STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
30.10.2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein amefanya ziara fupi ya kutembelea Kituo cha Damu Salama
kiliopo Sebleni mjini Unguja pamoja na kutembelea Maabara ya Uchunguzi wa
Maradhi katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na kupongeza hatua zilizofikiwa
huku akieleza azma ya serikali katika kuviimarisha vitengo hivyo.
Dk. Shein alianza
ziara yake katika Kituo cha Damu Salama kiliopo Sebleni mjini Unguja na
kujionea kazi zinazofanywa katika kituo hicho pamoja na kupata maelezo kutoka
kwa wataalamu mbali mbali wa kituoni hapo wakiongozwa na Dk. Mwanakheir Ahmed
Mahmoud.
Mara baada ya
kutembelea vitengo vilivyomo ndani ya kituo hicho, Dk. Shein alizungumza na
wafanyakazi wa kituo hicho na kuwaeleza jinsi alivyofarajika na huduma zinazoendeshwa
kituoni hapo ambazo zina umuhimu mkubwa katika
maisha ya jamii.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuchangia damu na kusisitiza kuwa bila ya
kuchangia damu hakuna damu itakayopatikana, hivyo suala la kuchangia damu ili
kuweza kukiimarisha kituo hicho ni jambo la msingi na linaumuhimu wake mkubwa
ndani ya jamii.
Akizungumzia
kuhusu suala zima la uhamasishaji juu ya kuchangia damu kwa lengo la
kukiimarisha kituo hicho kama kinavyofahamika pia kuwa ni benki ya damu ni
jambo muwafaka kwani ni jambo la nchi nzima kama ilivyo kwa uhamasishaji juu ya
maambukizi ya UKIMWI.
Alisisitiza kuwa
jambo la muhimu ni kuwekwa maandalizi na
mikakati endelevu ili kufikia lengo lililokusudiwa huku akisisitiza
kuwahaheshimu sambamba na kuwapongeza wale wote wanaochangia damu kwani
wamekuwa wakifanya jambo kubwa katika uhai wa mwanaadamu.
Aidha, Dk. Shein
aliueleza uongozi pamoja na wafanyakazi wa Kituo hicho kuwa ataendelea
kushirikiana na uongozi wa Wizara ya Afya ili kukiimarisha kituo hicho ili
kiweze kupata mafanikio zaidi.
Nao, wafanyakazi
wa Kituo hicho walimueleza Dk. Shein mafanikio yaliopatikana sambamba na
changamoto zilizopo huku wakisisitiza na
kuwataka wananchi pamoja na viongozi wa ngazi zote kuwahamasisha wananchi juu
ya umuhimu wa kuchangia damu.
Pamoja na hayo, wafanyakazi
hao walimueleza Dk. Shein umuhimu wa kituo hicho kuunganishwa na maabara ya
hospitali Kuu ya Mnazi mmoja pamoja na hospitali kuu za Chake, Wete na Mkoani Pemba
ili kurahisisha utoaji huduma wa damu kwa wagonjwa.
Wakati huo huo, Dk. Shein alitembelea Maabara ya Uchunguzi wa
Maradhi iliopo katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na kujionea huduma mbali
mbali za maabara zinazofanywa katika
Maabara hiyo pamoja na kupata maelezo ya kina juu ya kazi hizo
kitaalamu.
Nao, wataalamu wa
kituo hicho chini ya Mkuu wao Dk. Msafiri Marijani walimueleza Dk.
Shein kuwa hivi sasa kituo hicho kimeweza kupiga hatua kubwa na kuweza kupata
mashirikiano makubwa na hospitali ziliopo nje ya nchi hatua ambayo imepelekea
hadi madaktari wanafunzi kutoka nje kama vile Hospitali ya Haukland ya Norway
kufanya uchunguzi kupitia maabara hiyo.
Mara baada ya
ziara yake hiyo, Dk. Shein akizungumza na wafanyakazi wa Maabara hiyo ambayo yeye mwenyewe ni muasisi
aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa amefarajika na hatua iliyofikiwa hivi sasa
katika Maabara ikilinganishwa na pale ilipoanzishwa.
“Nilipoondoka maabara
hii haikuwa hivi, mabadiliko makubwa
yamefanyika...hongereni sana”,alisema Dk. Shein.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisema kuwa huduma za hospitali haziendi bila ya kuwepo Maabara
kwani Maabara ndiko kunakofanyiwa uchunguzi wa kutambulikana maradhi ya
mgonjwa.
Dk. Shein alisema
kuwa hatua hiyo ni kubwa na itambuliwe kuwa hizo ni juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wafadhili mbali mbali waliyoiunga mkono
Serikali katika kuiimarisha Maabara hiyo.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kuwa Sera ya Afya bado ni kuwa matibabu bure na kueleza haja kwa
wananchi kuelimishwa namna ya kuchangia huduma hizo za afya hasa ikizingatiwa
ongezeko kubwa la idadi ya watu hapa Zanzibar hivi sasa ikilinganishwa na mara baada ya
Mapinduzi ya mwaka 1964 wakati ilipotangaziwa huduma za afya.
Nao wataalamu wa
kitengo hicho walimueleza Dk. Shein changamoto zilizopo huku uongozi wa Wizara hiyo ukitoa pongezi kwa Dk. Shein kufuatia
ziara yake hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment