Habari za Punde

Bunge la kahawa latoa ujumbe

Na Salim Said Salim
 
BUNGE Maalum la Katiba linaoendelea Dodoma kwa mwendo wa kiguru cheche (kuchechema) sasa limegeuzwa na watu wengi wa Zanzibar kuwa mada kubwa ya kufanyiwa kila aina ya mzaha na dhihaka.
 
Hii inatokana na wananchi wengi kuhisi kinachoendelea Dodoma hivi sasa sio kutafuta katiba itayojenga mazingira ya kuwa na utawala bora na wa kidemokrasia, haki na sheria bali wajumbe kuikausha Hazina ili wajaze pochi zao wajijengee maisha bora.
 
Katika baraza za kahawa na vijiwe yanasikika mengi kuonyesha kinachofanyika katika kikao hicho sio kujadili rasimu ya katiba iliyotokana na maoni ya wananchi, bali kwa wajumbe wengi kufanya usanii wa mashindano ya nani anayefaa kupewa medali ya dhahabu na tunzo nyengine kwa kushinda wenzake kwa udanganyifu.
 
Kwa mfano, katika baraza moja nilimisikia kijana mmoja aliyejigeuza Mwenyekiti (Samuel Sitta), akiuliza nani ameizidi CCM kwa kudanganya watu kuwa wananchi waliotoa maoni yao kwa Tume ya Jaji Warioba walitaka mjadala wa rasimu ujikite na kinyume walivyotaka wao?
 
Hapo tena mtu mwengine aliyejifanya kuwa ni mjumbe wa kundi la watu 201, walioteuliwa na Rais kutoka makundi na taasisi mbali mbali alieleza kuwa ameagizwa na kundi analoliwakilisha kwa mjadala wa kutafuta katiba mpya kama inavyotakiwa na CCM uendelee.
 
Mwenyekiti akamuuliza; “Ulipoondoka Dodoma baada ya kumalizika ngwe ya kwanza ya mjadala uliwahi kuwasiliana na watu unaowawakilisha?”
 
Jamaa akajibu: “Naam Mheshimiwa Mwenyekiti. Nilifanya vikao usiku na mchana, wengine niliwatembelea majumbani kwao kutaka maoni yao, wengine niliwapigia simu na wengine niliwasiliana nao kwa barua pepe. Wote walisema tuendelee na UKAWA wafunikwe kawa”.
 
Hapo jamaa waliokuwa wanasikiliza wakapiga mabao waliokalia na wengine ukuta kuonyesha wanaunga mkono.
 
Mzee mmoja, naye akamuomba Mwenyekiti ruhusa ya kuchangia. Alipopewa nafasi kwanza alimshukuru Mwenyekiti kwa uzalendo wake kama unaoonyeshwa na CCM, hekima na busara ya aina yake.
 
Baada ya hapo akasema watu anaowawakilisha wametaka apendekeze posho iongezwe kwa fedha zilizotengwa kulipwa wajumbe waliosusia kikao na ambazo sasa hazitumiki.
 
Ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu wajumbe waliopo katika huo mkutano walikuwa wanalazimika kufanya kazi ya zaida na kwa hivyo ni haki yao kuongezwa posho.
 
Wajumbe wenzake hapo barazani walishangilia na kuunga mkono mmoja baada ya mwengine kwa vile baadhi yao walisema wameshanunua viwanja na wengine wanakarabati nyumba zao.
 
Mmoja alisema ameagiza basi kutoka Dubai na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekataa kumpunguzia kodi na kwa hivyo akiongezwa posho ataweza kulikomboa gari lake.
 
“Mimi ninayo harusi ya kijana wangu mwezi ujao na kwa hivyo ninahitaji fedha za ziada ili harusi ya mwaangu ifane na Mhesimiwa Mwenyekiti ninakuhakikishia wewe na wajumbe wako wote nitawaalika,”alidokeza mjumbe mwengine.
 
Mtu mwengine alipopewa nafasi ya kuchangia alisema utafiti alioufanya umeonyesha hata wagonjwa wanaokosa dawa katika hospitali za serikali kutokana na ukosefu wa fedha wamemtuma aliarifu Bunge Maalum kuwa katiba mpya ni muhimu kwao kuliko hizo dawa.
 
“Mimi pia nimeambiwa na wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati kuwa katiba inayotakiwa na CCM kwanza na madawati baadaye na hata yakikosekana potelea mbali”.
 
Mjumbe huyo wa baraza la kahawa (sio Baraza la Katiba) alisema ametumwa na anaowawakilisha kuilauni kauli ya Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kama kikao hicho kina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na Visiwani kupitisha rasimu ya katiba mpya.
 
