Na Hassan Hamad, India.
Kiasi cha wagonjwa 65,000 wenye ulemavu wa aina tofauti wanapatiwa
visaidizi pamoja na matibabu kila mwaka nchini India, hatua ambayo huwawezesha
kuendelea na shughuli zao za kimaisha kama kawaida.
Meneja wa kituo kikuu cha viungo bandia vya binadamu katika mji wa
Jaipur jimbo la Rajasthan kaskazini mwa India, Om Prakash Sharma alieleza hayo
mbele ya waandishi wa habari kutoka baadhi ya nchi za Afrika, Asia na Latin
America waliofika kituoni hapo hivi karibuni kwa ziara maalum ya kimasomo.
Sharma alisema kituo hicho kijulikanacho kwa jina la “Bhagwan
Mahaveer Viklang Sahayata Samiti (BMVSS), ndio kituo kikubwa zaidi duniani
kinachojihusisha na utengenezaji na utoaji wa viungo bandia vya binadamu
vikiwemo miguu na mikono.
Anafahamisha kuwa mara mgonjwa anapofika kituoni hapo au tawi
lolote la kituo hicho miongoni mwa matawi 23 yaliyoko nchini India, hufanyiwa
vipimo na baada ya siku chache hupatiwa viungo anavyohitaji bila ya malipo,
ambavyo humuwezesha kuendelea na shughuli zake kama ilivyokuwa awali baada ya
muda mfupi.
“Mara baada ya mgonjwa kupatiwa viungo anavyostahiki hufanyishwa
mazoezi na baada ya siku chache tu anaweza kufanya shughuli zake za kimaisha
ikiwa ni pamoja na kushiriki katika masuala ya kiuchumi pamoja na michezo”,
alieleza Sharma na kuongeza;
“Viungo vinavyotengenezwa na kituo hiki ni imara na vyenye viwango
vya hali ya juu, na vinatengezwa kisayansi. Vinaweza kudumu hadi miaka sita au
kumi bila ya kufanyiwa matengenezo ya aina yoyote”.
Anafahamisha kuwa mara nyingi wagonjwa wanaofika kwenye kituo
hicho ambacho pia hujulikana kwa jina la “Jaipur Foot Knee/Limb” pamoja na
matawi yake, ni wale waliopata ulemavu wa viungo kutokana na sababu mbali mbali
zikiwemo za kimaumbile, ajali za barabarani, matukio ya vita na maradhi mbali
mbali yakiwemo polio.
Sharma anaeleza kuwa kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1975 kwa
lengo la kuwasaidia wagonjwa wanaopoteza viungo kutokana na sababu mbali mbali
hasa watu wa daraja la chini, kilianza kwa kutengeneza na kutoa miguu na mikono
bandia 59, ambapo hadi kufikia katikati ya mwaka huu tayari kimewahudumia watu
wapatao milioni moja na laki nne (1.4 million), ambao ni wastani wa watu 50,000
hadi 65,000 kwa mwaka.
Anaongeza kuwa mbali na wagonjwa kupatiwa viungo hivyo, baadhi yao
wamekuwa wakipatiwa visaidizi vyengine vikiwemo vigari na baiskeli
ambavyo huwasaidia kuendeleza harakati zao za kimaisha ikiwa ni pamoja na
kufanya biashara mbali mbali. Pia baadhi yao wamekuwa wakipatiwa misaada ya
fedha na vitendelea kazi kwa masharti nafuu.
Katika jitihada za kuwasaidia wananchi hasa wa kiwango cha chini,
Sharma amesema baadhi ya watendaji hulazimika kusafiri katika maeneo tofauti
yaliyokumbwa na majanga yakiwemo vita ndani na nje ya India, ambako hufungua
kambi katika maeneo hayo na kutoa huduma za kimatibabu kwa waathirika.
ANAsema hadi kufikia mwaka 2014, tayari wametoa huduma katika
kambi zipatazo 26 katika nchi mbali mbali zikiwemo Afghanistan, Philippines,
Nigeria, Sudan, Rwanda na Kenya.
Mohamad Sehebay kutoka mji wa Uttar Pradesh aliyefika kituoni hapo
kwa ajili ya marekebisho ya mguu wake wa bandia, aliwaambia waandishi hao
kuwa amekuwa akiutumia mguu huo kwa kipindi cha miaka sita mfululizo bila ya
matatizo yoyote.
“Nilipata ajali ya barabarani mwaka 2008 na baada ya kupata
taarifa za kituo hiki nilikuja hapa, na nashkuru nilipatiwa mguu bandia na
unanisaidia sana. Tayari nilikuwa nimeshakata tamaa na maisha lakini namshukuru
Mwenyezi Mungu kwa msaada wa kituo hiki nimeendelea kuishi kwa matumaini
makubwa”, alisema Mohamad huku akionesha uso wa bashasha.
Wazo la kuanzishwa kituo hicho kinachofanya kazi kama taasisi
binafsi (NGO), lilikuja baada ya bwana
Mehta ambaye ni mwanzilishi wake kupata ajali mbaya ya barabarani,
na kuungwa mkono na madaktari wawili waliompatia matibabu, wote kutoka
hospitali ya Mahatma Gandhi, Jodhpur nchini India.

No comments:
Post a Comment