubaliano ya kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni, ili kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wazawa kwa manufaa ya taifa

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.