“Wananchi wanasema huyu mtu sio mwenzetu, ametumwa. Nimeelezwa sio tu lazima pawepo theluthi mbili na hata ikipatikana chini kidogo tu ya theluthi moja inatosha. Tumeamua kuwatesa…mapambano yanaendelea”, aliongeza na kushangiliwa.
 
Baada ya hapo, Mwenyekiti alisema anawapa pole wajumbe kwa kuwa na kazi kubwa zaidi kuliko hapo awali kwa vile wajumbe wanaojiita UKAWA walioamua kuisaliti nchi wamesusia.
 
Lakini kwa vile mcheza kwao hutunzwa atapeleka kwa wanaohusika ombi la wajumbe kuongezwa posho kwa vile fedha ziliokuwa zimetengwa kulipwa kwa waliosusia kikao zipo na hazijaguswa.
 
Vifijo, nderemo na makofi yakatanda barazani huku jamaa mmoja akiwa amenyanyua mkoba wake aliokuwa anakwenda kununulia dagaa sokoni akisema:” Wache wao wajaze dagaa mikoba yao…sisi tujaze noti. Kidumu Chama Cha Mapinduzi”.
 
 Niliondoka katika ile baraza nikiwa nimepata ujumbe mzito, nao ni namna wananchi walivyokasirishwa na matumzii makubwa ya fedha kwa mchakato wa katiba ambao umeonyesha kila dalili ya kutokuwa na mafanikio.
 
Kama itapiitishwa rasimu hiyo mpya inayotakiwa na CCM na ile ya Jaji Warioba kuwekwa kando, sijuwi tutaona usanii gani miongoni mwa wananchi kuelezea kutoridhika kwao na maoni yao kupuuzwa.
 
Wapo wanaosema sikio la kufa halisikii dawa, lakini kwa baadhi ya watu wanaamini kama hukusikia unayoambiwa duniani leo utayasikia kesho kabla ya kufa.
 
Watu wa aina hii ni wale wanaolitakiwa na wahenga kuelewa kuwa majuto ni mjukuu na sijui ni mjukuu wa aina gani atakuja kujutiwa kwa huu usanii tunaouona hivi saa.
 
Tusubiri tutaona kinachotokea huko mbele. Kwa nini tuandikie mate na wino upo?
 
Lakini ni vyema kukumbushana kuwa sio hekima na wala sio busara kudharau kauli ya Naibu Waziri wa Feha amabye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) licha ya kuambiwa hayo ni maoni yake na sio ya chama chake.
 
Vile vile sio jambo la busara kufumbia masikio nasaha ziliotolewa na watu mbali mbali, wakiwemo vionngozi wa dini na taasisi za kiraia na taaluma za kutaka Bunge la Katiba livunjwe na kuokoa mabilioni ya shilingi yasitumike ovyo.
 
Wakati baadhi yetu na familia zetu tunatibiwa nje ya nchi, mamilioni ya Watazania wanatetegemea hizo hospitali zetu ambazo hazina dawa kutokana na ukosefu wa fedha.
 
Vilevile tuwaonee imani watoto wetu wanaosoma wakiwa wamekaa chini na kukosa vitabu.
Sio vibaya mtu kupenda pochi yake, lakini aitunishe kwa kujituma kwa kazi halali na sio kuchota fedha za Hazina kwa kazi ambayo waanchi wanaovuja jasho usiku na mchana kuichangia hio hazina hawaioni kufanyika kwa uadilifu na ufanisi wanaoutarajia.
 
Wakati nilipoondoka katika lile baraza ya kahawa, niligundua vikombe vya wateja wengi viliuwa vikavu. Si ajabu kila mmoja ambaye mfuko wake ulikuwa umetoboka alikuwa anasubiri mwenzake amnunulie kikombe cha pili na ikiwezekana na kashata.
 
Lakini kwa waheshimiwa waliopo Dodoma kunuliana chakula na hata vinywaji kutokana na poshi zao kunona si shida.
 
Ama kweli hawakukosea wahenga waliposema aliyeshiba hamjui mwenye njaa, hata akiwa aliwahi kufunga saumu na kukaa muda mrefu bila ya kula chakula wala kunywa maji.
 
Lakini tukumbuke kwamba hao hao wahenga walisema..Mwenda tezi na omo hurejea ngamani. Ipo siku watarudi kwa wananchi wenye njaa na shida kemkemu, lakini sijui watawaambia nini.
 
Chanzo : Tanzania Daima

2 comments:

  1. Makala hii nzuri sana na ina ujumbe mzito.Itapendeza pia kuwekwa kwenye ukumbi wa mzalendo.net.Shukran sheikh Said.

    ReplyDelete
  2. Tafadhali namuomba msomaji mwenzangu aiweke makala hii kwenye mzalendo.net.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.