HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS
WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA
SABA WA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR.
TAREHE 31 OKTOBA, 2014
UTANGULIZI:
Mheshimiwa
Spika, napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutukutanisha hapa
tukiwa katika hali ya uzima na afya njema na kufanikiwa vizuri kushiriki katika
Mkutano huu wa Kumi na Saba wa Baraza la Wawakilishi.
Aidha,
napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Said Hassan Said kwa
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kuteuliwa kwa Mhe. Said kunaonyesha imani
kubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo juu yake, hasa kutokana na uzoefu wake na
uwezo wake mkubwa wa kuchapa kazi.
Tunamtakia kila la kheri na mafanikio mema katika kazi yake hiyo
mpya. Tunakuhakikishia ushirikiano wetu
kila wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa
heshima kubwa, niruhusu nitoe shukurani zangu za dhati kwako wewe binafsi,
Naibu Spika, Wenyeviti na wasaidizi wako wote kwa kuendelea kuliendesha Baraza
hili Tukufu kwa busara na umakini mkubwa. Pia nawashukuru Waheshimiwa Wenyeviti
na Wajumbe wa Kamati mbali mbali wa Baraza hili kwa busara zao katika
kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, pongezi maalum
nazitoa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu kwa hekima, busara na
uadilifu mkubwa. Aidha, nachukua fursa hii kumpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendelea kumsaidia vyema Mheshimiwa
Rais katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la
Wawakilishi, Mawaziri, Naibu Mawaziri kwa umahiri wao mkubwa katika kuchangia
mijadala mbali mbali ndani ya Baraza hili. Aidha, nawashukuru Makatibu Wakuu,
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, pia
navipongeza vyombo vya habari vya hapa Zanzibar,
hususan Shirika la Habari la Zanzibar (ZBC)
kwa kuwapasha habari mbali mbali
wananchi wetu kwa kupitia redio, TV na magazeti. Hali ambayo ilipelekea urahisi
kwa wananchi kufuatilia kwa makini matukio yote yaliyojiri Barazani. Vile vile,
nawapongeza wakalimani wetu wa lugha ya alama kwa kazi nzuri walioifanya ya
kutafsiri mawasilisho na mijadala katika kipindi chote cha kikao hikina
kuwawezesha wananchi wenzetu wenye ulemavu wa kusikia kufuatilia shughuli za
Baraza kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Spika, mwisho
navipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama pamoja na Idara Maalum za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wao mkubwa katika kudumisha
amani, usalama na utulivu uliopo hapa nchini.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI
Mheshimiwa Spika, tunatambua
kwamba nchi yetu inaendelea na mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo
kwa sasa katiba inayopendekezwa tayari imekabidhiwa kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Makabidhiano hayo
yalifanyika katika uwanja wa Jamhuri huko Dodoma, tarehe 8 Oktoba, 2014.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na tukio hili kubwa la kihistoria katika nchi yetu, hatuna budi kuwapongeza
viongozi wetu hawa kwa kuanzisha na kufanikisha kupata Katiba Inayopendekezwa
kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Nawanasihi wananchi wote kupata muda wa kuisoma kwa kina katiba hiyo
inayopendekezwa ili kuielewa na hatimaye kutumia haki yao ya kidemokrasia
kushiriki katika zoezi la upigaji kura ya maoni wakati muda utakapofika.
Mheshimiwa Spika, Kwa
niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nachukua fursa hii kuwapongeza kwa
dhati kabisa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mheshimiwa Samuel
John Sitta na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan kwa namna walivyoliendesha Bunge hilo Maalum kwa ufanisi na
mafanikio makubwa. Pia, nawapongeza wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba
walioshiriki katika kuandaa Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu
inajivunia hazina kubwa aliyotujaalia Mwenyezi Mungu ya amani na utulivu
tulionao ambao ni nyenzo kubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Hivyo,
hatuna budi sote kwa pamoja kuilinda na kuidumisha hazina hiyo kwani amani
ikivurugika hakuna hata mmoja miongoni mwetu atakaebaki salama. Serikali
itaendelea kwa juhudi zake zote kusimamia amani na utulivu tulionao na ni vyema
viongozi na wananchi tukatoa ushirikiano katika kufanikisha azma hii.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo bado inaendelea
kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa
moja katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za
wananchi walio wengi vijijini na mijini. Takriban zaidi ya asilimia 70 ya
wananchi wanategemea sekta hii kwa kuendeleza maisha yao. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sekta hii ilichangia wastani wa asilimia 30
ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa
Spika, kwa Msimu wa Kilimo cha Mpunga cha Masika 2013/2014, jumla ya ekari 30,444 (Unguja 12,548 na Pemba
17,896) zililimwa katika maeneo ya juu, sawa na
asilimia 87 na ekari 1,736
zililimwa katika maeneo ya umwagiliaji maji (Unguja ekari 1,143.61 na Pemba
ekari 592.8) sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa.
