Habari za Punde

Ban KI Moon : Hakuna nchi inayoweza kusimama peke yake

Mhe Spika  Anne Makinda ( Mb) akibadilishana mawazo na  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dr. Theo-Ben Gurirab
Pamoja jukumu kubwa la  mkutano wa  kamati ya maandalizi, Mhe. Spika alipata nafasi ya  kufika  katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambapo alipokelewa na Naibu  Mwakilishi wa Kudumu  Balozi, Ramadhani Mwinyi. Hapa Mhe. Spika  akisaini kitabu cha wageni na pembeni yake ni Balozi Ramadhan Mwinyi na  aliyeketi ni Bw. Eliufoo Ukhotya kutoka Ofisi ya Spika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, akizungumza na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Dunia wa Maspika wa Mabunge, wajumbe wa kamati hiyo akiwamo Mhe, Spika Anne Makinda ( Mb) walikutana kwa siku mbili  hapa Umoja wa Mataifa
Hapa   ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Bw. Jan Eliasson akisalimiana na  Mhe. Anne Makinda ( Mb) Spika wa Bunge  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania



 

Na Mwandishi Maalum, New York

Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, amesema,  kutokana  na dunia kukabiliwa   na   matatizo mengi    na ambayo yanatokea kwa wakati mmoja.Kuanzia  mlipuko wa  Ebola,    vita na machafuko ,  ugadi, uhalifu wa kupangwa na  mabadiliko ya tabia nchi.  Hakuna nchi ambayo inaweza kujidai kwamba  inaweza kusimama peke yake.

Ameyasema hayo siku ya jumanne wakati alipokuwa akibadilishana  mawazo na  wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa  Nne wa Dunia wa Maspika wa Mabunge, mkutano utakaofanyika mwezi Agosti,  2015 Jijini  New York.

Spika wa  Bunge la  Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne  Makinda ( Mb) ni  kati ya wajumbe  wa  Kamati hiyo ya Maandalizi ambayo imekutana kwa siku mbili   hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Ban Ki Moon, amewaambia Maspika hao  kwamba, dunia hivi sasa inakabiliwa na matatizo mengi sana  na  kuwa   baadhi yake  yanasababishwa kwa  viongozi kutosikiliza sauti za wananchi wao.

“ kuna matatizo mengi yanayotokea na mengine yanatokea  kwa sababu  viongozi hawasikilizi sauti za wananchi wao. Kuna pengo kubwa kati ya wananchi na viongozi wao”. amesema   Katibu Mkuu.

Na kwa sababu hiyo amesema, maspika wa mabunge na wabunge wao wanayonafasi kubwa ya kuepusha baadhi ya matatizo kwa kufikisha sauti na wananchi waliowachagua kwa viongozi wao.

Amesema bila ya  ushirikiano ndani ya taifa kama nchi moja moja na katika ngazi ya kimataifa hakuna nchi ambayo inaweza kuhimili   changamoto zinazotokana na matatizo  ya aina yoyote ile.

“ Hakuna nchi inayoweza kusimama peke yake,  wote lazima tushirikiane na kuwa kitu kimoja, lazima  sote tuonyesha utashi wa kisiasa,  tusaidiane kwa raslimali tulizonazo, tufanya kazi kwa pamoja  ili kuyashaghulikia matatizo tuliyonayo” amesema Ban Ki Moon.

Akatoa mfano wa   mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kama  moja  ya   tatizo kubwa ambalo siyo tu  limeleta madhara makubwa bali pia   athari zake zimeleta mtikisiko mkubwa katika sekta nzima ya afya.

Amesema kutokana kasi  ya  kusambaa kwa ugonjwa huo na athari zake  kiuchumi, kijamii na kimaendeleo ni wazi kwamba, pasipo kuwa na nguvu ya pamoja,  ushirikiano thabiti  wa   raslimali tulizo nazo hakuna nchi iwe kubwa kiasi gani au ndogo inayoweza kujihakikisha usalama dhidi ya ugonjwa huo.

Akizungumzia nafasi ya   Maspika na   Mabunge wanayoyaongoza  katika kukabiliana na matatizo yanayoikabili dunia hivi sasa iwe katika  ngazi ya  nchi husika au katika ngazi ya kimataifa. Ban  Ki Moon alikuwa na haya ya kusema.

“ Nyinyi mnawakilisha wananchi waliowachagua,  mnawakilisha sauti zao, ninayoheshima kubwa sana kwenu  pamoja na kazi mnazozifanya”

Akawachekesha  maspika hao kwa kusema, katika maisha yake yote ya utumishi hajawahi kufikilia kuwa mbunge ingawa amekuwa na uhusiano mzuri na wanasiasa.

Amesema  pamoja  na kuwa wawakilishi wa wananchi, wabunge ndio wanaopitisha bajeti za serikali zao  ikiwa ni pamoja na kupitisha mikataba ya kimataifa. 

Na hivyo   amewataka wabunge hao kushirikiana kwa karibu  na serikali zao na hasa katika  kupindi  kijacho ambacho serikali  zitakuwa zikijianda na utekelezaji wa  ajenda na malengo   mapya  ya maendeleo endelevu   baada ya  2015.

“ Hata kama serikali  zitakuwa na mipango mizuri , kama bunge halitapitisha bajeti  inayotakiwa ni wazi kwamba mipango hiyo haitaweza kutekelezwa kwa ukamilifu, kwa hiyo moja ya rai yangu kwenu   shirikianeni na serikali ili muweze kuwaletea wananchi wenu maendeleo endelevu” amesisitiza Katibu Mkuu.

Katika hatua nyingine  Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw Jan Eliasson akibadilishana mawazo na  wajumbe wa kamati  hiyo ya Maandalizi  amesema hakuna mtu anayeweza kufanya kila kitu  lakini kila mtu anaweza kufanya jambo  fulani.

Naibu  Katibu  Mkuu katika mazugumzo yake  pamoja na  mambo mengine ametilia sana  mkazo  umuhimu wa amani,  usalama, utawala wa sheria na demokrasia kama  baadhi ya nguzo za maendeleo.

Akasema   yapo mambo   muhimu ambayo mwananchi wa kawaida anayataka ambayo ni amani, maendeleo,  serikali na taasisi anazoziamini, ushiriki na sauti yake kusikika katika mambo yenye maslahi kwake.

“ Wananchi wanatuangalia sisi viongozi wao, je tunawashuri  ipasavyo, je tunazingatia maslahi yao. Wananchi   wa leo  siyo wale wazamani, wanauelewa   na ufahamu mkubwa wa mambo  yanayowazunguka na teknolojia ya mawasiliano imewaongezea   uelewa huo. Wanajua nini  wanachokitaka na nini wanakitarajia kutoka kwa viongozi wao” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Amewataka  Maspika, wabunge  pamoja na mihimili mingine ya dola kuwa na  mtizamo  mpya na fikra mpya na pana zaidi za siyo tu kushughulikia matatizo ya wananchi wao lakini pamoja na matatizo mbalimbali yanayoikabili dunia hivi sasa.

Na kuongeza kuwa kila mtu katika nafasi yake iwe serikali, bungeni, katika sekta binafsi au katika asasi zisizo za kiserikali anaowajibu  anaotakiwa kuutekeleza. Na kwamba makundi  hayo na mengine mengi  ya kijamii kwa umoja wao yanatakiwa kuingia katika kipindi kipya  cha ushirikiano na mshikamano.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.