Habari za Punde

Waziri Haroun Apokea Tende Tani 25 Kutoka kwa Mfalme Salman

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais,Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman  Akipokea sadaka ya tende kutoka kwa Balozi wa Saudia Nchini Tanzania iliyotolewa na  taasisi ya misada ya kibinaadamu ya mfalme  Salman wa Saudia Arabia,huko Sheria house Mazizini Mjini Zanzibar.
Balozi wa Saudia Nchini Tanzania Yahya Ahmad Okeish Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya sadaka ya tende kutoka taasisi ya misada ya kibinaadamu ya mfalme  Salman wa Saudia Arabia huko Sheria house Mazizini Mjini Unguja.

Na Fauzia Mussa – Maelezo

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais,Katiba, Sheria,Utumishi na utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman amepokea tani 25 za tende kutoka taasisi ya misada ya kibinaadamu ya mfalme  Salman wa Saudia Arabia .


Akizungumza mara baada ya  kupokea sadaka hiyo  huko Sheria house Mazizini Mjini Unguja Waziri Haroun amesema Serikali imekua ikipokea misaada mbalimbali kutoka Nchi hiyo ikiwemo nyama na tende kutokana na mapenzi, umoja na mashirikiano yaliopo baina ya Tanzania na Saudia arabia.

 

Hivyo  Waziri Haroun ameahidi kuendeleza kudumisha umoja na masharikiano yaliopo baina ya  Nchi mbili hizo kwa maslahi ya wazanzibari  na Taifa kwa ujumla.


"Mapenzi baina ya nchi mbili hizi yanazidi  kuiimarika siku hadi siku hasa upande wa Zanzibar, kupewa tani 25 kati ya   75  zilizotolewa kwa Tanzania yote ni jambo linalodhirisha upendo, kwaniaba ya Serikali tunamshukuru Mfalme wa Saudia kwa sadaka hii  na tunaahidi kuyadumisha mapenzi haya" alieleza mwalim Haruna.


Kwa upande wake Balozi wa Saudia Nchini Tanzania Yahya Ahmad Okeish  amesema jumla ya tani  75 za tende zimetolewa na Mfalme wa Saudia kama sadaka  kwa  Nchi ya Tanzania  ambapo tani 25  ni kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar, 25 Tanzania bara na 25 kwaajili ya watu maalum ikiwemo wakimbizi.


Alieleza kuwa mapenzi yaliopo kati ya Nchi mbili hizo yamesababishwa na  undugu wa dhati uliopo kati ya Tanzania na Saudia unaolinganishwa katika  mambo mbalimbali ikiwemo tabia ,silka, tamaduni  na hata desturi za Nchi hizo.


Mapema Balozi Okeish amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais  Katiba na sheria Mwalimu Harun Ali Suleiman kwa  hatua walizochukua hadi kuhakikisha sadaka hiyo inaingia Zanzibar pamoja na Taasisi zote zilizosaidia kufanikiwa kwa kufika sadaka hiyo Nchini.


Nae Katibu Mtendaji Kamisehni ya Wakfu na mali ya Amana Sheikh Abdalla Talib Abdalla  ameishukuru Serikali ya Oman kwa sadaka hiyo  na kuahidi kuwa itawafikia walengwa.


Amefahamisha kuwa miongoni mwa majukumu ya kamisehni hiyo ni kupokea na kugawa sadaka kwa wenye uhitaji hivyo amesema  kwa kushirikiana na taasisi za kidini  sadaka hiyo itagaiwa  kwa  kila anaestahiki.


"Sadaka hii tutaipeleka katika familia mbalimbali zenye uhitaji,

mahospitalini ambako kuna wagonjwa wetu, vituo vya kulelea watoto yatima na vituo vya kutunzia wazee katika Shehia zote za Unguja na Pemba" alieleza sheikh Abdalla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.