MAADHIMISHO
YA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
MRADI WA KUTOA MIKOPO KWA
WAJASIRIAMALI WADOGO (SELF) NA MKAKATI
WA KUPUNGUZA UMASIKINI WA KIPATO:
Ø SELF ni Mradi wa kutoa mikopo
kwa wajasiriamali wadogo kupitia asasi ndogo na za kati za fedha.
Ø SELF yatimiza miaka 13 ya
huduma ya kutokomeza umasikini nchini.
Ø SELF yaeleza mikakati yake, mafanikio
na changamoto
Tangu mwaka
1961 Serikali ya Tanzania imekuwa inapambana dhidi ya maadui watatu wa
maendeleo yaani; ujinga, maradhi na umasikini. Aidha, Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na MKUKUTA na MKUZA;
inaainishwa changamoto za kuyapata maendeleo na haja ya kuweka vipaumbele. Wakati
tukiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar,12
January 2014, changamoto kubwa inayoikabili Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kama ilivyo kwa serikali nyingine katika nchi zinazoendelea, ni jinsi
ya kutekeleza mipango ya kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki kikamilifu
katika shughuli kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na hatimaye nchi nzima;
ili waweze kuwa na maisha ya viwango vya kuridhisha na kustahimilika kama
vilivyoanishwa katika Malengo ya
Milenia.
Mpango wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA),umeandaliwa
katika nguzo kuu tatu. Nguzo ya kwanza ni ‘’Ukuaji wa Uchumi na Kupunguza
Umaskini wa Kipato.’’ Nguzo hii inaunganishwa kwa karibu na nguzo ya pili ya
‘’Kuimarisha Ubora wa Maisha na Ustawi wa Jamii’’, na nguzo ya tatu ni
‘’Utawala Bora na Uwajibikaji’’ ambayo ni msingi muhimu wa nguzo mbili
zilizotangulia.
Serikali
inatambua kwamba umasikini wa kipato ni chanzo na/au kichocheo cha maradhi na
ujinga katika jamii, ndiyo maana juhudi za dhati zinahitajika ili kuhakikisha kuwa,
sambamba na kupatikana kwa mahitaji ya msingi; chakula, mavazi na makazi, suala
la kuwawezesha wananchi kijikwamua wao wenyewe kiuchumi, ni la msingi kabisa;
hasa ikizingatiwa kwamba uwezo wa Serikali pia una ukomo kutokana na upungufu wa
rasilimali. Hivyo Serikali inatakiwa iandae mazingira mazuri ya kutekeleza
MKUKUTA na MKUZA; yanayoshirikisha jamii kubwa katika masuala ya kiuchumi.
Ndani ya MKUKUTA na MKUZA, imeainishwa miradi na programu mbalimbali kusaidia
Watanzania na hasa wale wa kipato cha chini mijini na vijijini waweze kujiajiri
na kuongeza vipato. Mradi wa SELF ni miongoni mwa miradi iliyoanzishwa, kwa
lengo hili.
Mradi wa kutoa Mikopo kwa wajasiriamali
wadogo (SELF ), ni Mradi wa kutoa mikopo kwa Asasi ndogo za kifedha ili
hatimaye asasi hizo ziweze kutoa mikopo hiyo kwa wananchi
wajasiriamali wenye kipato kidogo waliopo mijini na vijijini.
Lengo kuu la Mradi ni kukuza na kuboresha
upatikanaji wa huduma za kifedha, hivyo kuwapa fursa ya kushiriki katika
shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato ili kuondokana na
umaskini. Ili kufikia lengo hili, Mradi wa SELF unatekeleza shughuli zifuatazo:
1.
