MAENDELEO yaliyopatikana na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) katika kipindi cha miaka 47 ya uhai wake, yameelezwa kutokana utendaji makini na ushirikiano kati ya viongozi mbalimbali waliowahi kushika nyadhifa za kuiendesha kwa vipindi tafauti.
Akizungumza katika tafrija ya kuhitimisha wiki ya maadhimisho ya uzawa wa benki hiyo iliyofanyika juzi usiku kwenye ukumbi wa hoteli ya Grand Palace Malindi mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PBZ Abdulrahman Mwinyijumbe, alisema juhudi hizo ndizo zilizoifikisha ilipo benki hiyo.
Alieleza tangu wakati wa meneja wa kwanza wa benki hiyo marehemu Ernest Wakati na wengine waliofuata baadae, taasisi hiyo imekabiliana na changamoto mbalimbali lakini watendaji wake wamejidhatiti kuzifanyia kazi na kuiwezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Kutokana na mafanikio hayo, Mwinyijumbe alisema uchumi wa Zanzibar umeweza kuimarika maradufu, pamoja na wateja wanaotumia benki hiyo kurahisishiwa huduma na kupata fursa za mikopo inayowawezesha kustawisha maisha yao na familia zao.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Juma Amour Mohammed, alieleza matarajio ya taasisi hiyo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni kuzidi kuwasogezea huduma wananchi kwa ukaribu zaidi kwa kufungua matawi sehemu mbalimbali za nchi.
Aliwashukuru viongozi wote waliomtangulia, kwa kuwekea misingi madhubuti ya uendeshaji, busara na hekima ambazo wanaendelea kuzitumia katika kuhakikisha benki hiyo inazidi kuimarika na kuwa mkombozi nambari moja wa wananchi wa Zanzibar na wengine wanaoitumia.
Katika kuthamini mchango wa watendaji wake, benki hiyo iliwapa zawadi na vyeti wateja wake wa muda mrefu, pamoja na kuwatambulisha baadhi ya viongozi wastaafu, ambao kwa namna moja na nyengine, walichangia mafanikio ya benki hiyo.
Zawadi na vyeti hivyo vilikabidhiwa kwao na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Dk. Idrissa Muslim Hijja, aliyekuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye kabla ya hapo, alikata keki maalumu kuadhimisha sherehe hizo.
Benki ya Watu wa Zanzibar, iliasisiwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume, Juni 30, 1966, miaka miwili na nusu tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
No comments:
Post a Comment