Habari za Punde

Barabara Dar Kuendelea Kuimarishwa.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO Dar.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Mecki Sadiki amewataka wahandisi wanaosimamia ujenzi wa miradi ya barabara katika jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanawasimamia ipasavyo wakandarasi wanaojenga miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa viwango na muda uliopangwa na kuwaondolea wananchi adha ya usafiri inayotokana na ubovu wa barabara.

Aidha,amezitaka Mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo mbalimbali katika jiji la Dar es salaam kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaovunja sheria kwa kujenga majengo na kuta katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuziba mifereji ya maji  na  kubomoa kingo za mito hali inayosababisha mafuriko katika makazi ya watu wakati wa msimu wa mvua.

Akifungua kikao cha kwanza cha wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kilichofanyika leo jijini Dar es salaam kujadili na kutathmini utekelezaji  wa miradi ya barabara kwa mwaka 2014/2015 Bw. Sadiki  amesema kuwa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam yamekuwa yakikumbwa na mafuriko  kutokana na ujenzi holela katika mikondo ya maji, uharibifu wa kingo za mito, na uzibaji wa mifereji unaofanywa na baadhi ya watu kwa kujenga kuta jambo linalosababisha  uharibifu wa miundombinu kutokana na mafuriko wakati wa mvua.


Amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya barabara katika jiji la Dar es salaam, zaidi ya shilingi bilioni 88 zimependekezwa kuidhinishwa  katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa lengo la kufanya ukarabati wa kawaida, matengenezo ya barabara za zamani na mpya kwa kiwango cha lami na ujenzi  madaraja mapya na yale yaliyoharibiwa wakati wa msimu uliopita wa mvua.

Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti wameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu iliyoharibiwa vibaya wakati wa msimu wa mvua uliopita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam,  ujenzi wa barabara ya Uhuru,Daraja la Kinyerezi, Ujenzi wa kituo cha mabasi eneo la 
Machinga Complex, utekelezaji wa mradi wa barabara ya Shingofeni, 

Barabara ya Mombasa –Moshi bar na ujenzi wa barabara ya Ulongoni A kuelekea Kilimani.

Wamesema kuwa juhudi za usafi wa mito, madaraja na mifereji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam lazima iwe shirikishi ili mafanikio ya kuliweka jiji katika hali ya usafi  na usalama wakati wa  msimu wa mvua yaweze kuonekana na kuwaondolea usumbufu wananchi.


Aidha, wamezitaka mamlaka zinazohusika katika manispaa za za Ilala, Temeke na Kinondoni kuanisha maeneo yote hatarishi katika halmashauri zao ambayo wananchi wamevamia  mito kwa kujenga na kuharibu kingo za mito  waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.