Habari za Punde

Dk Shein amtumia salamu za pongezi Rais Jacob Zuma wa Afrika KusiniSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                              27 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amempelekea salamu za pongezi Rais Alfred Jacob Zuma wa Jamhuri ya Afrika Kusini kwa ushindi wa chama chake cha African National Congress (ANC) na yeye kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo kwa kipindi  cha pili.
 
Katika salamu zake hizo Dk. Shein amemueleza Rais Zuma kuwa kuchaguliwa kwake tena na hatimae kuapishwa rasmi kuongoza nchi hiyo ni uthibitisho wa imani waliyonayo kwake wananchi wa Jamhuri ya Afrika Kusini.
 
“Ni furaha kubwa kuona ndugu zetu wa Afrika Kusini wameonesha tena imani yao kwa uongozi wako na wa Chama cha ANC. Sisi tunaamini kuwa uhusiano wa kidugu kati ya nchi zetu utaimarishwa kwa manufaa ya watu wetu” Dk. Shein alimalizia salamu hizo.
 
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amempongeza Mheshimiwa Narendra Modi kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa India kufuatia uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.
 
Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu huyo mpya Dk. Shein alisema “tunakupongeza kwa ushindi wako ambao unadhihirisha imani waliyonayo wananchi wa India kuwa utaliongoza taifa hilo katika ngazi mpya ya maendeleo na mafanikio”
 
Salamu hizo zimeeleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanatarajia kushuhudia kipindi kipya cha kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na India.
 
Dk. Shein amemtakia afya njema na mafanikio Waziri Mkuu Narendra Modi katika kutimiza matarajio ya wananchi wake.
 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.