Habari za Punde

Tume ya Katiba ijali maoni ya wananchi

Na Salim Said Salim
 
HATUA ya pili ya mchakato wa katiba mpya ya Tanzania imeanza kwa mabaraza ya katiba kukutana na kufanya mijadala.
 
Kinachoshangaza ni kuona baadhi ya vyombo vya habari vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (sio vya umma) havitoi umuhimu kwa kilichokuwemo ndani ya rasimu ya awali ya katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
 
Badala yake vyombo vilivyojibandika heshima ya kuwa vya umma wakati ni vya propaganda ya serikali na chama tawala cha CCM hutoa nafasi kwa kundi fulani la watu kama ni wao tu ndio wanaofaa kusikika na sauti zao ziheshimiwe.
 
Watu hawa hawa ndio wanaosikika katika mijadala ya kuadhimisha mapinduzi, muungano na masuala mengine ya kitaifa.
 
Wananchi wa Zanzibar wanatakiwa wawe kama abiria waliofungwa vitambaa vya macho na hawajui wanakopelekwa na hawana haki ya kuuliza juu ya safari yao.
 
Lakini unapopita vijiweni na kusikia sauti za watu ambao hawapewi nafasi ya kusikika kupitia vyombo hivi vya habari vya serikali unapata mengi. Baadhi yao unaweza kuyaona ni ya kipuuzi, lakini kwa kweli hayafai kupuuzwa.

Tume ya Jaji Warioba imependekeza kuwepo serikali tatu na bado muundo huu wenye taswira ya shirikisho unaelezwa ndani ya rasimu kama muungano badala ya kuitwa shirikisho.
 
Baadhi ya wananchi wamesikika katika warsha zilizofanyika Zanzibar na kudokeza katika mabaraza ya katiba kuwa mfumo wa muungano unaopendekezwa una matatizo kwa jina na muundo.
 
Wapo wanaoona mfumo wa serikali ubadilike na kuwa na jina la shirikisho na sio muungano kwa sababu ipo tofauti kati ya muungano na shirikisho.
 
Wakati Tume ya Katiba imeeleza kuwa wananchi wengi wanataka mfumo wa serikali tatu, viongozi wa CCM bado wanang’ang’ania mfumo wa serikali mbili na wengine kuzungumzia moja.
 
Kwa maana hiyo watu wanaozungumzia haya hawataki kuheshimu maoni ya wengi au sawa na kusema palikuwa hapana faida ya kukusanya maoni ya wananchi.
 
Tunambiwa, ijapokuwa wengine tunayo shaka na kauli hiyo kuwa CCM inaongoza nchi kwa ridhaa ya wengi. Kama kweli viongozi wa CCM wanaheshimu maoni na uamuzi wa wengi kwanini waonekane wanatapatapa kulazimisha kuendelea na mfumo wa serikali mbili?
 
Ni vizuri kwa viongozi wa CCM wakaelewa nchi hii sio mali yao waliyorithishwa kama shamba la familia. Vile vile, sio mali ya CUF, CHADEMA au chama chochote kile kingine cha siasa, bali ni mali ya Watanzania wote.
 
Hata waliotangulia mbele ya haki wanayo haki ya kuheshimiwa makaburi yao.
 
Au ndiyo Watanzania wanaambiwa uundaji wa Tume ya Katiba ulikuwa na lengo la kuwahadaa wananchi na ulimwengu, kama tulivyoona kwa namna zilipotupiliwa mbali ripoti za tume mbalimbali zilizoundwa nchini na Serikali ya CCM?
 
Katika ukusanyaji maoni tumeona sauti ya watu wa Visiwani na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakitaka mfumo wa shirikisho la serikali tatu. Maoni kama hayo yalitolewa na CUF na CHADEMA. Sasa kwanini CCM haitaki kuheshimu maoni ya wengi?
 
Waswahili wanasema mkataa wingi ni mchawi na wengi tunaamini viongozi wa CCM ni waungwana, waaadilifu, sio wachawi na wala washirikina!
 
Kizungumkuti kikubwa ni kusikia baadhi ya viongozi wa CCM na vitimbakwiri vyao visivyokuwa na pahala pa kushika wakisema ati wanaotaka serikali tatu wanataka kuvunja muungano.
 
Sijui wapi wamepata ujabali wa kusema unafiki huu au wanataka kutueleza wachache, kutokana na hicho wanachokiita jeuri ya chama chao ya kutesa, ndio wenye haki ya kufuatwa na wengi kudharauliwa?
 
Wapo ninaoweza kusema ni wanafiki waliokubuhu wanapobwata kuwa wanaotaka shirikisho ni wasaliti. Je, wao wanaotaka mfumo wa serikali mbili (au mbili kuelekea moja) si wasaliti?
 
Wapi imeandikwa katika vitabu vitukufu vya Kuran na Biblia kwamba kidogo, mfano serikali mbili badala ya tatu ndio sahihi. Watu hawa, kwa bahati mbaya wamekuwa na ubavu wa hata kusema wasiotaka serikali mbili wahame nchi (sijui waende wapi).
 
Je, watu hawa wakiambiwa wao wahame nchi na watokomee kwengineko watafurahi? Au ndio itakuwa leseni ya kuwafungulia mashitaka ya kutukana viongozi?
 
Uzoefu umeonyesha maana ya viongozi, kwa mtazamo wa Jeshi la Polisi, ni wale wa CCM na wa vyama vingine wanastahiki kutukanwa na hata kupigwa na wanaofanyia hayo hawaguswi.
 
Ni vizuri kwa viongozi wetu, katika serikali na vyama vya siasa kuelewa kuwa kama hawataki kusulubiwa na wao wasiwasulubu watu wengine.
 
Chanzo - Tanzania Daima

1 comment:

  1. Kwakweli, vyombo vya khabari vimechangia sana kuirudisha nyuma Z'bar kimaendeleo.

    Baadhi ya waandishi wanadhani kufanya 'ufisadi wa khabari' ni kutukomoa sisi wasomaji, wasikilizaji na watazamaji lkn. kumbe pia wanaharibu taaluma zao!

    Kwa miaka kadhaa sasa wanakhabari wa Z'bar hawajiriki tena nje ya visiwa hivi, MZ'bar wa mwisho kwa miaka ya karibuni ni MARIN HASSA wa TBC na MOHD GHASSAN wa sauti ya Ujerumani!

    Hitoria itabaki tu kwa wale wale akina OTHMAN MIRAJI, AISHA YAHYA, SULUMA KASSIM, ZIANA SEIF nk.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.