Habari za Punde

Zanzibar itaendelea kuthamini misaada inayotolewa na Serikali ya Misri

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na balozi mdogo wa Misri anayemaliza muda wake balozi Walid Ismail, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na balozi mdogo wa Misri anayemaliza muda wake balozi Walid Ismail, ofisini kwake Migombani.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na balozi mdogo wa Misri anayemaliza muda wake balozi Walid Ismail, ofisini kwake Migombani.
Picha na Salmin Said OMKR

Na: Hassan Hamad, OMKR.
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuthamini misaada inayotolewa na Serikali ya Misri katika kuendeleza na kukuza uchumi wa Zanzibar.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameeleza hayo ofisini kwake Migombani, wakati akizungumza na balozi mdogo wa Misri anayemaliza muda wake balozi Walid Ismail.
 
Amesema Serikali ya Misri imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na ustawi wa jamii zikiwemo elimu, afya na kilimo.
 
Aidha amesifu mchango wa balozi huyo katika kipindi chake cha utumishi kwa kufanya mambo mengi mazuri yanayohitaji kuendelezwa na mwenzake atachukua nafasi yake hapa nchini.
Maalim Seif amesema mbali na balozi huyo kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini, bado anayo fursa na kuchangia maendeleo ya Zanzibar kwa kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar nje ya nchi, sambamba na kuwahamasisha wawekezaji na watalii kuja kuitembelea Zanzibar.
 
Mhe. Maalim Seif pia alitumia fursa hiyo kuipongeza Misri kwa kufanikisha uchaguzi wa Rais kwa amani na utulivu, na kuelezea matumaini yake kuwa wananchi wa nchi hiyo wataendelea kuishi kwa amani na usalama.
 
Nae balozi mdogo wa Misri anayemaliza muda wake wa utumishi hapa nchini balozi Walid Ismail, amesifu ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi na wananchi wa Zanzibar katika kutekeleza majukumu yake ya kibalozi.
 
Amesema Zanzibar ni kituo kizuri cha kufanyia kazi kutokana na ukarimu wa watu wake, pamoja na kuwepo amani na usalama kwa wakati wote.
 
Balozi Walid Ismail ameahidi kuwa akiwa nje ya Zanzibar ataendelea kuthamini mafanikio aliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa uhusiano kati ya Zanzibar na Misri.
 
Akihitimisha mazungumzo yake, balozi Walid alimkabidhi Makamu wa Kwanza wa Rais, zawadi maalum kama ishara ya ushirikiano mwema kati yake na viongozi pamoja na wananchi wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.