Habari za Punde

Dk Shein aufungua masjid Al Aqsa Bambi kijibwe mtu

  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Wazee wa Kijiji cha Kijibwe Mtu Bambi Wilaya ya kati Jimbo la Uzini Unguja, alipofika kuufungua Msikiti masjid Al Aqsa,uliojengwa kwa ufadhili wa Shekh Khalifa Bin Braik na Sheikh Ehab Hashish,kwa usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo Hilo Mohamed Raza Daramsi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akifungua pazia kama ishara ya ufunguzi wa Msikiti masjid Al Aqsa,katika Kijiji cha Kijibwe Mtu Bambi Wilaya ya kati Jimbo la Uzini Unguja,uliojengwa kwa ufadhili wa Shekh Khalifa Bin Braik na Sheikh Ehab Hashish, kwa usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo Hilo Mohamed Raza Daramsi,(kulia)
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(katikati) alipokuwa akiutembelea Msikiti masjid Al Aqsa,katika Kijiji cha Kijibwe Mtu Bambi Wilaya ya
kati Jimbo la Uzini Unguja,mara baada ya kuufungua rasmi,msikiti huo umejengwa kwa ufadhili wa Shekh Khalifa Bin Braik na Sheikh Ehab Hashish, kwa usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo Hilo Mohamed Raza
Daramsi,(kulia)    
 Wananchi na waislamu waliohudhuria katika Sherehe ya ufunguzi wa Msikiti masjid Al Aqsa,katika Kijiji cha Kijibwe Mtu Bambi Wilaya ya kati Jimbo la Uzini Unguja,wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na kuwapa nasaha katika kuuenzi Msikiti huo,uliojengwa kwa ufadhili wa Shekh Khalifa
Bin Braik na Sheikh Ehab Hashish, kwa usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo Hilo Mohamed Raza Daramsi,(kulia)[
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Waislamu na Wananchi wa Kijiji cha Kijibwe Mtu Bambi Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Unguja leo,wakati wa Ufunguzi wa msikiti Masjid Al Aqsa,uliojengwa kwa ufadhili wa Shekh Khalifa Bin Braik na Sheikh Ehab Hashish, kwa usimamizi wa Mwakilishi wa Jimbo Hilo Mohamed Raza Daramsi,(kulia)[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika kuvikomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia  na mmongonyoko wa maadili hapa nchini.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa msikiti, Al-Aqsa ulioko Bambi Kijibwemtu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika hotuba yake hiyo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali inaendeleza juhudi mbali mbali za kupambana na kuvitokomeza vitendo hivyo viovu katika jamii na kusisitiza kuwa mafanikio yake yanahitaji mashirikiano na ushiriki wa kila mmoja.
Alieleza kuwa inasikitisha kuona waathirika wakubwa wa vitendo hivyo vya aibu ni watoto na wanawake, hivyo alitumia fursa hiyo kukumbusha juu ya umuhimu wa malezi bora kwa watoto na suala la kuyalinda na kuyaendeleza maadili mema yaliorithiwa kutoka kwa wazazi pamoja na dini ya Kiislamu.
“Katika siku za hivi karibuni nimekuwa nikikumbusha juu ya umuhimu wa malezi katika shughuli mbali mbali kutokana na kuwepo kwa ongezeko la kesi za unyanyasaji wa kijinsia na mmongonyoko wa maadili….nadhani mnasikia vyombo vya habari vinavyotoa taarifa hizo kila mara:,alisema Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kufunguliwa kwa msikiti huo wenye sehemu ya madrasa katika mwezi huu wa Ramadhani hakika ni neema kubwa kutoka kwa Mola na kuna haja ya kutoa shukurani.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuutumia msikiti huo kama ni sehemu nzuri na yenye utulivu katika kutafuta fadhila na Baraka za Mwezi huu wa Ramadhani kama ilivyoelezwa katika Qur-an pamoja na hadith za Mtume Mohammad (S.A.W).
Pia, alitoa shukurani pamoja na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu familia ya Sheikh Khalifa Bin Braik pamoja na familia ya Sheikh Ehab Hashish kwa mitaji mikubwa waliyoweka katika ujenzi wa msikiti huo.
Aidha, alitoa shukurani na pongezi kwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mhe. Mohamed Raza kwa kujitolea kusimamia ujenzi wa msikiti huo hadi kukamilika kwake.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu kutogombania vyeo katika misikiti  pamoja na kujivisha mwenyewe jogho la uongozi katika misikiti na badala yake ni vyema ukakabidhiwa uongozi na Waislamu wenzio.
Alhaj Dk. Shein aliutaka uongozi wa msikiti huo pamoja na wananchi kwa ujumla kuulinda na kuuenzi msikiti huo na kutoa wito kwa wananchi kuendeleza tabia ya usafi ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira.
Nae Mwakilishi wa Jimbo hilo la Uzini Mhe. Mohammed Raza,  alimuhakikishia Dk. Shein kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wake kwa wananchi wa Jimbo lake na Majimbo mengine pamoja na viongozi wa ngazi zote katika kuleta maendeleo kwenye sekta zote ikiwa ni miongoni mwa wajibu wake kama kiongozi katika jamii.
Alisema kuwa msikiti huo umejengwa kwa muda wa mwezi mmoja na siku moja hivyo msikiti huo ni wa wananchi wa eneo hilo na wanawajibu kuchagua viongozi wanaowataka katika kuouongoza msikiti huo na kuwataka wale wote wanaotoa misaada ya kujengwa misikiti wasiwe na masharti kwa Waislamu.
Katika risala ya wananchi wa Bambi Kijibwemtu, walimueleza Alhaj Dk. Shein jinsi walivyofarijika na msaada huo mkubwa walioupata wa kujengewa msikiti wao kupitia Mwakilishi wa Jimbo lao na kupongeza jitihada zake katika kuwapelekea maendedeleo endelevu katika Jimbo lao.
Wananchi hao walieleza kuwa kabla ya kujengwa msikiti huo walikuwa wakisali katika msikiti mdogo uliopo pembeni mwa msikiti huo ambao ulikuwa umejengwa kwa miti na tope na kuezekwa makuti na kupelekea wakati wa mvua walikuwa wakisali majumbani mwao.
Walieleza kuwa kabla ya hapo walikuwa wakipata tabu sana ya kufuata misikiti kwa ajili ya sala ya ijumaa katika vijiji vyengine ambavyo viko mbali na eneo hilo.
Sambamba na  hayo, wananchi hao walieleza mafanikio waliyonayo pamoja na changamoto zinazowakabili na kutoa pongezi kwa Mwakilishi wao kwa kutimiza ahadi anazoziahidi na asizoziahidi katika Jimbo lao.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika ufunguzi huo akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Naibu Kadhi, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haji Omar Kheir, Masheikh pamoja na wananchi kutoka sehemu mbali mbali kike kwa kiume.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.