Utoaji wa mikopo kwa Asasi za
kifedha kwa lengo la kuwakopesha walengwa wa mradi wa SELF: Ukiwa ni mradi uliojizatiti kikamilifu kuwapa watu masikini
fursa ya kuwa na uchaguzi katika kujipangia maendeleo yao, kupambana na
umasikini, na kujenga msingi bora na imara ya vyanzo vya mapato kwa ajili ya
mahitaji yao ya kila siku; SELF – inatoa mikopo kwa Asasi za kifedha (Mashirika
yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), Kampuni
zinazotoa mikopo (Microfinance Companies), Jumuia za kijamii (CBOs), Benki za wananchi
za maendeleo (Community Banks) ambazo nazo hutoa mikopo kwa walengwa ambao ni
Wanawake,Vijana,Walemavu wake kwa waume, Wakulima na Wajasiriamali wadogo
wadogo. Mikopo hii inatolewa katika kiwango cha riba nafuu; kiwango ambacho
kitaziwezesha Asasi za kifedha kutoa mikopo kwa walengwa wanaofanya shughuli za
uzalishaji mali katika sekta rasmi na isiyo rasmi huku wakimudu gharama zao za
uendeshaji. Mikopo hii inatolewa tu kwa zile Asasi za kifedha zenye uwezo na
sifa nzuri katika kusimamia utoaji wa mikopo kwa kufuata taratibu bora na
sahihi za usimamizi wa fedha.
2.
Kujenga Uwezo: Katika kuhakikisha kuwa yanakuwepo
mazingira mazuri yanayo shajiisha kuwepo kwa huduma endelevu za kuweka na
kukopa, SELF imetenga fedha kwa shughuli zifuatazo:
Ø Kuendeleza Kada ya
Wafanyakazi: SELF imejizatiti katika kutoa mafunzo kwa mujibu wa tathmini ya
mahitaji ya mafunzo kwa wafanyakazi na viongozi wa asasi wabia wa mradi kwa Kada zifuatazo:
·
Wajumbe
wa bodi, kamati za mikopo na usimamizi wa fedha, maafisa mikopo pamoja na
makarani.
·
Wajasiriamali
wadogo walengwa wa mradi ambao ni wabia wa asasi za fedha zinazoshirikiana na Mradi.
·
Maafisa ushirika.
Ø Kuandaa kada ya Wakufunzi na
utayarishaji wa mitaala inayotumika kufundishia.
Ø Kusaidia ukarabati wa majengo
ya ofisi na vitendea kazi pamoja na samani za ofisini kwa asasi wabia wa mradi
3.
Uhamasishaji na Ufuataliaji: Ukiwa kama kielelezo cha jitihada za mwanadamu na matarajio yake katika
mapambano dhidi ya umaskini uliokithiri, mradi wa SELF umeandaa kampeni
mbalimbali kwa lengo la kuuelimisha umma kuhusu shughuli za mradi na kutoa
hamasa kwa wananchi ili waweze kuelewa umuhimu wa kujiajiri, kujipatia mikopo
na kuirejesha mikopo kwa wakati na kwa faida ya wote. Aidha ufuatiliaji na
tathmini ya mara kwa mara ya shughuli za mradi ni nguzo kuu katika kujua
maendeleo yake kwa ajili ya ufanisi.
Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 1999/2000,
ni Mradi uliobuniwa na Serikali na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ili kutoa huduma zilizo endelevu za kifedha kwa
jamii ambayo ilikuwa haijafikiwa na huduma rasmi za kifedha hususani jamii za
vijijini.
Serikali ilikusudia kutumia fedha hizi,
kuanzisha mfuko ambao utatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi kupitia
Asasi za Kifedha. Eneo la mwanzo la shughuli za Mradi wa SELF ilikuwa kwenye
mikoa 6 yaTanzania bara, ambayo wakati huo ilibainika kuwa nyuma kimaendeleo na
kwenye mikoa 5 ya Tanzania visiwani. Mikoa hiyo ilikuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dodoma, Singida na
Dodoma. Mnamo mwaka 2004/05, Serikali iliongeza eneo la Mradi wa SELF kufikia
mikoa 14 ya Tanzania Bara. Mikoa mipya iliyoongezwa ilikuwa Mwanza, Mara,
Ruvuma, Mbeya, Iringa, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi
wa SELF ilikwisha mwaka 2007. Hata hivyo kutokana na mahitaji makubwa ya huduma
za kifedha yaliyoibuliwa na Mradi, Serikali bila ufadhili wa nje iliendelea kugharamia
shughuli za Mradi, husasani uendeshaji. Mchango huu toka Serkalini pamoja na
mapato ya ndani ya Mradi yaliwezesha SELF kuendelea kutekeleza shughuli zake
kwa ufanisi mkubwa na mwaka 2009 mikoa 7 iliyokuwa imebaki kwa upande wa
Tanzania Bara iliongezwa kwenye eneo la Mradi. Mikoa iliyoongezwa ilikuwa ni
Manyara, Shinyanga, Tabora, Kagera, Kigoma, Rukwa na Dar es Salaam. Hivyo Mradi
wa SELF ukawa unatekelezwa, mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mradi wa SELF
umekuwa makini kutekeleza kwa vitendo majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Hali hii
imechangiwa na jitihada za makusudi za SELF zilizofanywa katika kuutangaza
Mradi, kuzihamasisha Asasi ndogo na za Kati za Fedha kuchukua mikopo yenye
masharti nafuuu na kuzifanya ziwe na fikira ya kutoa huduma iliyo endelevu kwa kujenga
uwezo wa kiutendaji kupitia mafunzo yanayotolewa na wataalamu waliobobea katika
masuala ya uendeshaji na usimamizi wa fedha. Aidha vitendea kazi vinavyotolewa
na Mradi vimekuwa ni motisha kwao ya
kutoa huduma vizuri na kuboresha utendaji.
Leo hii SELF sio
tu kwamba imekuwa ya kupigiwa mfano kutokana na sera zake zinazolenga kuleta
maendeleo kwa watu maskini, bali pia kwa mafanikio iliyoyapata ambayo
yanaifanya iwe mfano wa kuigwa miongoni mwa miradi inayosimamiwa na Serikali
inayojishughulisha na utoaji wa huduma za Kifedha, pale ambapo taasisi rasmi,
yaani Benki za biashara zimeshindwa kukidhi mahitaji kutokana na sera, sheria
na taratibu za kibenki. Kimataifa SELF imejijengea umaarufu kutokana na kushika
nafasi ya juu miongoni mwa miradi ya aina hii, inayofadhiliwa na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Uzoefu na mafanikio
yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ya mradi yameiwezesha SELF kuingia katika
awamu ya pili ya utekelezaji iliyoanza Julai 2010 na itamalizika Juni 2015.
Katika awamu hii ya pili ya utekelezaji, Serikali inakusudia kuibadilisha SELF
kutoka kuwa Mradi na kuwa taasisi inayojitegemea.
Katika kipindi cha miaka kumi na mitatu iliyopita, utoaji mikopo unaofanywa na SELF
kwa Asasi za Fedha umepanda kwa kasi na kuweza kuwafikia wananchi wengi wa
kipato cha chini waliopo mjini na vijijini kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali
hapo chini.
Kupanuka kwa Huduma za Kifedha Vijijini
na Mjini
Mwaka
|
02/03
|
03/04
|
04/05
|
05/06
|
06/07
|
07/08
|
08/09
|
09/10
|
10/11
|
11/12
|
12/13
|
1.Idadi ya Asasi za Kifedha
|
21
|
39
|
70
|
71
|
56
|
186
|
155
|
203
|
301
|
323
|
364
|
2.
Thamani ya mikopo kwa Asasi ‘’Tshs 000’’)
|
665,450
|
1,513
|
3,465
|
2,733
|
3,769
|
3,283
|
5,752
|
6,859
|
9,014
|
10,248
|
9,843
|
3.
Idadi ya wananchi waliokopeshwa
|
7,083
|
12,325
|
20,526
|
37,364
|
54,058
|
60,016
|
65,809
|
73,025
|
80,454
|
88,083
|
93,364
|
4.