Mheshimiwa Spika, katika msimu huo, jumla ya tani
21,895 za mpunga zimevunwa katika maeneo ya juu (tani 14,354 Pemba na Tani
7,541 Unguja) na tani 2,070 za mpunga katika maeneo ya umwagiliaji maji (Unguja
tani 1,302 na Pemba tani 768) zilivunwa.
Kupungua kwa uzalishaji wa mpunga
katika msimu ulioainishwa umetokana na uvamizi wa viwavi jeshi hasa katika mkoa
wa Kaskazini Unguja na kupungua kwa maeneo ya ukulima wa mpunga ekari 3,400
(Upenja ekari 700 na Mahonda ekari 2,700) kwa maeneo ambayo yanamilikiwa na
Kiwanda cha Sukari cha Mahonda ambapo tayari mashamba hayo yamepandwa miwa kwa
ajili ya uzalishaji wa Sukari.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuliendeleza eneo la hekta 2,410 Unguja na Pemba kwa
ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji maji kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini na Serikali ya Marekani.
Utekelezaji wa mradi huu mkubwa utasaidia sana katika kuendeleza kilimo cha mpunga kwa uhakika na kuongeza
uzalishaji na hivyo kuwaongezea kipato wakulima wetu na kuchangia katika
kupunguza umasikini.
Mheshimiwa Spika, matayarisho ya uzalishaji wa zao la mpunga kwa kipindi
cha 2014/2015 yamefikia hatua ifuatayo:
·
Serikali imeweza
kununua matrekta 20 kutoka SUMA JKT pamoja na kuyafanyia matengenezo matrekta
24 makongwe ambayo tayari yameanza kazi ya ukulima katika kwa msimu wa kilimo
cha mpunga 2014/2015. Lengo ni kuweza kulima eneo la ukubwa wa ekari 32,100 (Unguja
12,901 na Pemba 19,199).
·
Kwa upande wa pembejeo
Serikali imefanya zabuni ya ununuzi wa mbolea tani 750 (Urea tani 600 na TSP
tani 150), dawa ya kuulia magugu lita 15,000 pamoja na mbegu ya mpunga tani
150.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali zetu,
Serikali imekamilisha mapitio ya Sera na Sheria ya Misitu pamoja na Mpango wa
muda mrefu wa matumizi ya maliasili. Aidha, juhudi za kuendeleza zao la karafuu
nchini zinaendelea kwa matayarisho ya uzalishaji wa miche ya mikarafuu 650,000
katika vitalu vya Serikali na watu binafsi na hatimae kuisambaza kwa wakulima
katika msimu ujao wa masika 2014/2015.
Mheshimiwa Spika, katika kuiendeleza Sekta ya Mifugo, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa
wafugaji kuhusu ufugaji bora. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2014,
jumla ya wafugaji 5,432 wamepatiwa elimu hiyo kupitia vikundi vya wafugaji,
mashamba darasa ya mifugo na mfugaji mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka tani 8,118,519 hadi tani 8,397,540 na uzalishaji wa mayai umeongezeka kutoka
mayai
40,924,594 hadi mayai 49,900,389
kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2014. Aidha, huduma za upandishaji
ng’ombe kwa sindano zinaendelea kuimarika na upatikanaji wa mbegu za kupandishia
ng’ombe si tatizo tena kwa wafugaji.
Mheshimiwa Spika, kuhusu migogoro ya ardhi bado Serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi wa
kudumu tatizo hilo. Hali halisi inaonesha kwamba migogoro mingi ya ardhi
inasababishwa na wananchi wenyewe. Kesi nyingi zilizopo zinatokana na migogoro
ya mipaka, uvamizi wa ardhi na mauziano yasiyo rasmi. Baadhi ya migogoro
inasababishwa na muingiliano wa majukumu miongoni mwa taasisi na mamlaka
zinazosimamia masuala ya ardhi katika utoaji wa vibali usiozingatia masharti na
miongozo ya matumizi ya ardhi inayotolewa katika ngazi mbali mbali zikiwemo
Halmashauri za Wilaya, Madiwani pamoja na Masheha. Aidha, kuna baadhi ya
migogoro inasababishwa na watendaji wasio waaminifu ambao humilikisha na hata
kushiriki katika mauziano ya ardhi yasiyo rasmi hali ambayo inapelekea wananchi
kuuziana zaidi ya mara moja.
