Na Kija Elias, Moshi
Wauguzi wa zamu katika kituo
cha afya cha Pasua kilichopo manispaa ya Moshi, wanatuhumiwa kumtolea lugha chafu mama mjamzito ikiwemo
pia kumnyima kitanda na hivyo kujifungulia nje ya baraza ya nyumba ya
jirani muda mfupi baada ya kufukuzwa
kituoni hapo.
Mama huyo Josephine Michael
(21), mkazi wa kata ya Kaloleni, manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro alikumbwa
na mkasa huo Novemba 29 mwaka huu, baada ya kufika kituoni hapo kwa ajli ya
kupatiwa msaada wa kujifungua lakini katika hali isiyokuwa ya kiutu aliambulia
kufukuzwa na wauguzi hao wa zamu.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana, mama huyo alisema baada ya kufika katika kituo hicho cha afya, majira ya saa mbili usiku na kuwaeleza
wauguzi hao wa zamu juu ya kile
kilichokuwa kinamsibu, alielezwa kuwa hakuna kitanda kwa watu ambao si
wagonjwa.
Alisema baada ya kuambulia majibu
hayo, aliondoka kurejea nyumbani kwake na alipofika nyumbani hali yake
ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo kukimbilia kwa majirani kuomba msaada ambapo
kabla ya kupatiwa msaada huo na majirani mfuko wa uzazi ulipasuka.
Miongoni mwa waliojitoa muhanga
kuokoa uhai wa mama huyo pamoja na mtoto wake ni mwandishi wa habari, Safina
Sarwatt (Mtanzania), ambaye alilazimika kutumia mwanga wa simu yake ya
kiganjani kumzalisha mama huyo akishirikiana na majirani zake.
“Mama huyo alikuja kwenye kibaraza chetu huku akiomba msaada wa kujifungua, tulipo mwangalia
tulimkuta yupo katika hatua za mwisho kujifungua ndipo tulipotoka na kumtandikia khanga chini
na kuanza kumsaidia ambapo alifanikiwa
kujingua mtoto wa kiume akiwa salama,”alisema Sarwatt.
Sarwatt alisema licha ya
kutokuwa na utaalamu wowote aliendelea kutoa msaada huo na kumkimbiza katika
kituo cha afya cha Pasua.
“Tulipomaliza kumzalisha mama huyo
tulilazimika kufunga kitovu cha mtoto
kwa kutumia mfuko wa rambo, kutokana na kutokuwa na vifaa tiba na kisha
kumkimbiza hospitali kwa matibabu zaidi,”alisema.
Aidha alisema wakati wakimpatia
msaada huyo, umeme ulikatika na hivyo kuwa na giza ndipo walipolazimika kutumia
mwanga wa simu ya kiganjani ili kumsaidia mama huyo asipoteze uhai wake.
Akizungumza mama huyo akiwa
katika kituo cha afya cha Pasua wodi ya watoto, alimpongeza mwandishi huyo kwa
kuwa na moyo wa kipekee kwani ni watu
wachache ambao wanaweza kujitolea.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji
wa manispaa ya Moshi,Shaaban Ntarambe, hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa
kile alichodia suala hilo ni la kitaalamu na kuwataka waandishi wa habari
kuandika maswali ili ayawasilishe kwa wataalamu wake wa idara ya afya.
No comments:
Post a Comment