Jamii iliyonufaika
|
28,332
|
49,300
|
82,104
|
149,456
|
216,232
|
240,064
|
263,236
|
292,100
|
321,816
|
352,332
|
374,560
|
Hadi kufikia Juni 2013 tayari SELF
ilikuwa imeshatoa mikopo yenye thamani ya bilioni 52.3 kwa asasi za kifedha
zipatazo 364 (asilimia 60 kati ya hizo ni za vijijini). Mikopo hii imesaidia kukuza shughuli ndogo za kiuchumi na kunufaisha
zaidi ya wateja wapatao 93,372 ambao kati ya hao 58% ni wanawake. Aidha,
watu wapatao 374,560 kwa njia moja au nyingine wamenufaika na mikopo hii.
Mafunzo yanayotolewa na Mradi wa SELF kwa
viongozi na watendaji wa asasi ndogo na za kati za fedha yanalenga kuwajengea
uwezo juu ya utawala bora,usimamizi wa shughli za fedha na mikopo. Wajasiriamali
wadogo wanaokopa toka asasi wabia wa SELF nao pia hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali
na stadi za biashara. Mafunzo haya yanalenga kuwaongezea ujasiri wa kuthubutu
na kuongeza ubunifu katika biashara zao ili waweze kuwekeza vizuri kwenye mikopo
wanayoipata kwa kuifanyia biashara kwa njia za kitaalamu zitakazo waongezea tija
kwenye biashara zao.
Jedwali lifuatalo linaonyesha idadi ya wabia
wa mradi walionufaika na mafunzo toka Mradi mradi ulipoanza hadi kufikia Juni
2013.
Idadi ya Viongozi, Watendaji wa Asasi za kifedha,
Wajasiriamali wadogo na Watoa Huduma walionufaika na Mafunzo toka SELF.
Kundi
|
2000
- 2009
|
2010
- 2013
|
Jumla
|
Viongozi na Watendaji wa Asasi za kifedha
|
2,486
|
1,042
|
2,551
|
Wajasiriamali wadogo
|
3,175
|
4,558
|
5,649
|
Watoa huduma (Maafisa Ushirika ngazi ya
wilaya)
|
208
|
180
|
240
|
Mradi wa SELF umekuwa ukihakikisha huduma
za fedha zinazotolewa zinakuwa endelevu kwa wabia wake, ili wananchi wengi
zaidi hasa maeneo ya vijijini waweze kunufaika na huduma za kifedha. Mradi wa
SELF umekuwa ukihamasisha wabia wake kutoa huduma katika mazingira yaliyo bora,
salama na yenye mvuto, ili wananchi wengi waweze kuhamasika na kujiunga kwenye
huduma za kifedha.
Hadi kufikia mwezi June 2013, Mradi wa
SELF tayari ulikuwa umetoa jumla ya T.sh. 75,374 milioni kwa asasi za fedha 68 inazoshirikiana nazo katika kuhakikisha huduma
za kifedha zinawafikia wananchi kwa wingi zaidi, katika mazingira yaliyo salama
na kisasa zaidi. Kiasi hicho kimeziwezesha asasi hizo kununua samani za ofisi, vitendea
kazi kama vile kompyuta, mashine za kudurufu na kusikani karatasi, pikipiki,
kasiki, baiskeli, kukarabati majengo pamoja na kuandaa mikutanao kwa ajili ya wanachama
wao.
Mikopo inayotolewa kwa wabia wake pamoja na vitendea
kazi vya ofisi wanavyopewa wabia wa SELF, umezifanya asasi hizi kuongeza ufanisi
na kuimarisha utoaji huduma kawa katika viwango bora kabisa, na kuzifanya asasi
hizo ziweze kukua toka kwenye kiwango cha chini cha utoaji huduma hadi kwenye kiwango
cha kati, na zile asasi za fedha zilizo kuwa kwenye kiwango cha kati kukua na kufikia
kiwango cha juu cha utoaji huduma.
