STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
4.11.2014

NORWAY
imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi
ya maendeleo na kueleza kufarajika kwake
na utekelezaji wa miradi iliyofadhiliwa na nchi hiyo hapa Zanzibar kwa jinsi
ilivyopata mafanikio.
Balozi mpya wa
Norway Bibi Hanne Marie Kaarstad
aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo
yake Balozi Kaarstad alimueleza Dk. Shein kuwa Norway inajivunia mafanikio
yaliopatikana hapa Zanzibar katika miradi yake yote iliyoiunga mkono Zanzibar
ukiwemo mradi mkubwa wa umeme kutoka Pangani Tanga hadi Wesha, kisiwani Pemba.
Aidha, Balozi
huyo wa Norway alieleza kuwa mbali ya mradi huo mradi wa kusambaza maji
vijijini nao umepata mafanikio makubwa hatua ambayo imeweza kukuza uchumi na
kuimarisha sekta za maendeleo kwa wananchi wa vijijini.
Kutokana na hatua
hiyo, sambamba na mafanikio makubwa yaliopatikana katika miradi mbali mbali ambayo
Norway imesaidia hapa nchini, Balozi Kaarstad alimueleza Dk. Shein kuwa
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imo katika orodha ya kuendelea kufaidika
na misaada ya nchi hiyo.
Alisema kuwa nchi
yake hivi sasa imetenga nchi maalum ambazo itaendelea kuzisaidia na kuziunga
mkono katika kuimarisha miradi ya maendeleo kutokana na juhudi kubwa ilizopiga katika
kuendeleza miradi yake ambayo Tanzania ikiwemo Zanzibar tayari imepiga hatua
kubwa kwa hilo.
Pamoja na hayo,
Balozi huyo wa Norway alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria
utaendelezwa na kuimarishwa na nchi yake huku akisisitiza kuwa nchi yake
itaendelea kuunga mkono miradi mbali mbali hapa Zanzibar.
Kwa upande wa
uimarishaji wa sekta ya uvuvi, Balozi huyo aliemueleza juhudi zitakazochukuliwa
na afisi yake katika kuhakikisha suala hilo nalo linapewa kipaumbele kutokana
na umuhimu wake.
Nae Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza
Balozi Kaarstad kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake
wanathamini sana ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo sambamba na
misaada ya Norway kwa Zanzibar.
Dk. Shein alisema
kuwa wananchi wa Zanzibar hasa wa kisiwa
cha Pemba kamwe hawatosahau juhudi za nchi hiyo katika kuiunga mkono Zanzibar
kwa kuhakikisha kisiwa hicho kinapata umeme wa uhakika.
Alisema kuwa
kutokana na kuwepo kwa umeme huo wa uhakika ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji
katika kisiwa hicho huku akieleza mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia mradi
wa Shirika la Misaada la Norywa NORAD kwa awamu zake zote sambamba na
usambazaji wa umeme vijijini ambapo Norway ilisaidia.
Aidha,Dk. Shein
alimueleza Balozi Kaarstad kuwa azma ya Serikali anayoiongoza katika
uimarishaji wa sekta za maendeleo ni kuimarisha sekta ya uvuvi hasa wa bahari
kuu na kwa kutambua kuwa Norway imefanikiwa katika sekta hiyo aliona haja ya
kuwepo kwa mashirikiano kwa pande mbili hizo
Akizunguzia
kuhusu sekta ya afya, Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi hiyo kwa kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kupitia chuo chake
Kikuu cha Haukland kilicho Norway kwa mashirikiano mazuri kati yake na Hopitali
Kuu wa Mnazimmoja.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa Norway kwa kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia uimarishaji wa Chuo cha Kilimo kiliopo
Kizimbani, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akimueleza
mafanikio yaliopatikana katika uimarishaji wa amani na utulivu hapa nchini, Dk.
Shein alisema kuwa kuwepo kwa amani na utulivu ndio sababu kubwa inayowapelekea
watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar sanjari na
wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment