Habari za Punde

WHO yaipatia Zanzibar vifaa, gari tatu

Na Salum Vuai, Maelezo
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limeipa Zanzibar msaada wa vifaa mbalimbali vya huduma za afya ikiwemo magari matatu.

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ilifanyika jana katika viwanja vya Wizara ya Afya Manazimmoja, ambapo Mwakilishi wa WHO, Dk. Rufaro Chatora, alimkabidhi Waziri wa Afya, Juma Duni Haji.

Vifaa hivyo ni magari matatu, mafriji 11, ‘tags’ 200 za mafriji na 1000 za majokofu, vifaa vya maabara, seti kumi za kufanyia upasuaji, seti 50 za kupimia shinikizo la damu na seti 50 za vifaa vya kuzalishia.

Vifaa hivyo vyote vina thamani ya dola za Kimarekani 122,310 (sawa na shilingi milioni 199,609,920 za Tanzania).

Akizungumza kabla kukabidhi vifaa hivyo, Dk. Rufaro alieleza, ni matumaini ya shirika lake kuwa, msaada huo utatoa msukumo mkubwa katika kuimarisha huduma za afya, hasa vijijini.

Alisema, gari mbili kati ya hizo, ni kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo ya taifa, na nyengine, ni maalumu kwa ajili ya huduma za afya kwa jumla katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Wilaya hiyo ni kati ya zile zilizochaguliwa kuwa mfano katika mpango wa kutathmini mafanikio ya huduma za afya wilayani, zikiwemo 17 za Tanzania Bara, katika uzinduzi uliofanywa na WHO kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania Bara mwezi Septemba 2012.

Aidha, ameahidi kuwa WHO itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa jumla, katika jitihada zao za kuimarisha huduma za afya mijini na vijijini.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar, Waziri wa Afya Juma Duni Haji, alisema serikali inathamini misaada inayopata kutoka Umoja wa Mataifa, ambayo alisema kwa kiasi kubwa kuendeleza huduma za afya hasa maendeleo ya vijijini.

Alisema ni jukumu serikali kuwapatia huduma bora za kiafya wananchi wake, hasa kinamama waja wazito na watoto, ambao wanapaswa kutunzwa ili taifa lipate nguvu ya kuleta maendeleo.

Aliahidi kuwa, wizara yake itavitunza vifaa hivyo kwa manufaa ya wananchi kwa lengo la kuhakikisha vinadumu kwa muda mrefu na kuwaondoshea usumbufu wananchi.

1 comment:

  1. Kama hatujakubali kubadili utamaduni, hata tupewe nini hakiwezi kutusaidia.

    Hayo magari yataishia kwenda mazikoni shamba kila ambapo mfanyakazi atapata msiba...chezea Z'bar wewe!

    Hivi ni visiwa vya kusadikika, ukilaumu sana watu watajidai "sisi waislamu bwana, lazma twende mazikoni"

    Lkn. wanasahau kua fikhi ya mazishi ni 'faradhul-kifaya' kwa maana ya kwamba wakifanya baadhi, wengine jukumu limewaondokea.

    Inakua lazima pale tu ambapo vimetokea vifo vya mripuko. Na kama mtu hana uwezo wa kupeleka shamba mpaka ategemee magari ya SMZ basi azike KWEREKWE au aombe makaburi maeneo ya karibu!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.