Habari za Punde

Tanzania Yaihakikishia Dunia Hali ya Utalii Iko Salama

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Na Mwandishi Wetu, Riyadh

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kilichoanza leo Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia, ameihakikishia dunia kuwa hali ya utalii na amani viko imara nchini Tanzania kufuatia machafuko yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi katika baadhi ya maeneo.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo wakati akichangia Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka ya Taasisi hiyo ambapo pia Tanzania ilinufaika na programu mbalimbali ikiwemo kuandaa Mkutano wa Dunia Kanda ya Afrika wa Utalii wa Vyakula uliofanyika Arusha April mwaka huu na kufadhiliwa baadhi ya programu za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya Safu za Milima ya Usambara.

“Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza hili baada ya kumpongeza Katibu Mkuu na  Sekretarieti ya UN Tourism kwa utekelezaji ambao Tanzania pia imenufaika, naomba kutumia fursa hii kutoa taarifa kuwa Tanzania ni salama baada ya kadhia iliyojitokeza wakati wa uchaguzi.

“Serikali imefanya jitihada na kurejesha nchi yetu katika hali ya utulivu na hivyo kuendelea kuwa salama kwa watalii na vivutio vyetu vyote mnavyovijua viko salama. Nawakaribisha wajumbe wa Mkutano huu na wadau wengine wa utalii kuja na kuendelea  kutembelea nchi hii ambayo ni kivutio bora Afrika kwa utalii wa safari,” alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, mbali ya Tanzania kuwa miongoni mwa  nchi 32 pekee kati ya wanachama wa Umoja huo wanaofikia 160 kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji (Executive Committe), leo pia Baraza Kuu hilo limeipitisha Tanzania kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuhakiki wanachama (UN Tourism Credentials Committe).

Mkutano huo unaendelea jijini hapa na pamoja na mambo mengine utajadili kuhusu matumizi ya akili mnemba katika kutangaza utalii na pia jioni hii umemthibitisha Sheikha Nasser Al Nowais kutoka UAE kuwa Katibu Mtendaji mpya wa taasisi hiyo muhimu kwa sekta ya utalii duniani.

Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) anayemaliza muda wake, Zurab Pololikashvili akizungumza katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Baadhi ya wajumbe kutoka nchi mbalimbali wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) anayemaliza muda wake Zurab Pololikashvili (wa tano kutoka kushoto mstari wa mbele) katika picha ya pamoja na wajumbe nchi wanachama wa Shirika la Utalii Duniani mara baada ya kufungua Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.