Habari za Punde

SMZ yazuia kiwanja cha watoto kutumika Sikukuu Idd El Fitr

Na Rahma Suleiman
 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kiwanja cha kufurahisha watoto kilichopo eneo la Kariakoo, mjini Unguja, hakitatumika katika Sikukuu ya Idd El Fitr, mwaka huu, kutokana na ujenzi wake kutokamilika.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua kiwanja hicho, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee, alisema dhamira ya serikali ni kuona kiwanja kinakamilia mapema lakini kumejitokeza changamoto za kiufundi.

Alisema pamoja na bembea zote 12 kukamilika, baadhi ya maeneo yanaendelea kufanyiwa matengenezo, ambayo yatachukua zaidi ya miezi miwili kukamilika kwake.

Mzee alisema hata kama kiwanja hicho kitafunguliwa kwa muda kwa ajili ya sikukuu inayoanza mwanzoni mwa wiki ijayo, kutakuwa na wasiwasi wa usalama, kwani hata milango mikuu haijawekwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) inayowekeza katika mradi huo, Khamis Filfil Thani, alisema matumaini yake kuwa ifikapo Sikukuu ya Idd El Hajj, mwaka huu, kiwanja hicho kitakuwa tayari kutumika.


Hali hiyo pia iko katika kiwanja kama hicho kilichoko Tibirinzi, Chake Chake, Pemba, ambako kazi ya matengenezo yaliyotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu, yatachukua wiki mbili kutoka sasa.

Serikali ililazimika kuvifanyia matengenezo viwanja hivyo kutokana na uchakavu wa bembea, kwani zilikuwa zinahatarisha usalama wa watoto.

 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. Naipongeza smz kwa uamuzi huo kwa sababu mara hii watu walikamia sana kwenda na kungekuwa na watu wwngi mno wasiwasi wangu watoto wangekanyagana na mapakatokea maafa

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.