Hadi
kufikia mwezi June 2013, asilimia 12 ya wadau wanaoshirikiana na Mradi,
wameweza kukua toka kiwango cha chini kabisa cha utoaji huduma hadi kiwango cha
kati, wakati asilimia 3.4 ya asasi za fedha zilizo kwenye kiwango cha kati
zimeweza kufikia kiwango cha juu kabisa cha utoaji huduma za mikopo. Asilimia
31 ya wadau wa kiwango cha chini, waliweza kuimarisha huduma zao ndani ya kiwango
hicho na kuanza kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama wake. Kukua huku ni
muhimu, ili kuibua Asasi za kifedha endelelevu ambazo zitaendelea kutoa huduma
bora za kifedha kwa jamii na hivyo kukuza uchumi na kuboresha maendeleo ya
jamii nzima.
Akizungumza
katika moja ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Warajisi Wasaidizi na Maafisa
Ushirika wa Mikoa ya Tanzania bara na visiwani, Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani
Ms. Beatha Swai, aliwataka Maafisa ushirika wa mikoa yote waongeze bidii katika
kuwaelimisha viongozi wa SACCOS ili waweze kuzifahamu sheria za ushirika vizuri,
hivyo kuweza kuimarisha utendaji na usimamizi wao wa kazi. “ Mnatakiwa msimamie vizuri Sheria ya Ushirika kwa viongozi wa SACCOS kwa
kufuata misingi na kanuni za ushirika, ili kuongeza uelewa kwa viongozi wa SACCOs ili waweze kusimamia shughuli zao vizuri”
Bw.
Abdulhaman Mohamed Hassani, ambaye ni Katibu Mkuu wa taasisi ya kutoa mikopo ya
Jumuiya ya Changamoto ya Unguja (Changamoto Life Preservation Fund),
iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ya Saateni na
maeneo yanayozunguka; anasema kwamba; awali taasisi ilisajiliwa kama chama cha kuweka
akiba na kukopa (SACCOS). Lakini kufuatia utendaji mzuri na uhitaji mkubwa wa
huduma za kifedha uliokuwepo , uongozi uliamua kuongeza wigo wa kutoa huduma na
kuamua kubadilisha usajili wa SACCOS, na kuwa chama cha kijamii mwaka 2007. Anasema
Mradi wa SELF umeweza kukidhi mahitaji ya asasi yao kwa kuongeza mtaji kupitia mikopo
wanayoichukua SELF. Anaendelea “…..kutokana
na kuongozeka kwa mtaji tumekuwa tukitoa mikopo kwa wakati kwa wanachama wengi
zaidi tofauti na hapo awali, hivyo kuwafanya wanachama wetu kufanya biashara
kwa uhakika zaidi kwa kujiamini. Ajira 2,700 zimeweza kupatikana baada ya wajasiriamali
kuweza kupanua biashara zao”
Bw.
Abdulhaman Mohamed Hassani anaelezea jinsi mafunzo yaliyotolewa na Mradi wa SELF
kwa viongozi, na wajasiriamali wa asasi yao, yalivyoboresha na kuongeza ufanisi
wa utendaji kwa viongozi na kuwafanya kuongeza nidhamu ya fedha, kitu
kilichokuwa kikwazo kikubwa katika usimamizi wa asasi yao hapo awali, “……kwa upande wa wajasiriamali, mafunzo ya ujasiriamali kuhusu
stadi za biashara, usimamizi wa biashara na elimu ya ujasiriamali, yamewaongezea
ujasiri mkubwa wa kuthubutu na kuwa wabunifu katika biashara, hali inayowafanya
waweze kusimamia biashara zao kwa kujiamini”
“Vile
vile SELF imetusaidia kukarabati ofisi yetu, imekuwa ya kisasa na kuvutia zaidi;
hali inayotufanya tuaminike na kutambulika kwa wadau wengi zaidi. Nawashauri
wananchi wajiunge kwa wingi kwenye taasisi za kifedha, ili waweze kunufaika na
mikopo ya masharti nafuu, ni vigumu kufikiwa
na huduma za kifedha kwa mtu mmoja mmoja’’, anasema Bw. Abdulhaman Mohamed
Hassani.
