Habari za Punde

Dkt. Shein Azungumza na Balozi wa Ethiopia.

STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
                                                                    Zanzibar

Septemba 27, 2013
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ofisi za kibalozi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchi za nje hazinabudi kuendelea kuzitangaza vyema sera za uchumi na uwekezaji za Tanzania ili iendelee kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha sekta hizo.

Amesema uchumi wa Tanzania umeonekana kukua vizuri kutokana na mchango mkubwa unaotokana na sekta ya uwekezaji na utalii, hivyo ni vyema mkazo maalum ukawekwa katika kuimarisha sekta hizo nchi za nje.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi mpya wa Tanzania nchini Ethiopia Bibi Naimi Azizi ambaye alifika Ikulu Zanzibar kumuaga.

Rais wa Zanzibar amesema ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia imeanza kufanya kazi miaka mingi iliyopita jambo ambalo siyo tu linatoa fursa ya kipekee katika kufanya shughuli zake kwa ufanisi, lakini hatua hiyo itasaidia pia kuitangaza Tanzania kiutalii na kiuwekezaji katika nchi mbali mbali duniani.

Amefafanua kuwa ingawa sekta hizo zimekuwa zikifanya vizuri, bado fursa ipo ya kuweza kufanya vizuri zaidi, iwapo juhudi za makusudi zitachukuliwa kuzitangaza nchi za nje.

Akizungumzia mfano wa Ethiopia, amesema nchi hiyo kupitia shirika lake la ndege la “Ethiopian Airlines”, linalofanya safari za moja kwa moja nchini Tanzania, linaweza kuwa kichocheo kikubwa katika kukuza biashara ya utalii nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameongeza kuwa, Zanzibar bado inahitaji kupokea watalii wengi zaidi ili kufikia lengo ililojiwekea la watalii 500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2015. Hadi sasa inapokea watalii 200,000 kwa mwaka.

Akizungumzia maendeleo ya lugha ya Kiswahili, Rais wa Zanzibar amemuomba Balozi huyo kusisitiza haja ya kuzungumza lugha ya Kiswahili kila fursa ya kufanya hivyo inapopatikana, kwani alisema licha ya Umoja wa Afrika kukubali kuitumia lugha hiyo, bado matumizi yake hayajafikia kiwango kinachohitajika hasa katika medani za kimataifa.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia Bibi Naimi Azizi ameahidi kuwa atafanya kila linalowezekana kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.