Mheshimiwa Spika, idadi ya kesi zinazowasilishwa katika Mahakama ya Ardhi zimekuwa
zikiongezeka siku hadi siku na hili linatokana na hali halisi ya ufinyu
wa ardhi katika visiwa hivi vya Zanzibar ukilinganisha na ongezeko kubwa la
watu ambalo linaenda sambamba na ongezeko la harakati za kiuchumi na kijamii.
Pamoja na kwamba idadi ya kesi zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka lakini
kasi ya usikilizaji na utolewaji wa maamuzi nayo kwa kiasi kikubwa
imeongezeka. Kwa mfano mwaka wa fedha
2011/12 jumla ya kesi 188 zilifunguliwa kwa Unguja na Pemba na kwa mwaka
2013/14 kesi zilizofunguliwa ni 210.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kukabiliana
na hali hii kwa kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi inapungua au kumalizika
kabisa. Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa Serikali inajipanga katika kutekeleza
mikakati ifuatayo:
- Kutoa elimu kwa wananchi kufuata taratibu na
miongozo ya ardhi hasa katika umiliki na ujenzi wa nyumba.
- Kukamilisha maandalizi ya Sera ya Ardhi ambayo hivi
sasa ipo katika hatua za mwisho.
- Kuimarisha zoezi la utambuzi na Usajili wa Ardhi ili
kuepusha migogoro ya ardhi.
- Kuandaa Mpango Mkuu wa Taifa wa matumizi ya ardhi
ambao utawezesha wananchi kutumia ardhi kwa kuzingatia miongozo imara.
- Kuzipitia tena na kuzifanyia marekebisho Sheria za
Ardhi ikiwemo Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 1959.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeongeza idadi ya Mahakimu wa Mahakama ya Ardhi kutoka
watatu hadi watano na kuongeza idadi ya wakadiriaji (assessors) kutoka 11 hadi
26. Hali hiyo imepelekea kuimarika kwa Mahakama hiyo kiutendaji. Vile vile,
juhudi zinazoendelea hivi sasa za kupatikana majengo kwa ajili ya Mahakama za
Ardhi katika ngazi za Mikoa zitaimarisha zaidi utendaji wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, dira ya Serikali kuhusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi ni kuibadililisha Sekta
ya Mifugo na Uvuvi kutoka katika mfumo wa uzalishaji wa kujikimu hadi kufikia
kilimo cha biashara ifikapo mwaka 2020.
Azma hiyo, itafikiwa kwa mkakati wa kuimarisha hali ya uchumi na kijamii
kwa jamii za wafugaji na wavuvi kwa kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji,
kutoa huduma za ugani, kuongeza thamani na upatikanaji wa taarifa za masoko ili
kuongeza uzalishaji na kipato.
Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini inaendelea kuimarika siku hadi
siku kutokana na kukua kwa soko la ndani, linachangiwa na ongezeko kubwa la
mahitaji ya soko la utalii nchini ambalo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa za mifugo
na samaki, sambamba na ongezeko la watu mijini.
Hali hii imesababisha wananchi kuendelea kujiajiri katika sekta hizi
hasa vijana kutokana na tija zake.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mnasaba huo, mwelekeo wa Serikali hivi sasa ni kutatua
changamoto muhimu zilizopo ili kuweza kutoa matokeo makubwa sasa (Big Results
Now). Hizo ni pamoja na hizi zifuatazo:
1.
Kuendeleza utafiti na
utoaji wa huduma za ugani kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi, ili wafugaji
wetu waweze kupata faida kubwa, jambo ambalo litawafanya wananchi wengine hasa
vijana kuendelea kujiajiri katika sekta ya ufugaji na uvuvi. Suala la utafiti ni kikwazo kwa sekta zetu
hizi, kuanzishwa kwa idara ambayo pia inasimamia suala la utafiti haitoshi,
bali kuwepo kwa taasisi zinazojitegemea kushughulikia utafiti kisekta pamoja na
kuweka mazingira mazuri kwa utafiti, Serikali tayari imo katika mpango wa
kufanikisha suala zima la vituo vya utafiti kwa kuanzia na sekta ya uvuvi na
Serikali ya China na KOICA.
