Na Kija Elias, Moshi
KATIKA kukabiliana na matukio
ya uharibifu wa mazingira mkoani Kilimanjaro,
Shirika lisilo la kiserikali
linalojishughulisha na utunzaji na uhifadhi wa mazingira (TEACA), limekabidhi
mizinga 50 yenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa mtandao wa hifadhi ya msitu
wa nusu maili Kilimanjaro (KIHACONE).
Akikabidhi mizinga hiyo,
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Adoncome Mcharo, alisema uhamasishaji wa ufugaji wa
nyuki utawezesha kuondoa uvunaji ovyo wa misitu kwenye maeneo ya hifadhi na
kwamba wananchi hao watajikita katika
shughuli za ufugaji wa nyuki.
Alisema mpango huo wa kuwapatia
mizinga hiyo, utawawezesha wananchi kuwa na elimu ya utunzaji wa mazingira,
pamoja na kupata njia bora ya kisasa ya uvunaji
wa asali bila kutumia moto.
Kwa upande wake, Mbunge wa viti
Maalumu CCM, Dk. Bethy Machangu, alisema
ufugaji wa nyuki unaweza kubadili na kumkomboa mwananchi wa kipato cha chini endapo utapewa kipaumbele.
Alisema silaha kubwa ya
kupambana na umasikini ni kuwekeza kwa vijana na wanawake kuwa na ufanisi
katika ufugaji wa nyuki.
Awali akipokea mizinga hiyo,
Mwenyekiti wa mtandao wa vijiji 37, vinavyozunguka mlima Kilimanjaro, Boniface
Mbando, alisema mizinga hiyo itafungua njia kwa wananchi kuwekeza
zaidi katika
ufugaji wa nyuki.
Mtandao huo umekabidhi mizinga 50 kwa vijiji 10 vinavyozunguka
hifadhi ya mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati waliojiwekea.
No comments:
Post a Comment