Na.Mwandishi Wizara ya Afya.
Serikali ya Awamu ya Nane kupitia Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Ubalozi Mdogo wa China hapa Zanzibar, imeandaa programu maalumu ya muda mrefu na muda mfupi kwa wataalamu wa Afya kutoka Zanzibar kujifunza mbinu na teknolojia za kisasa za utumiaji wa vifaa katika matibabu ya maradhi ya saratani ya shingo ya kizazi.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar,Dk.Mngereza Mzee Miraji amewataka wataalamu wanaopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanatumia vyema ujuzi watakaoupata ili kusaidia jitihada za Serikali katika kupunguza na hatimaye kuondokana kabisa na maradhi ya saratani visiwani Zanzibar.
Amesema mafunzo hayo yanayotolewa yatakuwa ya muda mrefu na muda mfupi huku, yakilenga kuongeza uelewa na umahiri wa wataalamu katika utambuzi na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Balozi Mdogo wa China Zanzibar, Li Qianghua, amesema Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya afya, hususani katika kuboresha huduma za uchunguzi, kinga na matibabu ya saratani, ikiwa ni sehemu ya kudumisha urafiki wa kihistoria kati ya China na Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na Elimu ya Afya kutoka
Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Salim Slim pamoja
na mratibu wa kitengo cha maradhi yasioambukizika Zanzibar Zuhura Saleh Amour wamesema hadi sasa asilimia 97 ya walengwa
tayari wamepatiwa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, jambo
linaloonesha mafanikio makubwa ya juhudi za Serikali katika kuimarisha afya ya
wanawake nchini.
Jumla ya wataalamu 30 wa afya kutoka Zanzibar watapatiwa mafunzo hayo kupitia mpango unaoratibiwa na Wizara ya Biashara ya China kwa kushirikiana na Taasisi inayoshughulikia mafunzo kwa wataalamu wa biashara za kimataifa. Hatua hii inaashiria dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa DK.Hussein Ali Mwinyi katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma bora za afya, hasa katika mapambano dhidi ya maradhi ya saratani.
Mwisho

No comments:
Post a Comment