Na Rose Chapewa, Morogoro
WATU wawili wamefariki dunia mkoani hapa katika matukio tofauti likiwemo la mmoja kufa kwa kutumbukia mtoni baada ya kunywa pombe kupita kiasi.
Akizungumzia tukio la kwanza,Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema lilitokea Juni 18 mwaka huu saa 8 usiku katika eneo la Kiberege tarafa ya Mang’ula Wilayani Kilombero ambapo Philipo Mwandambo (55) alifariki baada ya kutumbukia mtoni.
Alisema mtu huyo alitumbukia kwenye mto Kinyuku Mang’ula,baada ya kunywa pombe kupita kiasi hali iliyomfanya kushindwa kuvuka wakati akielekea nyumbani kwake.
Kamanda Shilogile alisema chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na ulevi wa kupindukia, hivyo kuwataka wananchi kuacha tabia ya kunywa pombe kupita kiasi.
Akizungumzia tukio la pili alisema mkazi wa kijiji cha Vidunda tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, Anthan Vitalis (38) alikutwa amekufa baada ya kujinyonga na kamba ya Mkonge kwenye mti.
Alisema tukio hilo lilitokea Juni 18 mwaka huu saa 10 alfajiri ambapo inadaiwa marehemu huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili na alishawahi kutibiwa kwenye hospitali ya wagonjwa wa kilimi Milembe mkoani Dodoma.
Hata hivyo, alisema hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi
No comments:
Post a Comment