2.
Kuongeza uwezo wa
kitaaluma kwa wafanyakazi na kuajiri wataalamu zaidi ili kuongeza ufanisi wa
utoaji huduma mbali mbali kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi ikiwemo huduma
za ugani, ujasiriamali katika shughuli za ufugaji na uvuvi. Aidha, Serikali imo katika kuandaa mpango wa
kuanzisha Chuo cha Uvuvi hapa Zanzibar.
3.
Kuongeza ajira kwa
vijana kupitia shughuli za uzalishaji mifugo na uvuvi; ingawaje kila siku sekta
hizi zimekuwa muajiri mkubwa wa vijana, lakini kwa makusudi Wizara itaendelea
kuwawekea mazingira mazuri ya kuweza kujiajiri na kufanya kazi zao kwa
faida. Kwa hivyo, Serikali imekuwa
ikiandaa programu tofauti zitakazowasaidia pamoja na kuwaunganisha na taasisi
na mashirika ili kupata misaada na mikopo isiyo na masharti magumu.
4.
Kuendelea kuhamasisha
wananchi kupandisha ng’ombe wa maziwa na nyama kwa kufuga kibiashara na
kuondokana na mazoea. Kwani hivi sasa ni
kiasi cha asilimia 5 tu ndio ng’ombe wa kisasa wanaozalisha maziwa, bado fursa
ipo kwa watu kubadilisha ng’ombe wa asili.
5.
Kuimarisha miundombinu
ya kuendeleza uzalishaji wa mifugo ikiwemo vituo vya uzalishaji na utabibu wa
mifugo (animal health and production centres) karantini na majosho.
6.
Kuimarisha shughuli za
mazao ya baharini kwa kujenga kituo cha uzalishaji vifaranga vya samaki hapo
Beit el Ras kwa mashirikiano na Shirika la FAO na KOICA.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendelea kuandaa mazingira mazuri ya kisera, sheria, kanuni
na miongozo mbali mbali ili kuifanya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika
kuendeleza sekta endelevu, ufugaji wa ng’ombe pamoja na uwekezaji wa viwanda
vya usarifu wa samaki na mifugo bila kuathiri mazingira yetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imo katika kuandaa Mkakati Maalum wa Kuendeleza Sekta ya
Uvuvi hapa Zanzibar, pamoja na Mkakati wa Kusimamia Utawala wa Baharini. Aidha, Wizara inakusudia kutoa taaluma kwa
wadau wote wa sekta ya uvuvi ikiwemo wavuvi pamoja na kushirikisha jamii katika
kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kufanya tathmini ya shughuli za uvuvi; na
pia kushirikiana na wanajamii na vyombo vya sheria kuendeleza doria katika
maeneo ya hifadhi na shughuli nyengine za baharini.
MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 17, Baraza lako Tukufu lilikamilisha mambo makuu
manne yafuatayo:
i. Kujibu maswali yaliyoulizwa na Waheshimiwa
Wajumbe.
ii. Uwasilishwaji wa miswada minne (4) ya Sheria ambayo ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi
yetu.
iii. Kiapo cha uaminifu kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
iv. Hoja ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuliomba Baraza la
Wawakilshi kutoa maazimio kuhusu uimarishaji wa huduma za afya zinazotolewa kwa
wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu Wajumbe waliuliza na kujibiwa maswali ya msingi na
maswali ya nyongeza. Jumla ya maswali ya msingi 48 na maswali ya nyongeza 100
yaliulizwa na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika. Nawapongeza
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliouliza maswali ya msingi
ambayo yalikuwa na lengo la kudadisi utekelezaji na ufanisi wa shughuli za
Serikali. Aidha, nawapongeza na
kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa majibu sahihi ambayo yamewejengea
uelewa Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na wananchi kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa mwanzo
uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Wauguzi na Wakunga
(uanzishwaji wa Baraza la Usajili wa Wauguzi na Wakunga) Nam. 9 ya mwaka 1986
na kuanzisha badala yake Sheria mpya ya Wauguzi na Wakunga na Mambo
Yanayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, Mswada huu una madhumuni ya
kukabiliana na hali halisi ya mabadiliko yaliyopo hivi sasa ulimwenguni katika
sekta ya Uuguzi na Ukunga ambapo Sheria Nam. 9 ya 1986 inaonekana kutokidhi
haja kwa matumizi ya wakati huu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimwa Wajumbe wa Baraza
lako Tukufu walipata fursa ya kuchangia Mswada huu kwa kina ambapo wengi wao
waliiomba Serikali kuwa makini katika kusimamia utekelezaji wake ili kuleta
ufanisi uliokusudiwa. Pia wameiomba Serikali kuyaangalia upya maslahi ya
wauguzi na wakunga ili kuwapa motisha katika kutekeleza majukumu yao. Serikali imekisikia kilio hicho.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili uliowasilishwa
ulikuwa ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Shirika la Nyumba la Zanzibar.
