Na Hamad Shapandu, Pemba
MAKADA 14 wa CCM wamenusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Micheweni kwenda Konde kisiwani Pemba,kupoteza mwelekeo na kugonga mti.
Gari hilo aina ya Minibus yenye namba za usajili Z505 BQ iliyokuwa ikiendeshwa na Humud Seif Humud ilipata hitilafu hiyo muda mfupi baada ya kuondoka kituo cha magari Micheweni ikiwa imebeba wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM, wilaya ya Micheweni.
Mganga wa hospitali ya Micheweni, Dk. Amour Suleiman Khamis alisema majeruhi wote 14 walifikishwa katika hospitali hio na baadhi yao walikuwa wameumia vibaya.
Alisema abiria 10 walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani, huku wengine wakiendelea na matibabu.
Aliwataja walioumia kuwa ni Salimu Busaga Dida mkaazi wa Makangale, Halima Abeid wa Msuka, Omar Hamad Sheha, Khamis Juma Faki wa Konde, Msellem Kombo, Abdi Said na Amina Khatib Ali wa Msuka.
Wengine ni Riami Khamis Shaame, Ramadhan Omar Ahmed, Hadia Khamis Juma wote wakaazi wa Konde, Juma Omar Khamis wa Kifundi, Muhammad Ali wa Kicha, Kidawa Suleiman Khatib na dereva wa gari hilo, Humud Seif.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis walikuwa miongoni mwa viongozi waliokwenda kuwafariji majeruhi hao na kuwataka wawe na subira katika wakati huu mgumu.
Majeruhi Riami Khamis Shaame na Ramadhan Omar Ahmed walisema gari hilo halikuwa na mwendo wa kasi bali hitilafu za kufunguka ‘tairod’ ndio chanzo cha ajali hiyo.
Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa hususan viongozi wa CCM, wafanyakazi na wananchi wanaendelea kuwajulia hali katika hospitali waliyolazwa.
M/Mungu awajaalie wapone haraka,ili waendelee na majukumu yao ya kila siku.. Aamin
ReplyDelete