Bw.
Ally Adam Ally ni Mwenyekiti wa Serena SACCOS, ambayo imekuwa miongoni mwa
wanufaikaji wa huduma za fedha toka Mradi wa SELF. Yeye anasema, katika maeneo
yote ambako SELF imewafikia wananchi, imekuwa mkombozi mkubwa kwao hasa
kutokana na kutoa mikopo yenye masharti na riba nafuu inayowawezesha watu wa
kipato cha chini kuimudu.
Anasema tofauti
na asasi nyingine za kifedha kama benki na kampuni binafsi ambazo huweka
masharti magumu yanayohitaji dhamana, SELF imejidhirisha kuwa tofauti kabisa na
asasi hizo.
“Tumeweza
kuboresha maisha yetu tofauti na awali, kupitia mikopo ya SACCOS yetu, tumeweza
kuboresha maisha yetu, tumenunua vyombo vya moto kama pikipiki, magari na
kuboresha makazi yetu kwa kupitia mikopo, vilevile ada za watoto na zetu sisi
wenyewe zimekuwa zinapatika kwa urahisi sana tofauti na awali”, anasema Mwenyekiti
Ally Adam Ally.
Akizungumza na
Majira katika mahojiano maalum, Meneja wa Mradi wa SELF Bw. Abiah Kaaya,
anasema pamoja na mafanikio ambayo SELF imeyapata katika kipindi cha takribani
miaka kumi na tatu tangu kuanza huduma zake, bado kumekuwa na changamoto
mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo katika kutekeleza na kutimiza malengo ya
Mradi wa SELF.
‘’Utoaji wa huduma za Kifedha kwa
wananchi wa kipato cha chini ni dhana iliyoshamiri miaka ya karibuni hapa
Tanzania; Asasi zinazofanya shughuli hii zimejikita zaidi mijini na kwenye
maeneo yenye shughuli kubwa za kipato. Aidha upatikanaji wa huduma hizi katika
maeneo ya vijijini umekuwa bado uko katika kiwango cha chini, ambapo huwa ukifanyika
kwa utaratibu ambao si rasmi kutokana na kutokuwepo kwa Asasi zinazotambulika
kisheria.
Aidha, kwenye maeneo ambayo kuna Asasi
za kifedha zinazotoa huduma, kutokana na
udhaifu wa kiutendaji, hususan upungufu wa wafanyakazi wenye ujuzi utoaji wa
huduma ni duni na hazikidhi matakwa ya walengwa. Wafanyakazi wenye ujuzi mdogo
wamelazimika kuwa na majukumu mengi kwa wakati mmoja tofauti kabisa na uwezo
wao, utawakuta wakati mwingine wakifanya
kazi kama Mameneja, Maafisa Mikopo na Wahasibu. Katika utendaji kazi wa aina
hii, udhibiti na utunzaji wa fedha umekuwa tatizo kubwa; ni dhahiri kabisa kwa
asasi za aina hii kukabiliwa na hatari kubwa ya kushindwa kutoa huduma zilizo
endelevu kwa sababu ya zisizoridhisha zitolewazo na wafanyakazi wasio na
uzoefu, hali hii inapelekea kupoteza
pesa’’, anaeleza Meneja wa Mradi.
Anaeleza
kuwa changamoto nyingine inayozikabili Asasi za kifedha ni wananchi kuwa na
uelewa mdogo juu ya masuala kifedha, yahusuyo mikopo, akiba, riba n.k.; hivyo kushindwa
kutoa maamuzi sahihi kuhusu dhana nzima ya matumizi ya akiba na mikopo, ili
kuongezea kipato na hivyo kujikwamua kiuchumi. Aidha, mapungufu ya elimu hii,
inafanya wananchi kushindwa kufanya tathmini ya fursa zilizopo ili kuzitumia
vizuri kwa manufaa yao. Kuondokana na changomoto hii, Meneja wa Mradi wa SELF
anashauri asasi za fedha ziwe zinatoa elimu kwa wateja, wanachama na wananchi, ili
waweze kuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kutumia mikopo hiyo vizuri na kuwafanya
wafanye shughuli kwa malengo na mitizamo iliyo endelevu. Kwa upande wa viongozi
wa asasi za fedha, baadhi yao wamekuwa na uelewa mdogo wa masula ya kifedha,
hali inayowafanya washindwe kubuni vyanzo vingine vya mapato vilivyo imara na
kutegemea zaidi vyanzo vilivyopo tu. Viongozi na watendaji hawana budi kuelewa
kuwa kuendelea kuwepo kwa asasi zao kutategemea zaidi uwezo wao wa kubuni
mikakati itakayoziwezesha Asasi za fedha kuwa endelevu. Mikakati hiyo ni pamoja
na kupanua wigo wa eneo na huduma wanazotoa, kubuni vyanzo vipya vya mapato,
kudhibiti gharama za uendeshaji, kuboresha urejeshwaji wa mikopo na kudumisha
uongozi bora.
Anaendelea kueleza kuwa, tabia na mawazo
potovu yatokanayo na mila na desturi kuhusu mikopo, hasa ile itolewayo na
Serikali imekuwa changamoto kubwa inayofanya viwango vilichokusudiwa na
Serikali, vya kuifikishia mikopo jamii pale ilipo hasa sehemu za vijijini,
visifikiwe. Vilevile kuna desturi kwa baadhi ya jamii kuona mikopo kama chombo
kinachodhalilisha au chombo kinachotumika kuwakandamiza na kuwarudisha nyuma
kimaendeleo, pindi wanaposhindwa kulipa mikopo kwa wakati.
Utawala mbovu wa baadhi ya viongozi wa
Asasi za kifedha, ambao umekuwa hauzingatii misingi ya utawala bora, usiofuata utaratibu
uliowekwa wakati wa uchaguzi na usio zingatia huru na haki kwa viongozi wengine
umekuwa changamoto kubwa ya kuhakikisha huduma za kifedha zinatolewa katika
mzingira huru na ya haki. Viongozi wamekuwa wakiingilia kazi za meneja na
kuwafanya wafanye kazi katika mazingira magumu, yasio huru hivyo kushindwa
kusimamia majukumu yao vizuri, hiyo ni mojawapo ya changomoto zinazoelezwa na Meneja,
kwa asasi za fedha.
Anataja
changamoto nyingine inayozikabili Asasi za kifedha kuwa ni kutumiwa vibaya fursa
ya kuwepo kwa taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo. ‘Lipo tatizo kwa baadhi ya
Asasi za fedha kutumia vibaya fursa ya kuwepo kwa taasisi nyingi zinazotoa
mikopo kwa kuchukua mikopo mingi kwa
wakati mmoja toka kwa wakopeshaji tofauti kuliko uwezo wake wa kuitumia na
kuisimamia, hivyo kuwa na mikopo mingi isiyolipika hali ambayo inapunguza
ufanisi na uendelevu wa asasi hizo’’. Anasema juhudi za Serikali za kuhakikisha
kuwa kila mwananchi anapewa kitambulisho cha utaifa, ambazo zinaendelea sasa, pamoja na kuanzishwa chombo
kitakachokusanya taarifa za wakopaji (credit bureau), vitatoa ufumbuzi wa tatizo
hili; kwa sehemu kubwa.
Meneja wa Mradi wa SELF, anawashauri
wananchi waache kuwa na mawazo potofu, na wajiunge kwa wingi kwenye asisi za
fedha zinazotoa mikopo yenye riba nafuu, ili waweze kunufaike na mikopo hiyo
kuwafanya washiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishajimali, na kuongeza
vipato miongoni mwao na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa wananchi.
thats nice
ReplyDelete