Madhumuni ya Mswada huo ni kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba la Zanzibar kwa
mujibu wa sheria ili kuweza kuziendeleza nyumba ziliopo nchini, kusimamia kodi,
kujenga nyumba mpya na kutoa huduma nyengine zinazohusiana na masuala ya
nyumba.
Mheshimiwa Spika, katika michango ya Waheshimiwa
Wajumbe wameiomba Serikali kuwa makini na kuangalia madhumni ya kuanzishwa
nyumba za maendeleo zilizopo nchini ambazo zimeanzishwa na Marehemu Sheikh
Abeid Amani Karume pamoja na dhamira ya uanzishwaji wa sheria hii. Aidha,
Waheshimiwa Wajumbe walionesha kuwepo kwa tatizo la umiliki na ukodishwaji wa
nyumba kwa wananchi ambao wanaishi katika nyumba hizo.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Tatu uliowasilishwa
ulikuwa unahusu kufuta Sheria ya Baraza la Manispaa Nam. 3 ya mwaka 1995 na
Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji Nam. 4 ya mwaka 1995 na kuanzishwa
upya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2014 kwa madhumuni ya
kuanzisha Serikali za Mitaa, uwezo wake, kazi na wajibu, muundo, mpangilio,
fedha na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mswada huo Wajumbe wameishauri Serikali kuwa na tahadhari kubwa na
kuangalia kwa makini suala la kijiografia juu ya mipaka ya Serikali za Mitaa.
Aidha, waliishauri Serikali kumfanya Naibu Meya kuwa mfanyakazi wa kudumu na
pia wameiomba Serikali kuboresha maslahi ya Madiwani kwa kuwapatia mishahara na
sio kuwapa posho tu.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa Nne uliowasilishwa
unahusu kufuta Sheria Nam. 1 ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1998 na kuanzisha
Sheria mpya ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 2014 na Mambo Mengine Yanayohusiana na
Hayo. Mswada huu unalenga kuweka mfumo wa Kiutawala wa Serikali Kuu kuanzia
ngazi ya Shehia hadi Mkoa kwa kuzingatia mageuzi ya Serikali za Mitaa na
kuondoa kasoro zilizojitokeza katika sheria ya sasa ya Tawala za Mikoa na
kuweka mtiririko ulio bora zaidi kwa mujibu wa mahitaji ya sasa. Aidha,
madhumuni ya mswada huu ni kupata Sheria itakayoonesha wajibu, muundo, kazi na
uwajibikaji kwa kila ngazi ya Serikali Kuu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na
Shehia na kukuza uhusiano baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imesikia na kuzipokea hoja za Waheshimiwa Wajumbe kuhusiana na
miswada yote minne iliyowasilishwa na itazizingatia na kuzifanyia kazi hoja
hizo kadri hali itakavyoruhusu.
HITIMISHO:
Mhesimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe
binafsi kwa umahiri wako na umakini mkubwa katika kuliendesha Baraza letu. Vile
vile, narudia kuwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi, kwa kazi zao nzuri katika kusimamia utendaji wa Serikali na kwa
michango yao yenye tija katika kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika
Serikali.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote waliosaidia kutoa ufafanuzi wa hoja
mbali mbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wajumbe. Pia nawashukuru waandishi wa
habari na wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi yao nzuri ya kuwapatia taarifa
wananchi kuhusu majadiliano ya Baraza katika mkutano huu wa kumi na saba.
Mheshimiwa Spika, naomba tena kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe kwamba Serikali yao chini
ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein itajitahidi kuhakikisha
kwamba inaimarisha utendaji na uwajibikaji katika Serikali na kuendelea
kudumisha amani na utulivu.
Mheshimiwa
Spika, baada
ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako
Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 21 Januari, 2015 saa 3.00 asubuhi panapo
majaaliwa.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment