Habari za Punde

Mallim Seif afungua mkutano wa kimataifa wa SOS

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Mwenyekiti wa bodi ya SOS Zanzibar Mohd Bhaloo, wakati akiwasili Zanzibar Beach Resort kufungua mkutano wa kimataifa wa SOS.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa vijiji vya SOS, Zanzibar Beach Resort.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya SOS Zanzibar, Zanzibar Beach Resort.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa siku tano wa Kimataifa wa vijiji vya SOS unaofanyika Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa Kimataifa wa  SOS unaofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort. (picha na Salmin Said, OMKR)
 
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Kiasi cha watoto milioni 153 wanaishi bila ya uangalizi wa wazazi duniani kote, huku Tanzania ikiwa na watoto wa aina hiyo wapatao kumi na moja elfu, mia mbili na kumi na sita (11,216).
 
Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa siku tano kwa nchi wanachama wa vijiji vya SOS, unaofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.
 
Pamoja na mambo mengine mkutano huo unajadili namna ya kukuza uelewa katika uendelezaji wa vijiji vya watoto vya SOS, pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto zinazovikabili vijiji hivyo.
 
Maalim Seif amesema idadi ya watoto wanaokosa uangalizi wa wazazi imekuwa ikiongezeka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo kufariki kwa wazazi, hali ya umaskini, unyanyasaji  pamoja na talaka.
Amefahamisha kuwa matokeo ya hali hiyo ni kuongezeka kwa ajira za watoto ambapo  Zanzibar pekee inakisiwa kuwa na asilimia tisa nukta mbili (9.2) ya watoto kati ya umri wa miaka mitano hadi 17 wanaojihusisha na ajira hizo.
 
Amesema katika kukabiliana na tatizo hilo, juhudi za pamoja zinahitajika kati ya taasisi za umma na binafsi, kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa, sambamba na kuzisaidia familia zenye watoto yatima na zinazoishi katika mazingira magumu.
 
Amesema Serikali kwa upande wake inaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na SOS Zanzibar na Tanzania, na kuzitaka taasisi hizo kuzidisha bidii katika kuleta ufanisi.
 
Ameelezea matumaini yake kuwa kampeni ya CARE FOR ME  iliyozinduliwa na vijiji vya SOS mwaka 2012, italeta faraja na mafanikio kwa kuwapatia watoto huduma bora zikiwemo za kielimu.
 
Ameyashukuru mashirika ya misaada ya Norway (NORAD), Austria (ADA) na Denmark kwa kuunga mkono miradi ya SOS, hatua ambayo amesema inaisaidia Serikali kukabiliana na matatizo yanayowakabili watoto.
 
Mapema akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa bodi ya vijiji vya SOS Zanzibar Bw. Mohd Bhaloo, amesema SOS Zanzibar imekuwa imewahudumia watoto wapatao mia nane (800) kwa kuwapatia elimu bora, kupitia  skuli ya msingi na sekondari ya Hermann Gmeiner iliyo chini ya kijiji hicho.
 
Amefahamisha kuwa SOS Zanzibar pia ina kituo cha afya ambacho hutoa huduma kwa watoto wa kijiji hicho pamoja na wananchi wa maeneo ya karibu ambapo zaidi ya wagonjwa elfu moja na mia nne (1,400) hupatiwa matibabu katika kituo hicho kwa mwaka.
Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine SOS Zanzibar kupitia mpango wake wa kuwajengea uwezo watoto, inazisaidia familia 180 zenye watoto elfu moja Unguja na Pemba, ili ziweze kuimarisha huduma kwa watoto hao.
Akizungumzia kuhusu historia ya vijiji vya SOS Zanzibar, Bhaloo amesema azma ya kuanzishwa kwa vijiji hivyo iliasisiwa mwaka 1984 na kuanza kuwahudumia watoto kuanzia mwaka 1991.
Ameishukuru Serikali na taasisi binafsi kwa ushirikiano wao katika kuunga mkono juhudi za vijiji vya SOS, na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana tokea kuanzishwa kwa vijiji hivyo hapa nchini.
Mkutano huo wa siku tano unazishirikisha nchi mbali mbali zenye vijiji vya SOS zikiwemo Austria, Cameroon, Ethiopia, Malawi, Mozambique na Morocco. Nchi nyengine ni Uganda, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Tanzania na wenyeji Zanzibar.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.